YouVersion Logo
Search Icon

Zaburi 37

37
Kufanikiwa kwa waovu kusikufadhaishe
(Zaburi ya Daudi)
1Usihangaike kwa sababu ya waovu;
usiwaonee wivu watendao mabaya.
2Maana hao watatoweka mara kama nyasi;
watanyauka kama mimea mibichi.
3Mtumainie Mwenyezi-Mungu na kutenda mema,
upate kuishi katika nchi na kuwa salama.
4Uitafute furaha yako kwa Mwenyezi-Mungu,
naye atakujalia unayotamani moyoni.
5Mkabidhi Mwenyezi-Mungu maisha yako;
mtumainie yeye naye atafanya kitu.
6Ataufanya wema wako ungae kama mwanga,
na uadilifu wako kama jua la adhuhuri.
7Tulia mbele ya Mwenyezi-Mungu, mngojee kwa saburi;
usihangaike juu ya wale wanaofanikiwa,
watu wanaofaulu katika mipango yao mibaya.
8Epuka hasira wala usiwe na ghadhabu;
usihangaike maana hiyo huzidisha ubaya.
9Watu watendao mabaya wataangamizwa,
bali wanaomtumaini Mwenyezi-Mungu wataimiliki nchi.
10Bado kitambo kidogo, naye mwovu atatoweka;
utamtafuta pale alipokuwa, wala hutamwona.
11 # Taz Mat 5:5 Lakini wapole wataimiliki nchi,
hao watafurahia wingi wa fanaka.
12Mwovu hula njama dhidi ya mwadilifu,
na kumsagia meno kwa chuki.
13Lakini Mwenyezi-Mungu humcheka mwovu,
kwani ajua mwisho wake u karibu.
14Waovu huchomoa panga na kuvuta pinde zao,
wapate kuwaua maskini na fukara;
wawachinje watu waishio kwa unyofu.
15Lakini panga zao zitawapenya wao wenyewe,
na pinde zao zitavunjwavunjwa.
16Afadhali mali kidogo ya mtu mwadilifu
kuliko utajiri wa watu waovu wengi.
17Maana nguvu za waovu zitavunjwa,
lakini Mwenyezi-Mungu huwategemeza waadilifu.
18Mwenyezi-Mungu hutunza maisha ya watu waaminifu,
na urithi wao utadumu milele.
19Hawataaibika zikifika nyakati mbaya;
siku za njaa watakuwa na chakula tele.
20Lakini waovu wataangamia,
maadui za Mwenyezi-Mungu watanyauka kama maua nyikani;
naam, watatoweka kama moshi.
21Mtu mwovu hukopa bila kurudisha;
lakini mwadilifu hutoa kwa ukarimu.
22Waliobarikiwa na Mwenyezi-Mungu wataimiliki nchi,
lakini waliolaaniwa naye watafutiliwa mbali.
23Mwenyezi-Mungu huziongoza nyayo za mtu,
humlinda yule ampendezaye.
24Ajapoanguka, haanguki akabaki chini,
kwa sababu Mwenyezi-Mungu humtegemeza.
25Nilikuwa kijana na sasa ni mzee;
kamwe sijaona mwadilifu ameachwa na Mungu,
au watoto wake wakiombaomba chakula.
26Daima huwapa wengine kwa furaha na kukopesha,
na watoto wake ni baraka.
27Achana na uovu, utende mema,
nawe utaishi nchini daima;
28maana Mwenyezi-Mungu hupenda uadilifu,
wala hawaachi waaminifu wake.
Huwalinda hao milele;
lakini wazawa wa waovu wataangamizwa.
29Waadilifu wataimiliki nchi,
na wataishi humo milele.
30Mtu mwadilifu husema maneno ya hekima,
kwa ulimi wake hunena yaliyo ya haki.
31Huizingatia moyoni mwake sheria ya Mungu wake;
naye hatetereki katika mwenendo wake.
32Mtu mwovu humvizia mtu mwema na kujaribu kumuua;
33lakini Mwenyezi-Mungu hatamtia mtu mwema makuchani mwake,
wala kumwacha apatilizwe akishtakiwa.
34Mtumainie Mwenyezi-Mungu na kushika njia yake,
naye atakukuza uimiliki nchi,
na kuwaona waovu wakiangamizwa.
35Nilimwona mwovu mdhalimu sana,
alijiweka juu ya wote kama mierezi ya Lebanoni!
36Baadaye nikapita hapo, naye hakuwapo tena;
nikamtafuta, lakini hakuonekana tena.
37Mwangalie mtu mwema, mtu mwadilifu;
mtu anayependa amani hujaliwa wazawa.
38Lakini wakosefu wote wataangamizwa;
na wazawa wao watafutiliwa mbali.
39Mwenyezi-Mungu huwaokoa waadilifu,
na kuwalinda wakati wa taabu.
40Mwenyezi-Mungu huwasaidia na kuwaokoa;
huwatoa makuchani mwa waovu na kuwaokoa,
maana wanakimbilia usalama kwake.

Currently Selected:

Zaburi 37: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy