YouVersion Logo
Search Icon

Yoshua Mwana wa Sira 43

43
Ubora wa Jua
1Fahari ya huko juu ni kweu angani,
Kuba ya mbingu uonapo utukufu wake.
2Jua lizukapo huleta habari liendavyo;
Jinsi zinavyotisha kazi zake Aliye Juu!
3Wakati wa adhuhuri huikausha nchi,
Naye ni nani atakayehimili joto lake kali?
4Tanuri iliyopuliziwa huyeyusha madini; lakini vianga vya jua huiunguza milima, na ndimi zake hutoa mafukuto ya moto, na mwangaza wake hupofusha macho. 5BWANA ndiye mkuu, ambaye amelihuluku; tena kwa neno lake lahimiza mwendo wake.
Ubora wa Mwezi
6Mwezi nao pia huangaza kwa wakati wake, ili kutawala nyakati, na kuwa ishara ya ulimwengu.
7Kutoka kwa mwezi ni dalili ya sikukuu;
Nuru yake hupungua ukipita mwezi mpevu.
8Mwezi nao huitwa kwa jina lake;
Ukikua kwa ajabu ulivyobadilika;
Mwanga wa ajabu kati ya majeshi ya juu,
Ung'aapo katika anga la mbinguni.
Utukufu wa Nyota na Upinde wa Mvua
9Uzuri wa mbingu ndio fahari ya nyota, safusafu za kutoa nuru katika mahali pa BWANA palipo juu sana. 10Kwa neno lake Aliye Mtakatifu husimama taratibu, wala hazitasinzia mnamo mikesha yake.
Upinde wa mvua
11Uuangalie upinde wa mvua, kumhimidi Yeye aliyeufanya; uzuri wake unazidi sana katika mng'ao wake. 12Unaizungusha kuba ya mbingu duara ya fahari; nayo ndiyo mikono yake Aliye Juu iliyoupinda.
Maajabu ya Asili
13Kwa nguvu zake Yeye hutoa umeme, na kuvimemetesha vimulimuli vyake katika hukumu. 14Kwa amri yake hazina zafunguliwa, na mawingu yatoka ili kuruka kama ndege. 15Kwa uweza wake mkuu huyafanya mawingu kuwa magumu, na mvua ya mawe huvunjiwa mawe yake madogo. 16Sauti ya ngurumo yake huitetemesha nchi, na kwa kutokea kwake milima itatikisika. Kwa mapenzi yake kusi itavuma, 17pia na tufani ya kaskazi, na kimbunga. 18Mfano wa ndege wakiruka chini hunyunyiza theluji, na mfano wa nzige wakitua ndivyo inavyoanguka; jicho litashangaa kwa ajili ya uzuri wa weupe wake, na moyo utastaajabu kwa jinsi inavyonyesha. 19Sakitu tena huimimina juu ya nchi kama chumvi, na kuvifanya vijiti kuchanua maua mfano wa vito. 20Kisha huvumisha upepo wa baridi, na barafu itaganda juu ya maji; itayakalia kila makusanyiko ya maji, nayo maji yataivaa kana kwamba ni deraya. 21Huiunguza mimea ya milimani, na kuikausha nyika, na majani yote ya kondeni, kama moto. 22Ukungu ukitanda kama mawingu ni kupona vitu vyote; kama umande baada ya joto utaleta furaha. 23Kwa shauri lake amevituliza vilindi, na kupanda visiwa ndani yake. 24Wale wasafirio baharini hunena upana wake, na sisi tusikiapo kwa masikio yetu twamaka mno. 25Ndimo viendamo vile viumbe vya kigeni vya ajabu, jamii ya vyote vyenye uhai, yaani, viumbe vya vilindini vyenye nguvu.
26Kwa kusudi lake huifanikisha kazi yake,
Na kwa neno lake vyote vimekuwapo.
27Tuseme maneno mengi; hatutadiriki;
Jumla ya maneno ni, Ndiye vyote.
28Sisi tupateje uwezo wa kumtukuza?
Mradi ndiye Mkuu juu ya kazi zake zote.
29BWANA hutisha sana, naye ni mkuu mwenye kupita vitu vyote; naam, uweza wake ni wa ajabu. 30Mkija kumtukuza BWANA, mhimidini kadiri mwezavyo, maana hata hivyo kuna zaidi; mtakapomwadhimisha, tumieni nguvu zenu zote, maana hamtadiriki. 31Ni nani aliyemwona, hata aweze kumdhihirisha? Ni nani awezaye kumkuza alivyo? 32Mambo mengi sana yamefichwa, makubwa kupita hayo; maana tulizoziona ni chache tu katika kazi zake. 33Kwa kuwa BWANA ameviumba vitu vyote vilivyopo, nao wamchao amewapa hekima.

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy