YouVersion Logo
Search Icon

Yoshua Mwana wa Sira 44

44
Wimbo wa Kuwaenzi Wakale
1Haya na tuwasifu watu wa utauwa,
Na baba zetu katika vizazi vyao.
2BWANA aliwafanyizia utukufu mwingi,
Walio mashuhuri tangu siku za kale.
3Wale waliotawala katika milki zao,
Maarufu kwa kuwa walikuwa hodari;
Wale waliotoa mashauri kwa akili zao,
Na kuhubiri mambo kwa unabii wao;
4Wakuu wa mataifa kwa ajili ya mawaidha,
Waliowafaa watu kwa kuona mbele.
Wenye hekima katika mafundisho yao,
Wakitunga mithali za kupokezanya;
5Wenye kuvumbua nyimbo na ngoma,
Nao waliobuni tenzi kwa kuandika;
6Watu walekevu wenye majaliwa,
Ambao walistarehe katika makao yao;
7Hao wote walisifiwa katika vizazi vyao,
Na kutukuzwa katika siku zao.
8Baadhi yao waliacha jina nyuma yao,
Hata watu watangaze sifa zao;
9Baadhi yao hawana kumbukumbu,
Wamepotea kana kwamba hawakuwako;
Wamekuwa kana kwamba hawakuzaliwa,
Wala watoto wao baada yao;
10Lakini hawa walikuwa watu wa utauwa,
Wala kazi zao za haki hazisahauliki.
11Wema wao utawadumia wazao wao,
Na urithi wao una wana wa wana;
12Wazao wao wanashikamana na agano,
Na watoto wao kwa ajili yao.
13Kumbukumbu lao litadumu milele,
Wala haki yao haifutiki kamwe;
14Miili yao imezikwa katika amani,
Na jina lao laishi hata vizazi vyote.
15Mkutano wa watu wataitangaza hekima yao,
Na makusanyiko watazihubiri sifa zao.
Enoko
16 # Mwa 5:24; Ebr 11:5; Yud 14 Henoko alionekana kuwa mkamilifu, akaenda pamoja na BWANA, akatwaliwa naye; mfano wa kujuana naye hata vizazi vyote.
Nuhu
17 # Mwa 6:9—9:17 Nuhu mwenye haki alionekana amekamilika; wakati wa ukiwa mtupu akapata kuwa mbegu ya kufanya upya wanadamu; kwa ajili yake kukawa na mabaki hapo palipokuja gharika. 18Tena pamoja naye likafanyika agano la milele; ya kwamba wote wenye mwili wasifutwe tena.
Abrahamu
19 # Mwa 15:1—17:27; 22:1-18 Abrahamu alikuwa baba wa mataifa mengi; wala hakupatikana mtu mfano wake kwa utukufu; 20ambaye aliishika sheria yake Aliye Juu, na Mungu alifanya agano naye. Katika mwili wake akatilia agizo, naye alipojaribiwa alionekana kuwa amini. 21Kwa hiyo Mungu akamthibitishia kwa uapo ya kwamba atawabariki mataifa katika uzao wake, na kumzidisha kama mavumbi ya nchi, na kuwainua wazao wake kama nyota; na kuwapa urithi toka bahari mpaka bahari, na toka mto mpaka miisho ya dunia.
Isaka na Yakobo
22 # Mwa 17:19; 26:3-5; 27:28; 28:14 Kwa Isaka naye akalifanya kuwa thabiti, kwa ajili ya Abrahamu, baba yake. 23Agano la wazazi wake akampa, na baraka ilikaa juu ya kichwa cha Israeli. Akamthibitisha katika baraka zake, akampa urithi wake. Akaugawa urithi huo sehemu zake katikati ya makabila kumi na mawili; na kutoka kwake akamtokeza Yusufu, mtu wa rehema, mwenye kibali mbele ya wote wenye mwili.

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy