YouVersion Logo
Search Icon

Yoshua Mwana wa Sira 42

42
1Lakini mambo haya usiyatahayarikie, wala usimjali mtu yeyote, hata kutenda dhambi hivyo; 2torati yake Aliye Juu, na agano lake; na haki, uwafanyie wahalifu hukumu; 3kufanya hesabu na mshiriki na mawakili; na kupata ada itokayo katika urithi ilivyo haki; 4uhalisi wa mizani na mawe; mapato ama makubwa ama madogo; 5kufanya biashara na wachuuzi bila upendeleo; kuwarudi watoto sawasawa, na kumpiga mtumwa mbaya hata akitoka damu. 6Akiwapo mke aliye mwovu, kumlinda salama ni kuzuri; tena ufunge sana; ikiwapo mikono mingi. 7Kwa habari yoyote ya kuweka amana na iwe kwa hesabu na kwa kipimo; na kuhusu kutoa na kupokea mambo yote na yawe yameandikwa. 8Usitahayari kumfundisha aliye mjinga na baradhuli, hata na mtu mwenye mvi, mzee sana, akibishana na watoto. Hivyo utakuwa mwenye akili kweli kweli, na kuona kibali machoni pa kila mtu aliye hai.
Binti na Baba
9 # Sira 7:24-25; 26:10-12 Binti ni tunu ya siri kwa babaye amfanyaye asilale unono; maana kujisumbua kwa ajili yake hufukuza usingizi; akiwa ni msichana, asije akapita uzuri wa ujana wake; akiwa ameolewa, asije akachukiwa; 10akiwa ni bikira, asije akaharibiwa; akiwa ana mume, asije akawa mzinifu; nyumbani mwa babaye asije akapata mimba; nyumbani mwa mumewe asije akawa tasa. 11Umlinde sana binti aliye mshupavu, asije akakufanya mzaha kwa adui zako; kudharauliwa na watu wa mjini; mbayana miongoni mwa akina yahe; akakutia fedheha malangoni mbele ya makutano.
Wanawake
12Akaapo kisiwepo kizuizi cha kimia, wala alalapo yasiwepo maingilio. Asimwoneshe mtu yeyote uzuri wake, wala asiketi kudakua na wanawake wazima; 13kwa kuwa kutoka kwa mavazi huonekana nondo, na kutoka kwa mwanamke uovu wake. 14Ni afadhali ubaya wa mwanamume kuliko ubembe wa mwanamke, naam, wa binti atakayekuletea lawama na aibu.
UTUKUFU WA MUNGU
Kazi za Mungu
15Sasa nitayanena matendo ya BWANA, nami nitayadhihirisha mambo yake niliyoyaona. Kwa neno la BWANA vimekuwapo viumbe vyake, na kazi impendezayo ni sawasawa na amri yake. 16Jua litoapo nuru hudhihirika mahali pote; na kazi ya BWANA imejaa utukufu wake. 17Watakatifu wa Mungu hawawezi kuyatangaza maajabu ya miujiza yake, lakini Mungu amewapa majeshi yake uwezo wa kusimama mbele ya utukufu wake. 18Yeye huchunguza vilindi, na moyo wa binadamu, na kuyatambua mashauri yake ya siri; kwa maana Aliye Juu amaizi yote yaliyo ujuzi, naye hupenya ishara za ulimwengu, 19hutujulisha yaliyopita, na yatakayokuja, na kuzifunua alama za mambo yaliyofichwa. 20Hakuna wazo asilolijua, wala hakuna neno lolote ambalo limefichwa naye. 21Matendo makuu ya hekima yake ameyaratibisha, ambaye Yeye ni mmoja tu, tangu milele na hata milele; hakuzidishiwa kitu, wala kupunguziwa kitu; wala Yeye hana haja yoyote ya mshauri. 22Ee ajabu ya uzuri wa viumbe vyake! Mtu angeweza kuliona hilo hata kwa habari ya cheche. 23Vitu vyote vyaishi na kudumu daima, na kwa kila haja vyote vyamtii. 24Vyote vinahitilafiana, wala hakufanya chochote kisicho kamili; 25hata kimoja kinapita kingine kwa uzuri uzidio; naye ni nani atakayekinai kwa kuutazama utukufu wake?

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy