YouVersion Logo
Search Icon

Marko 15

15
Yesu mbele ya Pilato
1 # Mt 27:1-2; Lk 22:66; 23:1; Yn 18:28 Mara kulipokuwa asubuhi wakuu wa makuhani walifanya shauri pamoja na wazee na waandishi na baraza nzima, wakamfunga Yesu, wakamchukua, wakamleta mbele ya Pilato. 2#Mt 27:11-30; Lk 23:2-25; Yn 18:29—19:16 Pilato akamwuliza, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu, akamwambia, Wewe wasema. 3Nao wakuu wa makuhani walikuwa wakimshitaki mambo mengi. 4Pilato akamwuliza tena akisema, Hujibu neno? Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki! 5#Mk 14:61; Isa 53:7 Wala Yesu hakujibu neno tena, hata Pilato akastaajabu.
Pilato amtoa Yesu asulubiwe
6Basi wakati wa sikukuu huwafungulia mfungwa mmoja, wamwombaye. 7Palikuwa na mtu aitwaye Baraba, aliyefungwa pamoja na waasi, waliosababisha mauaji katika uhalifu huo. 8Makutano wakaja, wakaanza kuomba awafanyie kama vile alivyozoea. 9Pilato akawajibu, akisema, Je! Mnataka niwafungulie mfalme wa Wayahudi? 10#Yn 11:48; 12:19; Mt 21:38 Kwa maana alitambua ya kuwa wakuu wa makuhani wamemtoa kwa husuda. 11Lakini wakuu wa makuhani wakawachochea watu, kuwa afadhali awafungulie Baraba. 12Pilato akajibu tena akawaambia, Basi nimtendeje huyu mnayemnena kuwa ni mfalme wa Wayahudi? 13Wakapiga kelele tena, Msulubishe. 14Pilato akawaambia, Kwani ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, Msulubishe. 15Pilato kwa kupenda kuwaridhisha watu, akawafungulia Baraba; akamtoa Yesu, baada ya kumpiga mijeledi, ili asulubiwe.
Askari wamdhihaki Yesu
16Nao askari wakamchukua ndani ya behewa, ndiyo Praitorio (yaani, makao makuu ya mtawala), wakakusanya pamoja kikosi kizima. 17Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji la miiba, wakamtia kichwani; 18wakaanza kumsalimu, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! 19Wakampiga mwanzi wa kichwa, wakamtemea mate, wakapiga magoti, wakamsujudia. 20#Mt 27:31-56; Lk 23:26-49; Yn 19:16-30 Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua lile vazi la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe; wakampeleka nje ili wamsulubishe.
Kusulubiwa kwa Yesu
21 # Rum 16:13 Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashambani, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake. 22Wakamleta mpaka mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa. 23#Zab 69:21 Wakampa mvinyo iliyotiwa manemane, asiipokee. 24#Zab 22:18 Wakamsulubisha, wakagawa mavazi yake, wakayapigia kura kila mtu atwae nini. 25Basi ilikuwa saa tatu, nao wakamsulubisha. 26Palikuwa na anwani ya mashitaka yake iliyoandikwa juu, MFALME WA WAYAHUDI. 27Na pamoja naye walisulubisha wanyang'anyi wawili, mmoja mkono wake wa kulia na mmoja mkono wake wa kushoto. [ 28#Isa 53:12 Basi andiko likatimizwa linenalo, Alihesabiwa pamoja na waasi.] 29#Zab 22:7; Zab 109:25; Mk 14:58; Yn 2:19 Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisatikisa vichwa, wakisema, Ahaa! Wewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga katika siku tatu, 30jiponye nafsi yako, ushuke msalabani. 31Kadhalika na wakuu wa makuhani wakamdhihaki wao kwa wao, pamoja na waandishi, wakisema, Aliponya wengine; hawezi kujiponya mwenyewe. 32#Mt 16:1,4 Kristo, mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani tupate kuona na kuamini. Hata wale waliosulubiwa pamoja naye wakamsuta.
Kifo cha Yesu
33 # Amo 8:9 Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hadi saa tisa. 34#Zab 22:1 Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? 35Na baadhi yao waliosimama pale, walisema, Tazama, anamwita Eliya. 36#Zab 69:21 Na mmoja akaenda mbio, akajaza sifongo siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha, akisema, Acheni, na tuone kwamba Eliya anakuja kumteremsha. 37Naye Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho.
38 # Kut 26:31-33 Pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hadi chini. 39Basi yule kamanda, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu. 40#Lk 8:2-3 Palikuwako na wanawake wakitazama kwa mbali; miongoni mwao alikuwemo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, na Salome; 41hao ndio waliofuatana naye huko Galilaya, na kumtumikia; na wengine wengi waliopanda pamoja naye mpaka Yerusalemu.
Kuzikwa kwa Yesu
42 # Mt 27:57-61; Lk 23:50-55; Yn 19:38-42 Ilipofika wakati wa jioni, kwa sababu ni Maandalio, ndiyo siku iliyo kabla ya sabato, 43akaenda Yusufu, mtu wa Arimathaya, mstahiki, mtu wa baraza ya mashauri, naye mwenyewe anautazamia ufalme wa Mungu; akafanya ujasiri, akaingia mbele ya Pilato akauomba mwili wake Yesu. 44Lakini Pilato akastaajabu, kama amekwisha kufa. Akamwita yule kamanda, akamwuliza kwamba amekufa kitambo. 45Hata alipokwisha kupata hakika kutoka kwa yule kamanda, alimpa Yusufu yule maiti. 46Naye akanunua sanda ya kitani, akamteremsha, akamfungia ile sanda, akamweka katika kaburi lililochongwa mwambani; akavingirisha jiwe mbele ya mlango wa kaburi. 47Nao Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yose wakapatazama mahali alipowekwa.

Currently Selected:

Marko 15: SRUVDC

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy