YouVersion Logo
Search Icon

Marko 14

14
Mpango wa kumwua Yesu
1 # Mt 26:1-5; Lk 22:1-2 Baada ya siku mbili ilikuwa sikukuu ya Pasaka, na mikate isiyochachwa; wakuu wa makuhani na waandishi wakatafuta njia ya kumkamata kwa hila na kumwua.#Kut 12:1-27 2Kwa maana walisema, Isiwe kwa wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu.
Kupakwa mafuta katika Bethania
3 # Mt 26:6-13; Yn 12:1-8 Naye alipokuwapo Bethania, nyumbani mwa Simoni mwenye ukoma, akiwa amekaa mezani, alikuja mwanamke mwenye chupa ya marhamu yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa; akaivunja chupa akaimimina kichwani pake.#Lk 7:37-38 4Palikuwa na watu waliochukizwa katika nafsi zao wakisema, Kwa nini kupoteza marhamu namna hii? 5Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa dinari mia tatu na kuzidi, wakapewa maskini. Wakamnung'unikia sana yule mwanamke. 6Yesu akasema, Mwacheni; mbona mnamsumbua? Amenitendea kazi njema; 7#Kum 15:11 maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema; lakini mimi hamko nami sikuzote. 8Ametenda alivyoweza; ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko. 9Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake.
Yuda akubali kumsaliti Yesu
10 # Mt 26:14-16; Lk 22:3-6 Yuda Iskarioti, yule mmoja katika wale Kumi na Wawili, akaenda zake kwa wakuu wa makuhani, apate kumsaliti kwao. 11Nao waliposikia walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Akatafuta njia ya kumsaliti wakati wa kufaa.
Pasaka pamoja na wanafunzi
12 # Mt 26:17-19; Lk 22:7-13 Katika siku ya kwanza ya mikate isiyochachwa, walipoichinja Pasaka, wanafunzi wake wakamwambia, Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile Pasaka? 13Akatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni zenu mjini; atakutana nanyi mwanamume amebeba mtungi wa maji; mfuateni; 14#Mk 11:3 na popote atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba, Mwalimu asema, Kiko wapi chumba changu cha wageni, niile Pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu? 15Naye mwenyewe atawaonesha ghorofa kubwa, iliyotayarishwa; humo tuandalieni. 16Wanafunzi wakatoka, wakaenda mjini, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa Pasaka.
17 # Mt 26:20-29; Lk 22:14-23; Yn 13:21-26 Basi ilipokuwa jioni akaja pamoja na wale Kumi na Wawili. 18#Zab 41:9 Nao walipokuwa wameketi chakulani, wakila, Yesu alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu, naye anakula pamoja nami, atanisaliti. 19Wakaanza kuhuzunika, wakamwambia mmoja mmoja, Je! Ni mimi? 20Akawaambia, Ni mmoja wa hao Kumi na Wawili, ambaye achovya pamoja nami katika kombe. 21Kwa maana Mwana wa Adamu aenda zake kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu; ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa.
Kuanzishwa kwa Chakula cha Bwana.
22 # 1 Kor 11:23-25 Nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa, akasema, Twaeni; huu ndio mwili wangu. 23Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote. 24#Kut 24:8; Yer 31:31-34; Zek 9:11 Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. 25Amin, nawaambia ninyi, Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu.
Yesu atabiri kuwa Petro atamkana
26 # Mt 26:30-35; Lk 22:31-34,39 Nao walipokwisha kuimba walitoka kwenda katika mlima wa Mizeituni.#Zab 113—118 27#Zek 13:7 Yesu akawaambia, Mtakunguwazwa ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa,
Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika.
28 # Mt 28:16; Mk 16:7 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. 29Petro akamwambia, Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi. 30#Yn 13:38 Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, Leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. 31#Yn 11:16 Naye akazidi sana kusema, Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe. Na wote wakasema vile vile.
Yesu aomba katika Gethsemane
32 # Mt 26:36-46; Lk 22:40-46 Kisha wakaja mpaka katika bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa pindi niombapo.#Yn 18:1 33Akamtwaa Petro na Yakobo na Yohana pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. 34#Yn 12:27; Zab 43:5 Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe. 35Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke. 36#Mk 10:38 Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; lakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe. 37Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja? 38Kesheni na kuomba, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu. 39Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo. 40Akaja tena akawakuta wamelala, maana macho yao yamekuwa mazito, wala hawakujua la kumjibu. 41Akaja mara ya tatu, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike; yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu anatiwa mikononi mwao wenye dhambi. 42#Yn 14:31 Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia.
Kusalitiwa na kukamatwa kwa Yesu
43 # Mt 26:47-58; Lk 22:47-55; Yn 18:2-18 Basi alipokuwa katika kusema, mara Yuda alifika, mmoja wa wale Kumi na Wawili, na pamoja naye mkutano, wakiwa na panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee. 44Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni na kumpeleka chini ya ulinzi. 45Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu. 46Wakanyosha mikono yao wakamkamata. 47Na mmoja wao waliokuwapo akafuta upanga, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. 48Yesu akajibu, akawaambia, Je! Mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang'anyi? 49#Lk 19:47; 21:37 Kila siku nilikuwa mbele yenu hekaluni nikifundisha, msinikamate; lakini haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia. 50Ndipo wakamwacha, wakakimbia wote.
51Na kijana mmoja alimfuata, akiwa amejitanda mwili wake nguo ya kitani; wakamkamata; 52naye akaiacha ile nguo ya kitani, akakimbia akiwa uchi.
Yesu mbele ya baraza la wazee
53Nao wakamchukua Yesu kwa Kuhani Mkuu; wakamkusanyikia wote, wakuu wa makuhani na wazee na waandishi. 54Naye Petro akamfuata kwa mbali, hadi ndani katika behewa ya Kuhani Mkuu; akawa ameketi pamoja na watumishi, akiota moto. 55#Mt 26:59-68; Lk 22:63-71; Yn 18:19-24 Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione. 56Kwa maana wengi walimshuhudia uongo, lakini ushuhuda wao haukupatana. 57Hata wengine wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema, 58#Yn 2:19; 4:21,23 Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono. 59Wala hata hivyo ushuhuda wao haukupatana. 60Kisha Kuhani Mkuu akasimama katikati, akamwuliza Yesu, akisema, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? 61#Mk 15:5; Isa 53:7 Lakini akanyamaza, wala hakujibu neno. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu? 62#Dan 7:13; Zab 110:1 Yesu akasema, Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kulia wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni. 63Kuhani Mkuu akararua nguo zake, akisema, Tuna haja gani tena ya mashahidi? 64#Law 24:16; Yn 19:7 Mmesikia kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wote wakamhukumu kuwa imempasa kuuawa. 65Wengine wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, na kumpiga makonde, na kumwambia, tabiri. Hata watumishi nao wakamchukua wakampiga makofi.
Petro amkana Yesu
66 # Mt 26:69-75; Lk 22:56-62; Yn 18:25-27 Na Petro alikuwa chini behewani; akaja mmoja wa vijakazi wa Kuhani Mkuu, 67akamwona Petro akiota moto; akamkazia macho, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na yule Mnazareti, Yesu. 68Akakana, akasema, Sijui wala sisikii unayoyasema wewe. Akatoka nje hadi ukumbini; jogoo akawika. 69Na yule kijakazi akamwona tena, akaanza tena kuwaambia waliosimama pale, Huyu ni mmoja wao. 70Akakana tena. Kitambo kidogo tena wale waliosimama pale wakamwambia Petro, Hakika u mmoja wao, kwa sababu u Mgalilaya wewe. 71Akaanza kulaani na kuapiza, Simjui mtu huyu mnayemnena. 72#Mk 14:30 Na mara jogoo akawika mara ya pili. Petro akalikumbuka lile neno aliloambiwa na Yesu, Kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Na alipolifikiri, akalia.

Currently Selected:

Marko 14: SRUVDC

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy