Zaburi 103:1-8
Zaburi 103:1-8 BHN
Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu; nafsi yangu yote ilisifu jina lake takatifu! Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu! Usisahau kamwe wema wake wote. Ndiye anayenisamehe uovu wangu wote, na kuniponya magonjwa yote. Ndiye aniokoaye kutoka kifoni, na kunijalia rehema na fadhili zake. Ndiye anayeniridhisha mema maisha yangu yote, hata nabaki kijana mwenye nguvu kama tai. Mwenyezi-Mungu huhukumu kwa haki; huwajalia wanaodhulumiwa haki zao. Alimjulisha Mose mwongozo wake, aliwaonesha watu wa Israeli matendo yake. Mwenyezi-Mungu ni mwenye rehema na huruma; ni mvumilivu na mwingi wa fadhili.