Yoshua 21:20-45
Yoshua 21:20-45 NENO
Koo nyingine za Wakohathi, ambao pia ni Walawi, walipewa miji kutoka kabila la Efraimu: Katika nchi ya vilima ya Efraimu, walipewa: Shekemu (mji wa makimbilio kwa yeyote anayeshtakiwa kwa mauaji) na Gezeri, Kibsaimu na Beth-Horoni, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne. Pia kutoka kabila la Dani, wakapokea: Elteke, Gibethoni, Aiyaloni na Gath-Rimoni pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne. Kutoka nusu ya kabila la Manase, wakapokea: Taanaki na Gath-Rimoni pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji miwili. Miji hii kumi, na maeneo ya malisho ya kila mji, ilipewa koo za Wakohathi zilizobaki. Koo za Walawi za Wagershoni walipewa: kutoka nusu ya kabila la Manase: Golani katika Bashani (mji wa makimbilio kwa yeyote aliyeshtakiwa kwa mauaji) na Beeshtera, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji miwili; kutoka kabila la Isakari, walipewa: Kishioni, Daberathi, Yarmuthi na En-Ganimu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne; kutoka kabila la Asheri, walipewa: Mishali, Abdoni, Helkathi na Rehobu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne. Kutoka kabila la Naftali, walipewa: Kedeshi katika Galilaya (mji wa makimbilio kwa ajili ya yeyote anayeshtakiwa kwa mauaji), Hamoth-Dori na Kartani, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji mitano. Miji yote ya koo za Wagershoni ilikuwa kumi na tatu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji. Koo za Wamerari (Walawi waliobaki) walipewa: kutoka kabila la Zabuloni: Yokneamu, Karta, Dimna na Nahalali, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne; kutoka kabila la Reubeni, walipewa: Bezeri, Yahasa, Kedemothi na Mefaathi, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne; kutoka kabila la Gadi, walipewa: Ramothi katika Gileadi (mji wa makimbilio kwa ajili ya yeyote anayeshtakiwa kwa ajili ya mauaji), Mahanaimu, Heshboni na Yazeri, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne. Miji yote waliyopewa koo za Wamerari, waliokuwa mabaki ya Walawi, ilikuwa ni kumi na mbili. Miji yote ya Walawi katika eneo lililomilikiwa na Waisraeli ilikuwa arobaini na nane, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji. Kila mji kati ya miji hii ulikuwa na maeneo ya malisho kuuzunguka; ndivyo ilivyokuwa kwa miji hii yote. Kwa hiyo BWANA akawapa Israeli nchi yote aliyokuwa ameapa kuwapa baba zao, nao wakaimiliki na kukaa humo. BWANA akawapa pumziko kila upande, kama vile alivyokuwa amewaapia baba zao, hakuna hata mmoja wa adui zao aliyeweza kusimama mbele yao, BWANA akawatia adui zao wote mikononi mwao. Hakuna hata mojawapo ya ahadi nzuri ya BWANA kwa nyumba ya Israeli ambayo haikutimia; kila moja ilitimia.