YouVersion Logo
Search Icon

Yobu 34

34
1Kisha Elihu akaendelea kusema:
2“Sikilizeni maneno yangu enyi wenye hekima,
nitegeeni masikio yenu, nyinyi wenye ujuzi.
3 # Taz Yobu 12:11 Sikio huyapima maneno,
kama vile ulimi uonjavyo chakula.
4Basi, na tuchague lililo sawa,
tuamue miongoni mwetu lililo jema.
5Basi, Yobu ametamka: ‘Mimi Yobu sina hatia,
Mungu ameniondolea haki yangu.
6Ingawa sina hatia naonekana kuwa mwongo;
kidonda changu hakiponyeki ingawa sina kosa.’
7Ni nani aliye kama Yobu
ambaye kwake ubaradhuli ni kama kunywa maji?
8Huandamana na watenda maovu
hutembea na watu waovu.
9Maana amesema, ‘Mtu hapati faida yoyote,
kujisumbua kumpendeza Mungu.’
10“Kwa hiyo nisikilizeni, enyi wenye ujuzi.
Mungu kamwe hawezi kufanya uovu;
Mungu Mwenye Nguvu hawezi kufanya kosa.
11 # Taz Zab 62:12 Mungu atamlipa mtu kadiri ya matendo yake,
atamlipiza kulingana na mwenendo wake.
12Ni ukweli mtupu: Mungu hafanyi ovu;
Mungu Mwenye Nguvu kamwe hapotoshi haki.
13Je, kuna aliyemkabidhi mamlaka juu ya dunia?
Uwezo wake juu ya ulimwengu ni wake peke yake.
14Kama Mungu angejifikiria tu yeye mwenyewe,
akiondoa pumzi yake ya uhai duniani,
15viumbe vyote vingeangamia kabisa,
naye binadamu angerudi mavumbini.
16“Kama una akili sikiliza;
sikiliza ninachokuambia.
17Je, anayetawala ulimwengu kwa sheria zake anachukia haki?
Je, utathubutu kumhukumu mwadilifu na mwenye nguvu?
18Amwambiaye mfalme, ‘Wewe ni takataka!’
Na watu mashuhuri, ‘Nyinyi ni waovu!’
19Yeye hawapendelei wakuu,
wala kuwajali matajiri kuliko maskini,
maana wote hao ni kazi ya mikono yake.
20Kufumba na kufumbua hao wamekufa;
hutikiswa usiku na kuaga dunia;
nao wenye nguvu hufutiliwa mbali bila kutumia nguvu za mtu.
21“Macho ya Mungu huchunguza mienendo ya watu;
yeye huziona hatua zao zote.
22Hakuna weusi wala giza nene
ambamo watenda maovu waweza kujificha.
23Mungu hahitaji kumjulisha mtu
wakati wa kumleta mbele ya mahakama yake.
24Huwaangamiza wenye nguvu bila uchunguzi,
na kuwaweka wengine mahali pao.
25Kwa kuwa anayajua matendo yao yote,
huwaporomosha usiku wakaangamia.
26Huwachapa hadharani kwa ajili ya uovu wao,
27kwa sababu wameacha kumfuata yeye,
wakazipuuza njia zake zote.
28Hata wakasababisha kilio cha maskini kimfikie Mungu,
Mungu akasikiliza kilio chao hao walioteswa.
29Kama Mungu akinyamaza, nani awezaye kumlaumu?
Kama akificha uso wake, nani awezaye kumwona,
30liwe ni taifa au mtu mmojammoja?
Hufanya hivyo, mtu mbaya asitawale,#34:30 hati nyingine za kale: Lakini aweza kuyawekea mataifa na watu mtu mbaya kuwa mfalme, mdhalimu.
au wale wahatarishao maisha ya watu.
31“Tuseme mtu amemwambia Mungu,
‘Nimekosa, sitatenda dhambi tena.
32Nioneshe makosa nisiyoweza kuyaona
kama nimetenda mabaya sitayarudia tena.’
33Je, Mungu atapaswa kumwadhibu kama uonavyo wewe?
Wewe ndiwe unayeamua, sio mimi.
Basi, sema unachofikiri wewe.
34Mtu yeyote mwenye akili,
na kila mwenye hekima anayenisikiliza atasema:
35‘Yobu anaongea bila kutumia akili,
maneno yake hayana maana.’
36Laiti Yobu angechunguzwa mpaka mwisho,
kwa maana anajibu kama watu waovu.
37Huongeza uasi juu ya dhambi zake;
anaeneza mashaka kati yetu,
na kuzidisha maneno yake dhidi ya Mungu.”

Currently Selected:

Yobu 34: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy