YouVersion Logo
Search Icon

Mdo 19

19
Paulo katika Efeso
1Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; 2#Mdo 2:38akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. 3Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana. 4#Mt 3:11; Mk 1:4,7-8; Lk 3:4,16; Yn 1:26-27Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. 5Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. 6#Mdo 8:17; 10:44,46Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri. 7Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili.
8Akaingia ndani ya sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa miezi mitatu, akihojiana na watu, na kuwavuta katika mambo ya ufalme wa Mungu. 9#2 Tim 1:15; Mdo 9:2; Tit 3:10,11; 2 Kor 6:17; 2 Yoh 1:10Lakini wengine walikaidi, wakakataa kuamini, wakiitukana ile Njia mbele ya mkutano; basi, akaondoka akawaacha, akawatenga wanafunzi, akahojiana na watu kila siku katika darasa ya mtu mmoja, jina lake Tirano. 10Mambo haya yakaendelea kwa muda wa miaka miwili, hata wote waliokaa Asia wakalisikia neno la Bwana, Wayahudi kwa Wayunani.
Wana wa Skewa
11 # Mdo 14:3 Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; 12#Mdo 5:15hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.
13 # Lk 9:49 Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. 14Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. 15#Mk 1:34; Lk 4:41Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? 16Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.
17 # Mdo 5:5,11 Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa. 18Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. 19Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu.#19:19 Yapata kama shilingi 34,000. 20#Mdo 6:7; 12:24Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu.
Ghasia katika Efeso
21 # Mdo 23:11; Rum 1:13 Mambo hayo yalipokwisha kumalizika, Paulo akaazimu rohoni mwake, akiisha kupita katika Makedonia na Akaya, aende Yerusalemu, akisema, Baada ya kuwako huko, yanipasa kuuona na Rumi pia. 22#Mdo 17:14; Rum 16:23; 1 Kor 4:17Akatuma watu wawili miongoni mwa wale waliomtumikia kwenda Makedonia, nao ni Timotheo na Erasto, yeye mwenyewe akakaa katika Asia kitambo.
23 # Mdo 19:9; 2 Kor 1:8,9 Wakati huo kukatukia ghasia si haba katika habari ya Njia ile. 24#Mdo 16:16Kwa maana mtu mmoja, jina lake Demetrio, mfua fedha, aliyekuwa akifanya vihekalu vya fedha vya Artemi, alikuwa akiwapatia mafundi faida nyingi. 25Akawakusanya hao, pamoja na wengine wenye kazi ile ile, akasema, Enyi wanaume, mnajua ya kuwa utajiri wetu hutoka katika kazi hii. 26#Mdo 17:29Tena mnaona na kusikia ya kwamba si katika Efeso tu, bali katika Asia yote pia Paulo huyo ameshawishi watu wengi na kuwageuza nia zao, akisema ya kwamba hiyo inayofanywa kwa mikono siyo miungu. 27Si kwamba kazi hii yetu ina hatari ya kudharauliwa tu; bali na hekalu la mungu mke aliye mkuu, Artemi, kuhesabiwa si kitu, na kuondolewa utukufu wake, ambaye Asia yote pia na walimwengu wote humwabudu. 28Waliposikia haya wakajaa ghadhabu, wakapiga kelele, wakisema, Artemi wa Waefeso ni mkuu.
29 # Mdo 20:4 Mji wote ukajaa ghasia, wakaenda mbio wakaingia mahali pa michezo kwa nia moja, wakiisha kuwakamata Gayo na Aristarko, watu wa Makedonia waliosafiri pamoja na Paulo. 30Na Paulo alipotaka kuingia kati ya watu, wanafunzi hawakumwacha aingie. 31Na baadhi ya wakuu wa Asia, walio rafiki zake, wakatuma watu kwake, wakimsihi asijihudhurishe nafsi yake ndani ya mahali pa michezo. 32Basi wengine walikuwa wakilia hivi na wengine hivi; kwa maana ule mkutano ulikuwa umechafuka-chafuka, na wengi wao hawakuijua sababu ya kukusanyika kwao pamoja. 33Wakamtoa Iskanda katika mkutano, Wayahudi wakimweka mbele ya watu. Iskanda akawapungia mkono, akitaka kujitetea mbele ya wale watu. 34Lakini walipotambua ya kuwa yeye ni Myahudi, wakapiga kelele wote pia kwa sauti moja kwa muda wa kama saa mbili, wakisema, Artemi wa Waefeso ni mkuu.
35Na karani wa mji alipokwisha kuwatuliza watu, akasema, Enyi wanaume wa Efeso, ni mtu gani asiyejua ya kuwa mji wa Efeso ni mtunzaji wa hekalu la Artemi, aliye mkuu, na wa kitu kile kilichoanguka kutoka mbinguni? 36Basi kwa kuwa mambo haya hayawezi kukanushwa, imewapasa kutulia; msifanye neno la haraka haraka. 37Kwa maana mmewaleta watu hawa, wasioiba vitu vya hekalu wala kumtukana mungu mke wetu. 38Basi ikiwa Demetrio na mafundi walio pamoja naye wana neno juu ya mtu, baraza ziko, na maliwali wako; na washitakiane. 39Bali mkitafuta neno lo lote katika mambo mengine, yatatengenezwa katika kusanyiko lililo halali. 40Kwa maana tuna hatari ya kushitakiwa kwa ajili ya matata haya ya leo, ambayo hayana sababu; na katika neno hilo, hatutaweza kujiudhuru kwa mkutano huu. 41Alipokwisha kusema haya akauvunja mkutano.

Currently Selected:

Mdo 19: SUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy