YouVersion Logo
Search Icon

Mdo 20

20
Paulo Aenda Makedonia na Ugiriki
1Kishindo kile kilipokoma, Paulo akatuma kuwaita wanafunzi akawaonya, akaagana nao, kisha akaondoka aende zake mpaka Makedonia. 2Naye akiisha kupita pande zile na kuwafariji kwa maneno mengi, akafika Uyunani.
3Alipokwisha kukaa huko miezi mitatu, na Wayahudi kumfanyia vitimvi, alipotaka kwenda Shamu kwa njia ya bahari; basi akaazimu kurejea kwa njia ya Makedonia. 4#Mdo 17:10; 19:29; Rum 16:21Watu hawa wakafuatana naye, Sopatro Mberoya, mwana wa Piro, na Aristarko na Sekundo, watu wa Thesalonike; na Gayo mtu wa Derbe, na Timotheo; na Tikiko na Trofimo watu wa Asia. 5#Mdo 16:8Ila watu hao wamekwisha kutangulia wakamngojea Troa. 6Sisi tukatweka baada ya siku za mikate isiyotiwa chachu, tukatoka Filipi, tukawafikia Troa, safari ya siku tano, tukakaa huko siku saba.
Ziara ya Mwisho ya Paulo huko Troa
7 # 1 Kor 16:2; Mdo 2:42,46 Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane. 8Palikuwa na taa nyingi katika orofa ile tulipokuwa tumekusanyika. 9Kijana mmoja, jina lake Eutiko, alikuwa ameketi dirishani, akalemewa na usingizi sana; hata Paulo alipoendelea sana kuhubiri, akazidiwa na usingizi wake akaanguka toka orofa ya tatu; akainuliwa amekwisha kufa. 10#1 Fal 17:21Paulo akashuka, akamwangukia, akamkumbatia, akasema, Msifanye ghasia, maana uzima wake ungalimo ndani yake. 11Akapanda juu tena, akamega mkate, akala, akazidi kuongea nao hata alfajiri, ndipo akaenda zake. 12Wakamleta yule kijana, yu mzima, wakafarijika faraja kubwa sana.
Safari ya kutoka Troa hadi Mileto
13Lakini sisi tukatangulia kwenda merikebuni, tukaabiri kwenda Aso, tukikusudia kumpakia Paulo huko; kwa maana ndivyo alivyoagiza, yeye mwenyewe aliazimu kwenda kwa miguu. 14Alipotufikia huko Aso, tukampakia, kisha tukafika Mitilene. 15Tukatweka kutoka huko, na siku ya pili tukafika mahali panapokabili Kio; siku ya tatu tukawasili Samo, tukakaa Trogilio, siku ya nne tukafika Mileto. 16#Mdo 18:21Kwa sababu Paulo amekusudia kupita Efeso merikebuni, asije akakawia katika Asia; kwa maana alikuwa na haraka, akitaka kuwahi Yerusalemu siku ya Pentekoste, kama ikiwezekana.
Paulo asema na Viongozi wa Efeso
17Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso, akawaita wazee wa kanisa. 18#Mdo 18:19; 19:10Walipofika kwake, akawaambia,
Ninyi wenyewe mnajua tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa kwenu wakati wote, 19#Mdo 20:3nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kwa hila za Wayahudi; 20ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba, 21nikiwashuhudia Wayahudi na Wayunani wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo. 22#Mdo 19:21Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; 23#Mdo 9:16; 21:4,11isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja. 24#2 Tim 4:7; Mdo 21:13Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu. 25Na sasa, tazameni, mimi najua ya kuwa ninyi nyote niliowahubiria ufalme wa Mungu, nikienda huko na huko, hamtaniona uso tena. 26#Mdo 18:6Kwa hiyo nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa mimi sina hatia kwa damu ya mtu awaye yote. 27Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu.
28 # Zab 74:2; 1 Tim 4:16; 1 Pet 5:2 Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. 29#Mt 7:15; 10:16; Yn 10:12Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; 30#1 Yoh 2:19; Gal 4:17tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao. 31#Mk 13:35,37; 1 The 2:11Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi.
32 # Kum 33:3 Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa. 33#Mt 10:8; 1 Kor 9:12; 1 Sam 12:3Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. 34#Mdo 18:3; 1 Kor 4:12; 1 The 2:9Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. 35Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.
36 # Mdo 21:5 Alipokwisha kunena haya akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote. 37#Mdo 21:6; Rum 16:16; 1 Pet 5:14Wakalia sana wote, wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusu-busu, 38#Mdo 20:25wakihuzunika zaidi kwa sababu ya neno lile alilosema, ya kwamba hawatamwona uso tena. Wakamsindikiza hata merikebuni.

Currently Selected:

Mdo 20: SUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy