Soma Biblia Kila Siku Oktoba/2022Mfano

Linaloheshimika katika ulimwengu huu si sawa na lile linaloleta heshima mbele ya Mungu. Katika m.46-48 imeandikwa kwamba wanafunzi wakaanza kuhojiana, ni nani atakayekuwa mkubwa miongoni mwao. Naye Yesu alipotambua mawazo ya mioyo yao, alitwaa mtoto mdogo akamweka karibu naye, akawaambia, Ye yote atakayempokea mtoto huyu kwa jina langu anipokea mimi; na ye yote atakayenipokea mimi ampokea yeye aliyenituma. Kwa kuwa aliye mdogo miongoni mwenu nyote huyo ndiye mkubwa. Sasa Yesu amemaliza kazi yake Galilaya na kuanza kuelekea Yerusalemu ambapo atateswa (m.51, Ikawa, siku ya kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia, yeye aliukaza uso wake kwenuda Yerusalemu). Wasamaria walidai kwamba mahali pa kuabudu ni mlima Gerizimu, na Wayahudi kwamba ni Yerusalemu (unaweza kuangalia Yn 4:19-21 na Kum 11:29 kwa maelezo zaidi). Siku zile suala hili lilizidi kuleta mafarakano kati yao, kama habari ya m.53 inavyodokeza, Wenyeji hawakumkaribisha [Yesu] kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu. Maana ya m.59 si kwamba baba yake mtu huyu alikuwa amefariki au kuugua, bali alikuwa anataka tu aishi kwa baba yake mpaka atakapokufa. Ndipo angemfuata Yesu. Ndiyo maana Yesu alisema, Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona (Mt 10:37-39).
Andiko
Kuhusu Mpango huu

Soma Biblia Kila Siku Oktoba/2022 ni mpango wa kusoma Biblia sehemu kwa sehemu kila siku kwa mwezi wa Oktoba pamoja na maelezo mafupi yatakayokusaidia kuelewa kwa urahisi na kuendelea kutafakari neno la Mungu ulilosoma kwa siku husika. Katika mpango huu utasoma zaidi katika kitabu cha Luka. Karibu kujiunga na mpango huu na usome bure
More
http://www.somabiblia.or.tz