Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 119:17-48

Zaburi 119:17-48 Biblia Habari Njema (BHN)

Unitendee mimi mtumishi wako kwa ukarimu, nipate kuishi na kushika neno lako. Uyafumbue macho yangu, niyaone maajabu ya sheria yako. Mimi ni mkimbizi tu hapa duniani; usinifiche amri zako. Roho yangu yaugua kwa hamu kubwa ya kutaka kujua daima maagizo yako. Wewe wawakemea wenye kiburi, walaanifu, ambao wanakiuka amri zako. Uniepushe na matusi na madharau yao, maana nimeyazingatia maamuzi yako. Hata kama wakuu wanakula njama dhidi yangu; mimi mtumishi wako nitayatafakari maamuzi yako. Masharti yako ni furaha yangu; hayo ni washauri wangu. Nagaagaa chini mavumbini; unipe tena uhai kama ulivyoahidi. Nimeungama niliyotenda, nawe ukanijibu; unifundishe masharti yako. Unifundishe namna ya kushika kanuni zako, nami nitayatafakari matendo yako ya ajabu. Niko hoi kwa uchungu; unirudishie nguvu kama ulivyoahidi. Uniepushe na njia za upotovu; unifundishe kwa wema sheria yako. Nimechagua njia ya uaminifu; nimezingatia maagizo yako. Nazingatia maamuzi yako, ee Mwenyezi-Mungu; usikubali niaibishwe! Nitafuata maelekezo ya amri zako, maana unanipa maarifa zaidi. Ee Mwenyezi-Mungu, unifundishe kutii masharti yako; nami nitayashika mpaka mwisho. Unieleweshe nipate kuishika sheria yako, niifuate kwa moyo wangu wote. Uniongoze katika njia ya amri zako, maana humo napata furaha yangu. Unipe ari ya kuzingatia maamuzi yako, na si kwa ajili ya kupata faida isiyofaa. Uniepushe, nisifuate mambo ya upuuzi; unioneshe njia yako, unipe uhai. Unitimizie mimi mtumishi wako ahadi yako; ahadi unayowapa wale wanaokuheshimu. Uniokoe na lawama ninazoogopa; maana maagizo yako ni mema. Natamani sana kuzitii kanuni zako; unijalie uhai maana wewe ni mwadilifu. Fadhili zako zinijie, ee Mwenyezi-Mungu; uniokoe kama ulivyoahidi. Hapo nitaweza kuwajibu hao wanaonitukana, maana mimi nina imani sana na neno lako. Unijalie kusema ukweli wako daima, maana tumaini langu liko katika maagizo yako. Nitatii sheria yako daima, nitaishika milele na milele. Nitaishi katika uhuru kamili, maana nazitilia maanani kanuni zako. Nitawatangazia wafalme maamuzi yako, wala sitaona aibu. Furaha yangu ni kuzitii amri zako, ambazo mimi nazipenda. Naziheshimu na kuzipenda amri zako; nitayatafakari masharti yako.

Shirikisha
Soma Zaburi 119

Zaburi 119:17-48 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Umtendee mtumishi wako ukarimu, Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako. Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako. Mimi ni mgeni katika nchi, Usinifiche maagizo yako. Roho yangu imepondeka kwa kutamani Hukumu zako kila wakati. Umewakemea wenye kiburi, Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako. Uniondolee laumu na dharau, Kwa maana nimezishika shuhuda zako. Wakuu nao waliketi wakaninena, Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako. Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu, Na washauri wangu. Nafsi yangu imegandamia mavumbini, Unihuishe sawasawa na neno lako. Nilizisimulia njia zangu ukanijibu, Unifundishe amri zako. Unifahamishe njia ya maagizo yako, Nami nitayatafakari maajabu yako. Nafsi yangu imeyeyuka kwa huzuni, Unitie nguvu sawasawa na neno lako. Uniondolee njia ya uongo, Unineemeshe kwa sheria yako. Nimeichagua njia ya uaminifu, Na kuziweka hukumu zako mbele yangu. Nimeambatana na shuhuda zako, Ee BWANA, usiniaibishe. Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako, Utakaponipanulia ufahamu wangu. Ee BWANA, unifundishe njia ya amri zako, Nami nitaishika hadi mwisho. Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote. Uniendeshe katika mapito ya amri zako, Kwa maana nimependezwa nayo. Unielekeze moyo wangu katika shuhuda zako, Wala usiielekee tamaa. Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, Unihuishe katika njia yako. Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako, Iliyo ya wanaokucha. Uniondolee laumu niiogopayo, Maana hukumu zako ni njema. Tazama, nimeyatamani mausia yako, Unihuishe kwa haki yako. Ee BWANA, fadhili zako zinifikie na mimi, Naam, wokovu wako kulingana na ahadi yako. Nami nitamjibu neno anilaumuye, Kwa maana nilitumainia neno lako. Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe, Maana nimezingojea hukumu zako. Nami nitaitii sheria yako daima, Naam, milele na milele. Nami nitakwenda kwa uhuru, Kwa kuwa nimejifunza mausia yako. Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, Wala sitaona aibu. Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako, Ambayo nimeyapenda. Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda, Nami nitazitafakari amri zako.

Shirikisha
Soma Zaburi 119

Zaburi 119:17-48 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Umtendee mtumishi wako ukarimu, Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako. Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako. Mimi ni mgeni katika nchi, Usinifiche maagizo yako. Roho yangu imepondeka kwa kutamani Hukumu zako kila wakati. Umewakemea wenye kiburi, Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako. Uniondolee laumu na dharau, Kwa maana nimezishika shuhuda zako. Wakuu nao waliketi wakaninena, Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako. Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu, Na washauri wangu. Nafsi yangu imeambatana na mavumbi, Unihuishe sawasawa na neno lako. Nalizisimulia njia zangu ukanijibu, Unifundishe amri zako. Unifahamishe njia ya mausia yako, Nami nitayatafakari maajabu yako. Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito, Unitie nguvu sawasawa na neno lako. Uniondolee njia ya uongo, Unineemeshe kwa sheria yako. Nimeichagua njia ya uaminifu, Na kuziweka hukumu zako mbele yangu. Nimeambatana na shuhuda zako, Ee BWANA, usiniaibishe. Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako, Utakaponikunjua moyo wangu. Ee BWANA, unifundishe njia ya amri zako, Nami nitaishika hata mwisho. Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote. Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Kwa maana nimependezwa nayo. Unielekeze moyo wangu na shuhuda zako, Wala usiielekee tamaa. Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, Unihuishe katika njia yako. Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako, Inayohusu kicho chako. Uniondolee laumu niiogopayo, Maana hukumu zako ni njema. Tazama, nimeyatamani mausia yako, Unihuishe kwa haki yako. Ee BWANA, fadhili zako zinifikie na mimi, Naam, wokovu wako sawasawa na ahadi yako. Nami nitamjibu neno anilaumuye, Kwa maana nalitumainia neno lako. Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe, Maana nimezingojea hukumu zako. Nami nitaitii sheria yako daima, Naam, milele na milele. Nami nitakwenda panapo nafasi, Kwa kuwa nimejifunza mausia yako. Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, Wala sitaona aibu. Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako, Ambayo nimeyapenda. Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda, Nami nitazitafakari amri zako.

Shirikisha
Soma Zaburi 119

Zaburi 119:17-48 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Mtendee mema mtumishi wako, nami nitaishi; nitalitii neno lako. Yafungue macho yangu nipate kuona mambo ya ajabu katika sheria yako. Mimi ni mgeni duniani, usinifiche amri zako. Nafsi yangu inataabika kwa shauku kubwa kwa sheria zako wakati wote. Unawakemea wenye majivuno, waliolaaniwa, wanaoenda mbali na amri zako. Niondolee dharau na dhihaka, kwa kuwa ninazishika sheria zako. Ingawa watawala huketi pamoja na kunisingizia, mtumishi wako atatafakari juu ya maagizo yako. Sheria zako ni furaha yangu, nazo ni washauri wangu. BWANA Nimelazwa chini mavumbini, yahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako. Nilikueleza njia zangu ukanijibu, nifundishe sheria zako. Nijulishe mafundisho ya mausia yako, nami nitatafakari maajabu yako. Nafsi yangu imechakazwa kwa huzuni, uniimarishe sawasawa na neno lako. Niepushe na njia za udanganyifu, kwa neema unifundishe sheria zako. Nimechagua njia ya kweli, nimekaza moyo wangu katika sheria zako. Nimengʼangʼania sheria zako, Ee BWANA, usiniache niaibishwe. Nakimbilia katika njia ya maagizo yako, kwa kuwa umeuweka moyo wangu huru. Ee BWANA, nifundishe kuyafuata maagizo yako, nami nitayashika hadi mwisho. Nipe ufahamu, nami nitaishika sheria yako na kuitii kwa moyo wangu wote. Niongoze kwenye njia ya amri zako, kwa kuwa huko napata furaha. Ugeuze moyo wangu kuelekea sheria zako, na siyo kwenye mambo ya ubinafsi. Geuza macho yangu kutoka mambo yasiyofaa, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako. Mtimizie mtumishi wako ahadi yako, ili upate kuogopwa. Niondolee aibu ninayoiogopa, kwa kuwa sheria zako ni njema. Tazama jinsi ninavyoonea shauku mausia yako! Hifadhi maisha yangu katika haki yako. BWANA Ee BWANA, upendo wako usiokoma unijie, wokovu wako sawasawa na ahadi yako, ndipo nitakapomjibu anayenidhihaki, kwa kuwa ninalitumainia neno lako. Usilinyakue neno la kweli kutoka kinywani mwangu, kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika amri zako. Nitaitii amri yako daima, naam, milele na milele. Nitatembea huru, kwa kuwa nimejifunza mausia yako. Nitasema sheria zako mbele za wafalme wala sitaaibishwa, kwa kuwa ninazifurahia amri zako kwa sababu ninazipenda. Ninaziinulia amri zako ambazo ninazipenda mikono yangu, nami ninatafakari juu ya maagizo yako.

Shirikisha
Soma Zaburi 119