Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 119:17-48

Zaburi 119:17-48 SRUV

Umtendee mtumishi wako ukarimu, Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako. Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako. Mimi ni mgeni katika nchi, Usinifiche maagizo yako. Roho yangu imepondeka kwa kutamani Hukumu zako kila wakati. Umewakemea wenye kiburi, Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako. Uniondolee laumu na dharau, Kwa maana nimezishika shuhuda zako. Wakuu nao waliketi wakaninena, Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako. Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu, Na washauri wangu. Nafsi yangu imegandamia mavumbini, Unihuishe sawasawa na neno lako. Nilizisimulia njia zangu ukanijibu, Unifundishe amri zako. Unifahamishe njia ya maagizo yako, Nami nitayatafakari maajabu yako. Nafsi yangu imeyeyuka kwa huzuni, Unitie nguvu sawasawa na neno lako. Uniondolee njia ya uongo, Unineemeshe kwa sheria yako. Nimeichagua njia ya uaminifu, Na kuziweka hukumu zako mbele yangu. Nimeambatana na shuhuda zako, Ee BWANA, usiniaibishe. Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako, Utakaponipanulia ufahamu wangu. Ee BWANA, unifundishe njia ya amri zako, Nami nitaishika hadi mwisho. Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote. Uniendeshe katika mapito ya amri zako, Kwa maana nimependezwa nayo. Unielekeze moyo wangu katika shuhuda zako, Wala usiielekee tamaa. Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, Unihuishe katika njia yako. Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako, Iliyo ya wanaokucha. Uniondolee laumu niiogopayo, Maana hukumu zako ni njema. Tazama, nimeyatamani mausia yako, Unihuishe kwa haki yako. Ee BWANA, fadhili zako zinifikie na mimi, Naam, wokovu wako kulingana na ahadi yako. Nami nitamjibu neno anilaumuye, Kwa maana nilitumainia neno lako. Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe, Maana nimezingojea hukumu zako. Nami nitaitii sheria yako daima, Naam, milele na milele. Nami nitakwenda kwa uhuru, Kwa kuwa nimejifunza mausia yako. Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, Wala sitaona aibu. Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako, Ambayo nimeyapenda. Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda, Nami nitazitafakari amri zako.

Soma Zaburi 119