Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 119

119
Sheria ya Mungu
1Heri watu wanaoishi bila kosa,
wanaozingatia sheria ya Mwenyezi-Mungu.
2Heri wanaozingatia matakwa yake,
wanaomtafuta kwa moyo wao wote,
3watu wasiotenda uovu kamwe,
bali daima hufuata njia zake.
4Ee Mungu, umetupatia kanuni zako
ili tuzishike kwa uaminifu.
5Laiti mwenendo wangu ungeimarika,
kwa kuyafuata masharti yako!
6Nikizingatia amri zako zote,
hapo kweli sitaaibishwa.
7Nitakusifu kwa moyo mnyofu,
nikijifunza maagizo yako maadilifu.
8Nitayafuata masharti yako;
usiniache hata kidogo.
Kutii sheria ya Mungu
9Kijana atatunzaje maisha yake kuwa safi?
Kwa kuyaongoza kadiri ya neno lako.
10Najitahidi kukutii kwa moyo wote;
usiniache nikiuke amri zako.
11Nimeshika neno lako moyoni mwangu,
nisije nikakukosea.
12Utukuzwe, ee Mwenyezi-Mungu!
Unifundishe masharti yako.
13Nitayarudia kwa sauti
maagizo yako yote uliyotoa.
14Nafurahi kufuata maamuzi yako,
kuliko kuwa na utajiri mwingi.
15Nazitafakari kanuni zako,
na kuzizingatia njia zako.
16Nayafurahia masharti yako;
sitalisahau neno lako.
Kufurahia sheria ya Mungu
17Unitendee mimi mtumishi wako kwa ukarimu,
nipate kuishi na kushika neno lako.
18Uyafumbue macho yangu,
niyaone maajabu ya sheria yako.
19Mimi ni mkimbizi tu hapa duniani;
usinifiche amri zako.
20Roho yangu yaugua kwa hamu kubwa
ya kutaka kujua daima maagizo yako.
21Wewe wawakemea wenye kiburi, walaanifu,
ambao wanakiuka amri zako.
22Uniepushe na matusi na madharau yao,
maana nimeyazingatia maamuzi yako.
23Hata kama wakuu wanakula njama dhidi yangu;
mimi mtumishi wako nitayatafakari maamuzi yako.
24Masharti yako ni furaha yangu;
hayo ni washauri wangu.
Kushika sheria ya Mungu
25Nagaagaa chini mavumbini;
unipe tena uhai kama ulivyoahidi.
26Nimeungama niliyotenda, nawe ukanijibu;
unifundishe masharti yako.
27Unifundishe namna ya kushika kanuni zako,
nami nitayatafakari matendo#119:27 matendo yako: Au Mafundisho yako. yako ya ajabu.
28Niko hoi kwa uchungu;
unirudishie nguvu kama ulivyoahidi.
29Uniepushe na njia za upotovu;
unifundishe kwa wema sheria yako.
30Nimechagua njia ya uaminifu;
nimezingatia maagizo yako.
31Nazingatia maamuzi yako, ee Mwenyezi-Mungu;
usikubali niaibishwe!
32Nitafuata maelekezo ya amri zako,
maana unanipa maarifa zaidi.
Kuomba maarifa
33Ee Mwenyezi-Mungu, unifundishe kutii masharti yako;
nami nitayashika mpaka mwisho.
34Unieleweshe nipate kuishika sheria yako,
niifuate kwa moyo wangu wote.
35Uniongoze katika njia ya amri zako,
maana humo napata furaha yangu.
36Unipe ari ya kuzingatia maamuzi yako,
na si kwa ajili ya kupata faida isiyofaa.
37Uniepushe, nisifuate mambo ya upuuzi;
unioneshe njia yako, unipe uhai.
38Unitimizie mimi mtumishi wako ahadi yako;
ahadi unayowapa wale wanaokuheshimu.
39Uniokoe na lawama ninazoogopa;
maana maagizo yako ni mema.
40Natamani sana kuzitii kanuni zako;
unijalie uhai maana wewe ni mwadilifu.
Kutegemea sheria ya Mungu
41Fadhili zako zinijie, ee Mwenyezi-Mungu;
uniokoe kama ulivyoahidi.
42Hapo nitaweza kuwajibu hao wanaonitukana,
maana mimi nina imani sana na neno lako.
43Unijalie kusema ukweli wako daima,
maana tumaini langu liko katika maagizo yako.
44Nitatii sheria yako daima,
nitaishika milele na milele.
45Nitaishi katika uhuru kamili,
maana nazitilia maanani kanuni zako.
46Nitawatangazia wafalme maamuzi yako,
wala sitaona aibu.
47Furaha yangu ni kuzitii amri zako,
ambazo mimi nazipenda.
48Naziheshimu na kuzipenda amri zako;
nitayatafakari masharti yako.
Kuwa na imani na sheria ya Mungu
49Ukumbuke ahadi yako kwangu mimi mtumishi wako,
ahadi ambayo imenipa matumaini.
50Hata niwapo taabuni napata kitulizo,
maana ahadi yako yanipa uhai.
51Wasiomjali Mungu hunidharau daima,
lakini mimi sikiuki sheria yako.
52Ninapoyakumbuka maagizo yako ya tangu kale,
nafarijika, ee Mwenyezi-Mungu.
53Nashikwa na hasira kali,
nionapo waovu wakivunja sheria yako.
54Masharti yako yamekuwa wimbo wangu,
nikiwa huku ugenini.
55Usiku ninakukumbuka, ee Mwenyezi-Mungu,
na kushika sheria yako.
56Hii ni baraka kubwa kwangu,
kwamba nazishika kanuni zako.
Heshima kwa sheria ya Mungu
57Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, ndiwe riziki yangu kuu;
naahidi kushika maneno yako.
58Naomba radhi yako kwa moyo wangu wote;
unionee huruma kama ulivyoahidi!
59Nimeufikiria mwenendo wangu,
na nimerudi nifuate maamuzi yako.
60Bila kukawia nafanya haraka
kuzishika amri zako.
61Waovu wametega mitego waninase,
lakini mimi sisahau sheria yako.
62Usiku wa manane naamka kukusifu,
kwa sababu ya maagizo yako maadilifu.
63Mimi ni rafiki ya wote wakuchao,
rafiki yao wanaozitii kanuni zako.
64Dunia imejaa fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu,
unifundishe masharti yako.
Ukamilifu wa sheria ya Mungu
65Umenitendea vema mimi mtumishi wako,
kama ulivyoahidi, ee Mwenyezi-Mungu.
66Unifundishe akili na maarifa,
maana nina imani sana na amri zako.
67Kabla ya kuniadhibu nilikuwa nikikosea,
lakini sasa nashika neno lako.
68Wewe ni mwema na mfadhili;
unifundishe masharti yako.
69Wenye kiburi wanasema uongo juu yangu,
lakini mimi nashika kanuni zako kwa moyo wote.
70Mioyo yao imejaa upumbavu,
lakini mimi nafurahia sheria yako.
71Nimefaidika kutokana na taabu yangu,
maana imenifanya nijifunze masharti yako.
72Sheria uliyoweka ni bora kwangu,
kuliko mali zote za dunia.
Ukamilifu wa sheria ya Mungu
73Mikono yako iliniumba na kuniunda;
unijalie akili nijifunze amri zako.
74Wakuchao wataniona na kufurahi,
maana tumaini langu liko katika neno lako.
75Najua hukumu zako ni adili, ee Mwenyezi-Mungu,
na kwamba umeniadhibu kwani wewe ni mwaminifu.
76Fadhili zako na zinipe faraja,
kama ulivyoniahidi mimi mtumishi wako.
77Unionee huruma nipate kuishi,
maana sheria yako ni furaha yangu.
78Wenye kiburi waaibike kwa maana wamenifanyia hila,
lakini mimi nitazitafakari kanuni zako.
79Wote wakuchao na waje kwangu,
wapate kuyajua maamuzi yako.
80Moyo wangu na uzingatie masharti yako,
nisije nikaaibishwa.
Sala wakati wa kudhulumiwa
81Niko hoi kwa kukungojea uniokoe;
naweka tumaini langu katika neno lako.
82Macho yangu yanafifia nikingojea ulichoahidi.
Nauliza: “Utakuja lini kunifariji?”
83Nimekunjamana kama kiriba katika moshi,
hata hivyo sijasahau masharti yako.
84Mimi mtumishi wako nitasubiri mpaka lini?
Utawaadhibu lini wale wanaonidhulumu?
85Wenye kiburi wamenichimbia mashimo,
watu ambao hawafuati sheria yako.
86Amri zako zote ni za kuaminika;
watu wananitesa bila haki; unisaidie!
87Karibu wangefaulu kuniangamiza,
lakini mimi sijavunja kanuni zako.
88Unisalimishe kadiri ya fadhili zako,
nipate kuzingatia maamuzi uliyotamka.
Sheria ya Mungu ni ya kutegemewa
89Neno lako, ee Mwenyezi-Mungu, ladumu milele;
limethibitika juu mbinguni.
90Uaminifu wako wadumu vizazi vyote,
umeiweka dunia mahali pake nayo yadumu.
91Kwa amri yako viumbe vyote vipo leo,
maana vitu vyote ni watumishi wako.
92Kama sheria yako isingekuwa furaha yangu,
ningalikwisha angamia kwa taabu zangu.
93Sitasahau kamwe kanuni zako,
maana kwa hizo umenipa uhai.
94Mimi ni wako, uniokoe,
maana nimejitahidi kuzishika kanuni zako.
95Waovu wanivizia wapate kuniua;
lakini mimi natafakari masharti yako.
96Nimetambua kila kitu hufikia kikomo,
lakini amri yako ni kamilifu.
Kuipenda sheria ya Mungu
97Naipenda sana sheria yako!
Naitafakari mchana kutwa!
98Amri yako iko nami daima,
yanipa hekima kuliko maadui zangu.
99Ninaelewa kuliko waalimu wangu wote,
kwa kuwa nayatafakari maamuzi yako.
100Nawapita wazee kwa busara yangu,
kwa sababu nazishika kanuni zako.
101Najizuia nisifuate njia mbaya,
nipate kulizingatia neno lako.
102Sikukiuka maagizo yako,
maana wewe mwenyewe ulinifundisha.
103Maneno yako ni matamu sana kwangu;
naam, ni matamu kuliko asali!
104Kwa kanuni zako napata hekima,
kwa hiyo nachukia kila mwenendo mbaya.
Sheria ya Mungu ni mwanga
105Neno lako ni taa ya kuniongoza,
na mwanga katika njia yangu.
106Nimeapa na kuthibitisha kiapo changu,
kwamba nitashika maagizo yako adili.
107Ee Mwenyezi-Mungu, ninateseka mno;
unijalie uhai kama ulivyoahidi.
108Ee Mwenyezi-Mungu, upokee sala yangu ya shukrani;
na kunifundisha maagizo yako.
109Maisha yangu yamo hatarini daima,
lakini siisahau sheria yako.
110Waovu wamenitegea mitego,
lakini sikiuki kanuni zako.
111Maamuzi yako ni riziki kubwa kwangu milele;
hayo ni furaha ya moyo wangu.
112Nimekusudia kwa moyo wote
kufuata masharti yako milele.
Usalama katika sheria ya Mungu
113Nawachukia watu wanafiki,
lakini naipenda sheria yako.
114Wewe ni ngao yangu, kwako napata usalama;
naweka tumaini langu katika neno lako.
115Ondokeni kwangu, enyi waovu,
ili nipate kushika amri za Mungu wangu.
116Uniimarishe ulivyoahidi, nami nitaishi;
usikubali niaibike katika tumaini langu.
117Unitegemeze, niwe salama;
niwe daima msikivu kwa masharti yako.
118Unawakataa wote wanaokiuka masharti yako;
mawazo yao maovu ni ya bure.
119Waovu wote wawaona kuwa takataka,
kwa hiyo mimi napenda maamuzi yako.
120Natetemeka kwa kukuogopa wewe;
nimejaa hofu kwa sababu ya hukumu zako.
Utii wa sheria ya Mungu
121Nimefanya mambo mema na adili;
usiniache makuchani mwa maadui zangu.
122Uahidi kunisaidia mimi mtumishi wako;
usikubali wenye kiburi wanidhulumu.
123Macho yangu yanafifia nikingojea uniokoe,
nikingojea utimize uliyoahidi.
124Unitendee mimi mtumishi wako kadiri ya wema wako,
unifundishe masharti yako.
125Mimi ni mtumishi wako, unipe maarifa,
nipate kujua maamuzi yako.
126Ee Mwenyezi-Mungu, sasa ni wakati wa kufanya kitu,
kwa maana watu wanavunja sheria yako.
127Mimi, nazipenda amri zako,
kuliko hata dhahabu safi kabisa.
128Kwa hiyo, nafuata kanuni zako zote;#119:128 nafuata kanuni zako zote: Maana katika Kiebrania si dhahiri.
kila njia potovu naichukia.
Hamu ya kutii sheria za Mungu
129Maamuzi yako ni ya ajabu;
kwa hiyo nayashika kwa moyo wote.
130Maelezo ya mafundisho yako huleta mwanga;
huwapa akili watu wasiojua kitu.
131Nafungua kinywa kwa hamu kubwa,
maana ninatamani sana amri zako.
132Unigeukie na kunionea huruma,
kama uwatendeavyo wanaokupenda.
133Uniimarishie hatua zangu kama ulivyoahidi;
usikubali mimi nitawaliwe na uovu.
134Unikomboe kutoka udhalimu wa binadamu,
ili nipate kuzishika kanuni zako.
135Uniangazie uso wako kwa wema,
unifundishe masharti yako.
136Macho yangu yabubujika machozi kama mto,
kwa sababu watu hawaishiki sheria yako.
Ukamilifu wa sheria ya Mungu
137Ee Mwenyezi-Mungu, wewe ni mwadilifu;
na hukumu zako ni za haki.
138Umetoa maamuzi yako,
kwa haki na uthabiti.
139Upendo wangu kwako wanifanya niwake hasira,
maana maadui zangu hawajali maneno yako.
140Ahadi yako ni hakika kabisa,
nami mtumishi wako naipenda.
141Mimi ni mdogo na ninadharauliwa;
hata hivyo sisahau kanuni zako.
142Uadilifu wako ni wa haki milele;
sheria yako ni ya kweli.
143Taabu na huzuni vimenipata,
lakini amri zako ndizo furaha yangu.
144Maamuzi yako ni ya haki daima;
unijalie maarifa nipate kuishi.
Kuomba usalama
145Nakulilia kwa moyo wangu wote;
unijibu, ee Mwenyezi-Mungu, nifuate kanuni zako.
146Nakulilia, unisalimishe;
nipate kuyazingatia maamuzi yako.
147Naamka kabla ya pambazuko na kukuomba msaada;
naweka tumaini langu katika maneno yako.
148Nakaa macho usiku kucha,
ili nitafakari juu ya maagizo yako.
149Kwa fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, unisikie;
unisalimishe kwa uadilifu wako.
150Wale wanaonidhulumu vibaya wanakaribia,
hao wako mbali kabisa na sheria yako.
151Lakini wewe u karibu nami, ee Mwenyezi-Mungu,
na amri zako zote ni za kuaminika.
152Tangu zamani, nimejifunza maamuzi yako;
ambayo umeyaweka hata yadumu milele.
Kuomba msaada
153Uangalie mateso yangu, uniokoe,
kwa maana sikuisahau sheria yako.
154Unitetee na kunikomboa;
unijalie uhai kama ulivyoahidi.
155Waovu hawataokolewa kamwe,
maana hawajali juu ya masharti yako.
156Huruma yako ni kubwa, ee Mwenyezi-Mungu,
unijalie uhai kama ulivyoahidi.
157Maadui na wadhalimu wangu ni wengi,
lakini mimi sikiuki maamuzi yako.
158Niwaonapo wahaini hao nachukizwa mno,
kwa sababu hawazishiki amri zako.
159Tazama, ee Mungu, ninavyozipenda kanuni zako!
Unijalie uhai kadiri ya fadhili zako.
160Kitovu cha neno lako ni ukweli,
maagizo yako yote adili, yadumu milele.
Kuzingatia sheria ya Mungu
161Wakuu wanidhulumu bila kisa,
lakini mimi naheshimu maneno yako kwa moyo wote.
162Nafurahi kwa sababu ya neno lako,
kama mtu aliyekuta kitu cha thamani kuu.
163Nachukia kabisa uongo,
lakini naipenda sheria yako.
164Nakusifu mara saba kila siku,
kwa sababu ya maagizo yako adili.
165Wapendao sheria yako wana amani kuu;
hakuna kinachoweza kuwaangusha.
166Ee Mwenyezi-Mungu, nakungojea uniokoe;
mimi natimiza amri zako.
167Nazingatia maamuzi yako;
nayapenda kwa moyo wote.
168Nazingatia kanuni na maamuzi yako;
wewe wauona mwenendo wangu wote.
Kuomba msaada
169Kilio changu kikufikie, ee Mwenyezi-Mungu!
Unijalie akili kama ulivyoahidi.
170Ombi langu likufikie;
uniokoe kama ulivyoahidi.
171Nitasema sifa zako mfululizo,
maana wanifundisha masharti yako.
172Nitaimba juu ya neno lako,
maana amri zako zote ni za haki.
173Uwe daima tayari kunisaidia,
maana nimeamua kufuata kanuni zako.
174Natazamia sana uniokoe, ee Mwenyezi-Mungu;
sheria yako ndiyo furaha yangu.
175Unijalie kuishi nipate kukusifu;
na maagizo yako yanisaidie.
176Natangatanga kama kondoo aliyepotea;
uje kunitafuta mimi mtumishi wako,
maana sikusahau amri zako.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 119: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha