Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 51:1-14

Yeremia 51:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nitachochea upepo wa kuangamiza dhidi ya Babuloni, dhidi ya wakazi wa Kaldayo. Nitawapeleka wapepetaji Babuloni, nao watampepeta; watamaliza kila kitu katika nchi yake watakapofika kuishambulia toka kila upande wakati wa maangamizi yake.” Usiwape nafasi wapiga mshale wa Babuloni; usiwaache wavute upinde, wala kuvaa mavazi yao ya vita. Usiwahurumie vijana wake; liangamize kabisa jeshi lake. Wataanguka na kuuawa katika nchi ya Wakaldayo, watajeruhiwa katika barabara zake. Lakini Israeli na Yuda hawakuachwa na Mungu wao Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ingawa nchi yao imejaa hatia mbele yake yeye Mtakatifu wa Israeli. Kimbieni kutoka Babuloni, kila mtu na ayaokoe maisha yake! Msiangamizwe katika adhabu yake, maana huu ndio wakati wa Mungu wa kulipa kisasi, anaiadhibu Babuloni kama inavyostahili. Babuloni ilikuwa kikombe cha dhahabu mkononi mwa Mwenyezi-Mungu, ambacho kiliilewesha dunia nzima. Mataifa yalikunywa divai yake, hata yakapatwa wazimu. Ghafla Babuloni imeanguka na kuvunjikavunjika; ombolezeni kwa ajili yake! Leteni dawa kutuliza maumivu yake; labda utaweza kuponywa. Tulijaribu kuuponya Babuloni, lakini hauwezi kuponywa. Uacheni, twendeni zetu, kila mmoja katika nchi yake, maana hukumu yake ni kuu mno imeinuka mpaka mawinguni. Mwenyezi-Mungu amethibitisha kuwa hatuna hatia. Twendeni Siyoni tukatangaze matendo ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Mwenyezi-Mungu amezichochea roho za wafalme wa Media, kwa maana amenuia kuiangamiza Babuloni. Naam, hicho ndicho kisasi cha Mwenyezi-Mungu; analipiza kisasi kwa ajili ya hekalu lake. Noeni mishale yenu! Chukueni ngao! Twekeni bendera ya vita kushambulia kuta za Babuloni. Imarisheni ulinzi; wekeni walinzi; tayarisheni mashambulizi. Mwenyezi-Mungu amepanga na kutekeleza mambo aliyosema juu ya wakazi wa Babuloni. Nchi hiyo imejaa mito na hazina tele, lakini mwisho wake umefika, uzi wa uhai wake umekatwa. Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameapa kwa nafsi yake: “Hakika nitakujaza majeshi mengi kama nzige, nayo yatapiga vigelegele vya ushindi juu yako”

Shirikisha
Soma Yeremia 51

Yeremia 51:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

BWANA asema hivi, Angalia, nitaamsha juu ya Babeli, na juu yao wakaao Leb-kamai, upepo uharibuo. Nami nitawatuma wapepetaji watakaompepea mpaka Babeli, nao wataifanya nchi yake kuwa tupu; kwa kuwa katika siku ya taabu watakuwa juu yake pande zote. Juu yake apindaye upinde, mwenye upinde na apinde upinde wake, na juu yake ajiinuaye katika dirii yake; msiwaachilie vijana wake; liangamizeni jeshi lake lote. Nao wataanguka, wakiwa wameuawa, katika nchi ya Wakaldayo, wakiwa wametumbuliwa katika njia zake kuu. Kwa maana Israeli, wala Yuda, hakuachwa na Mungu wake, BWANA wa majeshi; ijapokuwa nchi yao imejaa hatia juu yake aliye Mtakatifu wa Israeli. Kimbieni kutoka kati ya Babeli, kila mtu na ajiokoe nafsi yake; msikatiliwe mbali katika uovu wake; maana ni wakati wa kisasi cha BWANA, atamlipa malipo. Babeli umekuwa kikombe cha dhahabu mkononi mwa BWANA; kilicholevya dunia yote; mataifa wamekunywa mvinyo wake; kwa sababu hiyo mataifa wameingiwa na wazimu. Babeli umeanguka na kuangamia ghafla; mwombolezeni; twaeni zeri kwa maumivu yake; ili labda apate kuponywa. Tungependa kuuponya Babeli, Lakini haukuponyeka; Mwacheni, nasi twendeni zetu, Kila mtu hata nchi yake mwenyewe; Maana hukumu yake inafika hata mbinguni, Nayo imeinuliwa kufikia mawinguni. BWANA ameitokeza haki yetu; Njooni, tutangaze katika Sayuni Habari za kazi ya BWANA, Mungu wetu. Inoeni hiyo mishale; zishikeni ngao kwa nguvu; BWANA ameziamsha roho za wafalme wa Wamedi; kwa sababu shauri lake ni juu ya Babeli auangamize; maana ni kisasi cha BWANA, kisasi cha hekalu lake. Twekeni bendera ya vita juu ya kuta za Babeli, imarisheni ulinzi, wawekeni walinzi, tayarisheni waviziao; kwa maana BWANA ameazimia na kutenda yote aliyoyasema juu yao wakaao Babeli. Ewe ukaaye juu ya maji mengi, uliye na hazina nyingi, mwisho wako umewadia, kadiri ya tamaa zako. BWANA wa majeshi ameapa kwa nafsi yake, akisema, Hakika nitakujaza watu, kama nzige, nao watapiga kelele juu yako.

Shirikisha
Soma Yeremia 51

Yeremia 51:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

BWANA asema hivi, Angalia, nitaamsha juu ya Babeli, na juu yao wakaao Leb-kamai, upepo uharibuo. Nami nitapeleka wageni mpaka Babeli, watakaompepea; nao wataifanya nchi yake kuwa tupu; kwa kuwa katika siku ya taabu watakuwa juu yake pande zote. Juu yake apindaye upinde, mwenye upinde na apinde upinde wake, na juu yake ajiinuaye katika dirii yake; msiwaachilie vijana wake; liangamizeni jeshi lake lote. Nao wataanguka, hali ya kuuawa, katika nchi ya Wakaldayo, hali ya kutumbuliwa katika njia kuu zake. Kwa maana Israeli, wala Yuda, hakuachwa na Mungu wake, BWANA wa majeshi; ijapokuwa nchi yao imejaa hatia juu yake aliye Mtakatifu wa Israeli. Kimbieni kutoka kati ya Babeli, kila mtu na ajiokoe nafsi yake; msikatiliwe mbali katika uovu wake; maana ni wakati wa kisasi cha BWANA, atamlipa malipo. Babeli umekuwa kikombe cha dhahabu mkononi mwa BWANA; kilicholevya dunia yote; mataifa wamekunywa mvinyo wake; kwa sababu hiyo mataifa wameingiwa na wazimu. Babeli umeanguka na kuangamia ghafula; mpigieni yowe; twaeni zeri kwa maumivu yake; ili labda apate kuponywa. Tungependa kuuponya Babeli, Lakini haukuponyeka; Mwacheni, nasi twendeni zetu, Kila mtu hata nchi yake mwenyewe; Maana hukumu yake inafika hata mbinguni, Nayo imeinuliwa kufikilia mawinguni. BWANA ameitokeza haki yetu; Njoni, tutangaze katika Sayuni Habari za kazi ya BWANA, Mungu wetu. Inoeni hiyo mishale; zishikeni ngao kwa nguvu; BWANA ameziamsha roho za wafalme wa Wamedi; kwa sababu shauri lake ni juu ya Babeli auangamize; maana ni kisasi cha BWANA, kisasi cha hekalu lake. Twekeni bendera juu ya kuta za Babeli, yatieni malindo nguvu, wawekeni walinzi, tengenezeni waviziao; kwa maana BWANA ameazimia na kutenda yote aliyoyasema juu yao wakaao Babeli. Ewe ukaaye juu ya maji mengi, uliye na hazina nyingi, mwisho wako umewadia, kadiri ya tamaa zako. BWANA wa majeshi ameapa kwa nafsi yake, akisema, Hakika nitakujaza watu, kama nzige, nao watapiga kelele juu yako.

Shirikisha
Soma Yeremia 51

Yeremia 51:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Hili ndilo asemalo BWANA: “Tazama nitaamsha roho ya mwangamizi dhidi ya Babeli na wenyeji wa Leb-Kamai. Nitawatuma wageni Babeli kumpepeta na kuiharibu nchi yake; watampinga kila upande katika siku ya maafa yake. Usimwache mpiga upinde afunge kamba upinde wake, wala usimwache avae silaha zake. Usiwaonee huruma vijana wake; angamiza jeshi lake kabisa. Wataanguka barabarani waliouawa katika nchi ya Wakaldayo, wakiwa na majeraha ya kutisha. Kwa maana Israeli na Yuda hawajaachwa na Mungu wao, BWANA wa majeshi, ingawa nchi yao imejaa uovu mbele zake yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli. “Kimbieni kutoka Babeli! Okoeni maisha yenu! Msiangamizwe kwa sababu ya dhambi zake. Ni wakati wa kisasi cha BWANA, atamlipa kile anachostahili. Babeli alikuwa kikombe cha dhahabu katika mkono wa BWANA; aliufanya ulimwengu wote ulewe. Mataifa walikunywa mvinyo wake; kwa hiyo sasa wameingiwa na wazimu. Babeli ataanguka ghafula na kuvunjika. Mwombolezeni! Tafuteni zeri ya kutuliza maumivu yake, labda anaweza kupona. “ ‘Tungemponya Babeli, lakini hawezi kuponyeka; tumwacheni, na kila mmoja wetu aende nchi yake mwenyewe, kwa kuwa hukumu yake inafika angani, inapanda juu hadi mawinguni.’ “ ‘BWANA amethibitisha haki yetu; njooni, tutangaze katika Sayuni kitu ambacho BWANA Mungu wetu amefanya.’ “Noeni mishale, chukueni ngao! BWANA amewaamsha wafalme wa Wamedi, kwa sababu nia yake ni kuangamiza Babeli. BWANA atalipiza kisasi, kisasi kwa ajili ya Hekalu lake. Inueni bendera dhidi ya kuta za Babeli! Imarisheni ulinzi, wekeni walinzi, andaeni waviziaji! BWANA atatimiza kusudi lake, amri yake juu ya watu wa Babeli. Wewe uishiye kando ya maji mengi na uliye na wingi wa hazina, mwisho wako umekuja, wakati wako wa kukatiliwa mbali. BWANA wa majeshi ameapa kwa nafsi yake mwenyewe: ‘Hakika nitakujaza na watu, kama kundi la nzige, nao watashangilia kwa ushindi juu yako.’

Shirikisha
Soma Yeremia 51