Yeremia 51:1-14
Yeremia 51:1-14 NENO
Hili ndilo asemalo BWANA: “Tazama nitaamsha roho ya mwangamizi dhidi ya Babeli na wenyeji wa Leb-Kamai. Nitawatuma wageni Babeli kumpepeta na kuiharibu nchi yake; watampinga kila upande katika siku ya maafa yake. Usimwache mpiga upinde afunge kamba upinde wake, wala usimwache avae silaha zake. Usiwaonee huruma vijana wake; angamiza jeshi lake kabisa. Wataanguka barabarani waliouawa katika nchi ya Wakaldayo, wakiwa na majeraha ya kutisha. Kwa maana Israeli na Yuda hawajaachwa na Mungu wao, BWANA wa majeshi, ingawa nchi yao imejaa uovu mbele zake yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli. “Kimbieni kutoka Babeli! Okoeni maisha yenu! Msiangamizwe kwa sababu ya dhambi zake. Ni wakati wa kisasi cha BWANA, atamlipa kile anachostahili. Babeli alikuwa kikombe cha dhahabu katika mkono wa BWANA; aliufanya ulimwengu wote ulewe. Mataifa walikunywa mvinyo wake; kwa hiyo sasa wameingiwa na wazimu. Babeli ataanguka ghafula na kuvunjika. Mwombolezeni! Tafuteni zeri ya kutuliza maumivu yake, labda anaweza kupona. “ ‘Tungemponya Babeli, lakini hawezi kuponyeka; tumwacheni, na kila mmoja wetu aende nchi yake mwenyewe, kwa kuwa hukumu yake inafika angani, inapanda juu hadi mawinguni.’ “ ‘BWANA amethibitisha haki yetu; njooni, tutangaze katika Sayuni kitu ambacho BWANA Mungu wetu amefanya.’ “Noeni mishale, chukueni ngao! BWANA amewaamsha wafalme wa Wamedi, kwa sababu nia yake ni kuangamiza Babeli. BWANA atalipiza kisasi, kisasi kwa ajili ya Hekalu lake. Inueni bendera dhidi ya kuta za Babeli! Imarisheni ulinzi, wekeni walinzi, andaeni waviziaji! BWANA atatimiza kusudi lake, amri yake juu ya watu wa Babeli. Wewe uishiye kando ya maji mengi na uliye na wingi wa hazina, mwisho wako umekuja, wakati wako wa kukatiliwa mbali. BWANA wa majeshi ameapa kwa nafsi yake mwenyewe: ‘Hakika nitakujaza na watu, kama kundi la nzige, nao watashangilia kwa ushindi juu yako.’