Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 51

51
1Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Nitachochea upepo wa kuangamiza dhidi ya Babuloni,
dhidi ya wakazi wa Kaldayo.
2Nitawapeleka wapepetaji Babuloni,
nao watampepeta;
watamaliza kila kitu katika nchi yake
watakapofika kuishambulia toka kila upande
wakati wa maangamizi yake.”
3Usiwape nafasi wapiga mshale wa Babuloni;
usiwaache wavute upinde,
wala kuvaa mavazi yao ya vita.
Usiwahurumie vijana wake;
liangamize kabisa jeshi lake.
4Wataanguka na kuuawa katika nchi ya Wakaldayo,
watajeruhiwa katika barabara zake.
5Lakini Israeli na Yuda hawakuachwa na Mungu wao Mwenyezi-Mungu wa majeshi,
ingawa nchi yao imejaa hatia mbele yake yeye Mtakatifu wa Israeli.
6Kimbieni kutoka Babuloni,
kila mtu na ayaokoe maisha yake!
Msiangamizwe katika adhabu yake,
maana huu ndio wakati wa Mungu wa kulipa kisasi,
anaiadhibu Babuloni kama inavyostahili.
7Babuloni ilikuwa kikombe cha dhahabu
mkononi mwa Mwenyezi-Mungu,
ambacho kiliilewesha dunia nzima.
Mataifa yalikunywa divai yake,
hata yakapatwa wazimu.
8Ghafla Babuloni imeanguka na kuvunjikavunjika;
ombolezeni kwa ajili yake!
Leteni dawa kutuliza maumivu yake;
labda utaweza kuponywa.
9Tulijaribu kuuponya Babuloni,
lakini hauwezi kuponywa.
Uacheni, twendeni zetu,
kila mmoja katika nchi yake,
maana hukumu yake ni kuu mno
imeinuka mpaka mawinguni.
10Mwenyezi-Mungu amethibitisha kuwa hatuna hatia.
Twendeni Siyoni tukatangaze
matendo ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.
11Mwenyezi-Mungu amezichochea roho za wafalme wa Media, kwa maana amenuia kuiangamiza Babuloni. Naam, hicho ndicho kisasi cha Mwenyezi-Mungu; analipiza kisasi kwa ajili ya hekalu lake.
Noeni mishale yenu!
Chukueni ngao!
12Twekeni bendera ya vita
kushambulia kuta za Babuloni.
Imarisheni ulinzi;
wekeni walinzi;
tayarisheni mashambulizi.
Mwenyezi-Mungu amepanga na kutekeleza
mambo aliyosema juu ya wakazi wa Babuloni.
13Nchi hiyo imejaa mito na hazina tele,
lakini mwisho wake umefika,
uzi wa uhai wake umekatwa.
14Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameapa kwa nafsi yake:
“Hakika nitakujaza majeshi mengi kama nzige,
nayo yatapiga vigelegele vya ushindi juu yako”
15Mwenyezi-Mungu ndiye aliyeumba dunia kwa nguvu yake,
aliyeuimarisha ulimwengu kwa hekima yake,
na kwa maarifa yake akazitandaza mbingu.
16Anapotoa sauti yake maji hutitima mbinguni,
hufanya ukungu upande kutoka mipaka ya dunia.
Hufanya umeme umulike wakati wa mvua
huvumisha upepo kutoka ghala zake.
17Kila mtu ni mpumbavu bila maarifa,
kila mhunzi anaaibishwa na vinyago vyake;
maana sanamu zake ni udanganyifu mtupu,
wala hazina pumzi ndani yake.
18Hazina thamani, ni udanganyifu mtupu;
wakati watakapoadhibiwa,
nazo zitaangamia.
19Mungu aliye hazina ya Yakobo si kama hizo,
maana yeye ndiye aliyeviumba vitu vyote,
na Israeli ni kabila lililo mali yake;
Mwenyezi-Mungu wa Majeshi, ndilo jina lake.
Mwisho wa Babuloni
20Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Wewe Babuloni ni rungu na silaha yangu ya vita;
nakutumia kuyavunjavunja mataifa,
nakutumia kuangamiza falme.
21Nakutumia kuponda farasi na wapandafarasi,
magari ya kukokotwa na waendeshaji wake.
22Ninakutumia kuwaponda wanaume na wanawake,
wazee na vijana,
wavulana na wasichana.
23Ninakutumia kuponda wachungaji na makundi yao,
wakulima na wanyama wao wa kulimia,
wakuu wa mikoa na madiwani.
24“Nitaiadhibu Babuloni na wakazi wote wa Kaldayo mkiona kwa macho yenu wenyewe, kwa sababu ya uovu wote walioufanya katika Siyoni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
25Mimi ninapingana nawe ewe mlima mharibifu,
mlima unaoharibu dunia nzima!
Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
Nitanyosha mkono wangu dhidi yako,
nitakuangusha kutoka miambani juu
na kukufanya kuwa mlima uliochomwa moto;
26hata hamna jiwe lako litakalochukuliwa kujengea,
hakuna jiwe litakalochukuliwa kuwekea msingi!
Utakuwa kama jangwa milele.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
27Tweka bendera ya vita duniani,
piga tarumbeta kati ya mataifa;
yatayarishe mataifa kupigana naye;
ziite falme kuishambulia;
falme za Ararati, Mini na Ashkenazi.
Weka majemadari dhidi yake;
walete farasi kama makundi ya nzige.
28Yatayarishe mataifa kupigana naye vita;
watayarishe wafalme wa Medi, watawala na mawakili wao,
tayarisheni nchi zote katika himaya yake.
29Nchi inatetemeka na kugaagaa kwa maumivu,
maana nia ya Mwenyezi-Mungu kuhusu Babuloni ni thabiti:
Ataifanya nchi ya Babuloni kuwa jangwa,
ataifanya iwe bila watu.
30Askari wa Babuloni wameshindwa kupigana,
wamebaki katika ngome zao;
nguvu zao zimewaishia,
wamekuwa kama wanawake.
Nyumba za Babuloni zimechomwa moto,
malango yake ya chuma yamevunjwa.
31Tarishi baada ya tarishi wanapiga mbio,
mjumbe mmoja anamfuata mjumbe mwingine,
kumpasha habari mfalme wa Babuloni
kwamba mji wake umevamiwa kila upande.
32Vivuko vya mto vimetekwa,
ngome zimechomwa moto,
askari wamekumbwa na hofu.
33Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli asema hivi:
“Babuloni ni kama uwanja wa kupuria nafaka
wakati unapotayarishwa.
Lakini bado kidogo tu,
wakati wa mavuno utaufikia.”
34Mfalme Nebukadneza wa Babuloni
aliuharibu na kuuponda mji wa Yerusalemu
aliuacha kama chungu kitupu;
aliumeza kama joka.
Alijaza tumbo lake vitu vyake vizurivizuri,
akautupilia mbali kama matapishi.
35Watu wa Yerusalemu na waseme:
“Babuloni na ulipizwe ukatili uleule,
tuliotendwa sisi pamoja na jamaa zetu!
Babuloni ipatilizwe
kwa umwagaji wa damu yetu.”
Mwenyezi-Mungu atasaidia
36Kwa hiyo asema hivi Mwenyezi-Mungu:
“Nitawatetea kuhusu kisa chenu,
na kulipiza kisasi kwa ajili yenu.
Nitaikausha bahari ya Babuloni
na kuvifanya visima vyake vikauke.
37Babuloni itakuwa rundo la magofu,
itakuwa makao ya mbweha,
itakuwa kinyaa na kitu cha kuzomewa;
hakuna mtu atakayekaa huko.
38Wababuloni watanguruma pamoja kama simba;
watakoroma kama wanasimba.
39Wakiwa na uchu mkubwa
nitawaandalia karamu:
Nitawalewesha mpaka wapepesuke;
nao watalala usingizi wa daima
na hawataamka tena.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
40Nitawashusha chini kama kondoo wa kuchinjwa,
kama vile kondoo dume na beberu.
41Ajabu kutekwa kwa Babuloni;
mji uliosifika duniani kote umechukuliwa!
Babuloni umekuwa kinyaa kati ya mataifa!
42Bahari imefurika juu ya Babuloni,
Babuloni imefunikwa mawimbi yaliyochafuka.
43Miji yake imekuwa kinyaa,
nchi ya ukavu na jangwa,
nchi isiyokaliwa na mtu yeyote,
wala kupitika na binadamu yeyote.
44Nitamwadhibu mungu Beli huko Babuloni,
nitamfanya akitoe alichokimeza.
Mataifa hayatamiminika tena kumwendea.
Ukuta wa Babuloni umebomoka.
45“Tokeni humo enyi watu wangu!
Kila mtu na ayasalimishe maisha yake,
kutoka hasira kali ya Mwenyezi-Mungu.
46Msife moyo wala msiwe na hofu,
kwa sababu ya uvumi mnaosikia nchini.
Mwaka huu kuna uvumi huu,
mwaka mwingine uvumi mwingine;
uvumi wa ukatili katika nchi,
mtawala mmoja dhidi ya mtawala mwingine.
47Kweli siku zaja,
nitakapoadhibu sanamu za Babuloni;
nchi yake yote itatiwa aibu,
watu wake wote watauawa humohumo.
48Kisha mbingu, dunia na vyote vilivyomo
vitaimba kwa furaha kuhusu kuanguka kwa Babuloni,
waangamizi watakapofika kutoka kaskazini kuushambulia.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
49Babuloni umesababisha vifo duniani kote;
sasa wenyewe utaangamizwa kwa mauaji ya Israeli.
50“Nyinyi mlinusurika kifo,
ondokeni sasa, wala msisitesite!
Ingawa mko nchi ya mbali mkumbukeni Mwenyezi-Mungu,
ukumbukeni pia mji wa Yerusalemu.
51Mnasema: ‘Tumeaibishwa na kufadhaishwa;
aibu imezifunika nyuso zetu,
kwa sababu wageni wameingia
katika sehemu takatifu za nyumba ya Mwenyezi-Mungu.’
52“Kwa hiyo, wakati unakuja,
nasema mimi Mwenyezi-Mungu,
ambapo nitaviadhibu vinyago vya Babuloni,
na majeruhi watapiga kite katika nchi yake yote.
53Ingawa Babuloni atapanda mpaka mbinguni,
na kuziimarisha ngome zake ndefu,
waangamizi watakuja kutoka kwangu kumvamia.
2Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
Maangamizi zaidi juu ya Babuloni
54“Sikiliza! Kilio kinasikika kutoka Babuloni!
Kishindo cha maangamizi makubwa
kutoka nchi ya Wakaldayo!
55Maana mimi Mwenyezi-Mungu naiangamiza Babuloni,
na kuikomesha kelele yake kubwa.
Adui ananguruma kama mawimbi ya maji mengi,
sauti ya kishindo chao inaongezeka.
56Naam, mwangamizi anaijia Babuloni;
askari wake wametekwa,
pinde zao zimevunjwavunjwa.
Mimi Mwenyezi-Mungu ni Mungu mwenye kuadhibu,
hakika mimi nitalipiza kisasi kamili.
57Nitawalewesha wakuu na wenye hekima wake,
watawala wake, madiwani na askari wake;
watalala usingizi wa milele wasiinuke tena.
Nasema mimi mfalme ambaye jina langu ni Mwenyezi-Mungu wa Majeshi.
58“Mimi Mwenyezi-Mungu wa Majeshi nasema:
Ukuta mpana wa Babuloni
utabomolewa mpaka chini,
na malango yake marefu
yatateketezwa kwa moto.
Watu wanafanya juhudi za bure,
mataifa yanajichosha maana mwisho wao ni motoni!”
Ujumbe wa Yeremia unapelekwa Babuloni
59Mnamo mwaka wa nne wa utawala wake, mfalme Sedekia alikwenda Babuloni pamoja na ofisa wa askari wake aitwaye Seraya mwana wa Neria na mjukuu wa Maseya. Kutokana na fursa hiyo mimi Yeremia nilimpa Seraya ujumbe. 60Nilikuwa nimeandika kitabuni maafa yote niliyotangaza juu ya Babuloni na pia maneno mengine kuhusu Babuloni. 61Nilimwambia Seraya: “Utakapofika Babuloni ni lazima uwasomee wote ujumbe huu. 62Kisha umalizie na maneno haya: ‘Ee Mwenyezi-Mungu, wewe umesema kwamba utapaharibu mahali hapa hata pasikaliwe na kiumbe chochote, mwanadamu au mnyama, na kwamba nchi hii itakuwa jangwa milele.’ 63Utakapomaliza kusoma kitabu hiki, kifungie jiwe, kisha ukitumbukize katikati ya mto Eufrate, ukisema: 64‘Hivi ndivyo mji wa Babuloni utakavyozama, wala hautainuka tena, kwa sababu ya maafa ambayo Mwenyezi-Mungu anauletea.’”#51:64 anauletea: Kiebrania: Anayouletea, nao watachoka. Mwisho wa maneno ya Yeremia.

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 51: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia