Zaburi 52:1-9
Zaburi 52:1-9 BHN
Mbona, ewe jitu, wajivunia ubaya wako dhidi ya wenye kumcha Mungu? Kila wakati unawaza maangamizi; ulimi wako ni kama wembe mkali! Unafikiria tu kutenda mabaya. Wewe wapenda uovu kuliko wema, wapenda uongo kuliko ukweli. Ewe mdanganyifu mkuu, wapenda mambo ya kuangamiza wengine. Kwa hivyo Mungu atakuangamiza milele, atakunyakua na kukuondoa nyumbani mwako; atakungoa katika nchi ya walio hai. Waadilifu wataona hayo na kuogopa, kisha watakucheka na kusema: “Tazameni yaliyompata mtu huyu! Yeye hakutaka Mungu awe kimbilio lake; bali alitegemea wingi wa mali yake, na kutafuta humo usalama wake!” Lakini mimi ni kama mzeituni mbichi, unaostawi katika nyumba ya Mungu. Nazitegemea fadhili zake milele na milele. Ee Mungu, nitakushukuru daima, kwa ajili ya mambo uliyofanya. Nitatangaza kwamba wewe ni mwema, mbele ya watu wako waaminifu.