Zaburi 146:1-10
Zaburi 146:1-10 BHN
Msifuni Mwenyezi-Mungu! Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee nafsi yangu! Nitamsifu Mwenyezi-Mungu maisha yangu yote; nitamwimbia Mungu wangu muda wote niishipo. Msiwategemee wakuu wa dunia; hao ni binadamu tu, hawawezi kuokoa. Binadamu akitoa pumzi yake ya mwisho, anarudi mavumbini alimotoka; na hapo mipango yake yote hutoweka. Heri mtu anayesaidiwa na Mungu wa Yakobo, mtu aliyeweka tumaini lake kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, aliyeumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo. Yeye hushika ahadi yake milele. Yeye huwapatia wanaoonewa haki zao, huwapa wenye njaa chakula. Mwenyezi-Mungu huwapa wafungwa uhuru, huwafungua macho vipofu. Mwenyezi-Mungu huwainua waliokandamizwa; huwapenda watu walio waadilifu. Mwenyezi-Mungu huwalinda wageni, huwategemeza wajane na yatima; lakini huipotosha njia ya waovu. Mwenyezi-Mungu atawala milele, Mungu wako, ee Siyoni, ni mfalme vizazi vyote! Msifuni Mwenyezi-Mungu!