Zaburi 146:1-10
Zaburi 146:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Msifuni Mwenyezi-Mungu! Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee nafsi yangu! Nitamsifu Mwenyezi-Mungu maisha yangu yote; nitamwimbia Mungu wangu muda wote niishipo. Msiwategemee wakuu wa dunia; hao ni binadamu tu, hawawezi kuokoa. Binadamu akitoa pumzi yake ya mwisho, anarudi mavumbini alimotoka; na hapo mipango yake yote hutoweka. Heri mtu anayesaidiwa na Mungu wa Yakobo, mtu aliyeweka tumaini lake kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, aliyeumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo. Yeye hushika ahadi yake milele. Yeye huwapatia wanaoonewa haki zao, huwapa wenye njaa chakula. Mwenyezi-Mungu huwapa wafungwa uhuru, huwafungua macho vipofu. Mwenyezi-Mungu huwainua waliokandamizwa; huwapenda watu walio waadilifu. Mwenyezi-Mungu huwalinda wageni, huwategemeza wajane na yatima; lakini huipotosha njia ya waovu. Mwenyezi-Mungu atawala milele, Mungu wako, ee Siyoni, ni mfalme vizazi vyote! Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Zaburi 146:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Haleluya. Ee nafsi yangu, umsifu BWANA. Nitamsifu BWANA muda ninaoishi, Nitamwimbia Mungu wangu ningali ni hai. Msiwatumainie wakuu, Wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake. Pumzi yake inapomtoka, anarudi katika udongo wake, Siku iyo hiyo mipango yake hutoweka. Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake, Na tumaini lake ni kwa BWANA, Mungu wake, Aliyezifanya mbingu na nchi, Bahari na vitu vyote vilivyomo. Huishika kweli milele, Huwafanyia hukumu walioonewa, Huwapa wenye njaa chakula; BWANA hufungua waliofungwa; BWANA huwafumbua macho waliopofuka; BWANA huwainua walioinama; BWANA huwapenda wenye haki; BWANA huwahifadhi wageni; Huwategemeza yatima na mjane; Bali njia ya wasio haki huiharibu. BWANA atamiliki milele, Mungu wako, Ee Sayuni, kwa vizazi vyote. Haleluya.
Zaburi 146:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Haleluya. Ee nafsi yangu, umsifu BWANA. Nitamsifu BWANA muda ninaoishi, Nitamwimbia Mungu wangu ningali ni hai. Msiwatumainie wakuu, Wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake. Pumzi yake hutoka, huurudia udongo wake, Siku hiyo mawazo yake yapotea. Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake, Na tumaini lake ni kwa BWANA, Mungu wake, Aliyezifanya mbingu na nchi, Bahari na vitu vyote vilivyomo. Huishika kweli milele, Huwafanyia hukumu walioonewa, Huwapa wenye njaa chakula; BWANA hufungua waliofungwa; BWANA huwafumbua macho waliopofuka; BWANA huwainua walioinama; BWANA huwapenda wenye haki; BWANA huwahifadhi wageni; Huwategemeza yatima na mjane; Bali njia ya wasio haki huipotosha. BWANA atamiliki milele, Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. Haleluya.
Zaburi 146:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Msifuni BWANA! Ee nafsi yangu, umsifu BWANA, Nitamsifu BWANA maisha yangu yote; nitamwimbia Mungu wangu sifa wakati wote ningali hai. Usiweke tumaini lako kwa wakuu, kwa wanadamu ambao hufa, ambao hawawezi kuokoa. Roho yao itokapo hurudi mavumbini, siku hiyo hiyo mipango yao yote hukoma. Heri yeye ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake, ambaye tumaini lake ni katika BWANA, Mungu wake, Muumba wa mbingu na nchi, na bahari na vyote vilivyomo: BWANA anayedumu kuwa mwaminifu milele na milele. Naye huwapatia haki waliodhulumiwa, na kuwapa wenye njaa chakula. BWANA huwaweka wafungwa huru, BWANA huwafumbua vipofu macho, BWANA huwainua waliolemewa na mizigo yao, BWANA huwapenda wenye haki. BWANA huwalinda wageni na kuwategemeza yatima na wajane, lakini hupinga njia za waovu. BWANA atamiliki milele, Mungu wako, ee Sayuni, kwa vizazi vyote.