Maombolezo 3:22-66
Maombolezo 3:22-66 BHN
Kwamba fadhili za Mwenyezi-Mungu hazikomi, huruma zake hazina mwisho. Kila kunapokucha ni mpya kabisa, uaminifu wake ni mkuu mno. Mwenyezi-Mungu ndiye hazina yangu hivyo nitamwekea tumaini langu. Mwenyezi-Mungu ni mwema kwa wanaomtegemea, ni mwema kwa wote wanaomtafuta. Ni vema mtu kungojea kwa saburi ukombozi utokao kwa Mwenyezi-Mungu. Ni vema mtu kujifunza uvumilivu tangu wakati wa ujana wake. Heri kukaa peke na kimya, mazito yanapompata kutoka kwa Mungu. Yampasa kuinama na kujinyenyekesha, huenda ikawa tumaini bado lipo. Yampasa kumgeuzia shavu mwenye kumpiga, na kuwa tayari kupokea matusi yake. Mwenyezi-Mungu hatatutupa milele. Ingawa atufanya tuhuzunike, atakuwa na huruma tena kadiri ya wingi wa fadhili zake. Yeye hapendelei kuwatesa wala kuwahuzunisha wanadamu. Wafungwa wote nchini wanapodhulumiwa na kupondwa; haki za binadamu zinapopotoshwa mbele yake Mungu Mkuu, kesi ya mtu inapopotoshwa mahakamani, je, Mwenyezi-Mungu haoni hayo? Nani awezaye kuamuru kitu kifanyike Mwenyezi-Mungu asipopanga iwe hivyo? Maafa na mema hutokea tu kwa amri yake Mungu Mkuu. Kwa nini mtu anung'unike, ikiwa ameadhibiwa kwa dhambi zake? Na tupime na kuchunguza mwenendo wetu, tupate kumrudia Mwenyezi-Mungu. Tumfungulie Mungu huko mbinguni mioyo yetu na kumwomba: “Sisi tulikukosea na kukuasi nawe bado hujatusamehe. “Umejizungushia hasira yako ukatufuatia, ukatuua bila huruma. Umejizungushia wingu zito, sala yeyote isiweze kupenya humo. Umetufanya kuwa takataka na uchafu miongoni mwa watu wa mataifa. “Maadui zetu wote wanatuzomea. Kitisho na hofu vimetuandama, tumepatwa na maafa na maangamizi. Macho yangu yabubujika mito ya machozi kwa sababu ya kuangamizwa kwa watu wangu. “Machozi yatanitoka bila kikomo, mpaka Mwenyezi-Mungu kutoka huko mbinguni aangalie chini na kuona. Nalia na kujaa majonzi, kuona yaliyowapata kina mama wa mji wangu. “Nimewindwa kama ndege na hao wanichukiao bila sababu. Walinitupa shimoni nikiwa hai na juu yangu wakarundika mawe. Maji yalianza kunifunika kichwa, nami nikafikiri, ‘Huu ni mwisho wangu.’ “Kutoka chini shimoni nilikulilia ee Mwenyezi-Mungu. Wewe umenisikia nikikulilia: ‘Usiache kusikia kilio changu cha msaada bali unipatie nafuu.’ Nilipokuita ulinijia karibu ukaniambia, ‘Usiogope!’ “Umenitetea katika kisa changu ee Mwenyezi-Mungu, umeyakomboa maisha yangu. Umeuona uovu niliotendewa ee Mwenyezi-Mungu, uniamulie kwa wema kisa changu. Umeuona uovu wa maadui zangu, na mipango yao yote ya hila dhidi yangu. “Umesikia matukano yao ee Mwenyezi-Mungu, na mipango yao yote ya hila dhidi yangu. Maneno na mawazo ya maadui zangu siku nzima ni juu ya kuniangamiza mimi. Wakati wote, wamekaa au wanakwenda, mimi ndiye wanayemzomea. Uwalipize, ee Mwenyezi-Mungu kadiri ya hayo matendo yao, kadiri ya mambo waliyotenda wenyewe. Uipumbaze mioyo yao, na laana yako iwashukie. Uwafuatie kwa hasira, uwaangamize, uwafanye watoweke ulimwenguni.”







