Maombolezo 3:22-66
Maombolezo 3:22-66 NENO
Kwa sababu ya upendo mkuu wa BWANA, hatuangamii, kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe. Ni mpya kila asubuhi, uaminifu wako ni mkuu. Nimeiambia nafsi yangu, “BWANA ni fungu langu, kwa hiyo nitamngojea.” BWANA ni mwema kwa wale wanaomtumaini, na kwa yule anayemtafuta; ni vyema kungojea kwa utulivu kwa ajili ya wokovu wa BWANA. Ni vyema mtu kuchukua nira bado angali kijana. Na akae peke yake awe kimya, kwa maana BWANA ameiweka juu yake. Hata azike uso wake mavumbini bado tumaini litakuwepo. Na atoe shavu lake kwa yule ampigaye, na ajazwe na aibu. Kwa kuwa watu hawakatiliwi mbali na Bwana milele. Ingawa huleta huzuni, ataonesha huruma, kwa kuwa upendo wake usiokoma ni mkuu. Kwa maana hapendi kuwaletea mateso au huzuni watoto wa wanadamu. Kuwaponda chini ya nyayo wafungwa wote katika nchi, Kumnyima mtu haki zake mbele za Aliye Juu Sana, kumnyima mtu haki: Je, Bwana asione mambo kama haya? Nani awezaye kusema nalo likatendeka kama Bwana hajaamuru? Je, si ni kwenye kinywa cha Aliye Juu Sana ndiko yatokako maafa na mambo mema? Je, mwanadamu yeyote aliye hai aweza kulalamika wakati anapoadhibiwa kwa ajili ya dhambi zake? Tuzichunguze njia zetu na kuzijaribu, na tumrudie BWANA Mungu. Tuinue mioyo yetu pamoja na mikono yetu kwa Mungu mbinguni, na tuseme: “Tumetenda dhambi na kuasi nawe hujasamehe. “Umejifunika mwenyewe kwa hasira na kutufuatilia; umetuchinja bila huruma. Unajifunika mwenyewe kwa wingu, ili pasiwe na ombi litakaloweza kupenya. Umetufanya takataka na uchafu miongoni mwa mataifa. “Adui zetu wote wamefumbua vinywa vyao wazi dhidi yetu. Tumeteseka kwa hofu kuu na shida ya ghafula, uharibifu na maangamizi.” Vijito vya machozi vinatiririka kutoka machoni mwangu, kwa sababu watu wangu wameangamizwa. Macho yangu yatatiririka machozi bila kukoma, bila kupata nafuu, hadi BWANA atazame chini kutoka mbinguni na kuona. Lile ninaloliona huniletea huzuni nafsini kwa sababu ya wanawake wote wa mji wangu. Wale waliokuwa adui zangu bila sababu wameniwinda kama ndege. Walijaribu kukomesha maisha yangu ndani ya shimo na kunitupia mawe; maji yalifunika juu ya kichwa changu, nami nikafikiri nilikuwa karibu kukatiliwa mbali. Nililiitia jina lako, Ee BWANA, kutoka vina vya shimo. Ulisikia ombi langu: “Usikizibie masikio yako kilio changu nikuombapo msaada.” Ulikuja karibu nilipokuita, nawe ukasema, “Usiogope.” Ee Bwana, ulichukua shauri langu, ukaukomboa uhai wangu. Umeona, Ee BWANA, ubaya niliotendewa. Tetea shauri langu! Umeona kina cha kisasi chao, mashauri yao yote mabaya dhidi yangu. Ee BWANA, umesikia matukano yao, mashauri yao yote mabaya dhidi yangu: kile adui zangu wanachonongʼona na kunungʼunikia dhidi yangu mchana kutwa. Watazame! Wakiwa wameketi au wamesimama, wananidhihaki katika nyimbo zao. Uwalipe kile wanachostahili, Ee BWANA, kwa yale ambayo mikono yao imetenda. Weka pazia juu ya mioyo yao, laana yako na iwe juu yao! Wafuatilie katika hasira na uwaangamize chini ya mbingu za BWANA.







