Zaburi 107:1-22
Zaburi 107:1-22 SRUV
Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. Na waseme hivi waliokombolewa na BWANA, Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi. Akawakusanya kutoka nchi zote, Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini. Walitangatanga jangwani katika njia ya nyika; Hawakuona mji wa kukaa. Waliona njaa na kiu, Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Akawaongoza kwa njia ya kunyoka, Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa. Na wamshukuru BWANA, kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Maana hushibisha nafsi yenye shauku, Na nafsi yenye njaa huijaza mema. Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na minyororo, Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu, Wakalidharau shauri lake Aliye Juu. Hata akawadhili moyo kwa taabu, Wakajikwaa, wala pasiwe na wa kuwasaidia. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya kutoka kwa shida zao. Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti, Akaivunja minyororo yao. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Maana ameivunja milango ya shaba, Ameyakata mapingo ya chuma. Wapumbavu, kwa sababu ya ukosaji wao, Na kwa sababu ya maovu yao, hujitesa. Nafsi zao zachukia kila namna ya chakula, Wameyakaribia malango ya mauti. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya kutoka kwa shida zao. Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Na wamtolee dhabihu za kushukuru, Na kuyasimulia matendo yake kwa kuimba.