Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 107:1-22

Zaburi 107:1-22 NENO

Mshukuruni BWANA, kwa kuwa yeye ni mwema, fadhili zake zadumu milele. Waliokombolewa wa BWANA na waseme hivi, wale aliowaokoa kutoka mkono wa adui, wale aliowakusanya kutoka nchi mbalimbali, kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini. Baadhi yao walitangatanga jangwani, hawakuona njia ya kuwafikisha mji ambao wangeweza kuishi. Walikuwa na njaa na kiu, nafsi zao zikadhoofika. Ndipo walipomlilia BWANA katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao. Akawaongoza kwa njia iliyo sawa hadi mji ambao wangeweza kuishi. Basi na wamshukuru BWANA kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu, kwa maana yeye humtosheleza mwenye kiu, na kumshibisha mwenye njaa kwa vitu vyema. Wengine walikaa gizani na katika huzuni kuu, wafungwa wakiteseka katika minyororo, kwa sababu waliasi dhidi ya maneno ya Mungu, na kudharau ushauri wa Aliye Juu Sana. Aliwatumikisha kwa kazi ngumu; walijikwaa na hapakuwa na mtu wa kuwasaidia. Ndipo walipomlilia BWANA katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao. Akawatoa katika giza na huzuni kuu na akavunja minyororo yao. Basi na wamshukuru BWANA kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu, kwa kuwa yeye huvunja malango ya shaba na kukata mapingo ya chuma. Wengine wakawa wapumbavu kutokana na uasi wao, wakapata mateso kwa sababu ya uovu wao. Wakachukia kabisa vyakula vyote, wakakaribia malango ya mauti. Ndipo walipomlilia BWANA katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao. Akalituma neno lake na kuwaponya, akawaokoa kutoka maangamizi yao. Basi na wamshukuru BWANA kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu. Na watoe dhabihu za kushukuru, na wasimulie matendo yake kwa nyimbo za furaha.