Zaburi 107:1-22
Zaburi 107:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake zadumu milele! Semeni hivyo, enyi mliokombolewa na Mwenyezi-Mungu, watu ambao aliwaokoa katika taabu, akawakusanyeni kutoka nchi za kigeni: Kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini. Baadhi walitangatanga katika jangwa tupu, wasiweze kufikia mji wa kukaa. Waliona njaa na kiu; wakavunjika moyo kabisa. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Aliwaongoza katika njia iliyonyoka, mpaka wakaufikia mji wa kukaa. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Yeye huwatosheleza walio na kiu; na wenye njaa huwashibisha mema. Baadhi waliishi katika giza na ukiwa, wafungwa katika mateso na minyororo, kwa sababu waliasi maagizo ya Mungu, na kuyapuuza mashauri yake Mungu Mkuu. Walikuwa hoi kwa kazi ngumu, wakaanguka chini, pasiwe na wa kuwasaidia. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Aliwatoa katika giza na ukiwa, na minyororo yao akaivunjavunja. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Yeye huvunja na kufungua milango ya shaba, na kukatakata fito za chuma. Baadhi walipumbaa kwa sababu ya dhambi zao, waliteseka kwa sababu ya uovu wao; chakula kikawa kinyaa kwao, wakawa nusura wafe. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Kwa neno lake aliwaponya, akawaokoa wasiangamie. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Wamtolee tambiko za shukrani; wasimulie matendo yake kwa nyimbo za shangwe.
Zaburi 107:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. Na waseme hivi waliokombolewa na BWANA, Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi. Akawakusanya kutoka nchi zote, Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini. Walitangatanga jangwani katika njia ya nyika; Hawakuona mji wa kukaa. Waliona njaa na kiu, Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Akawaongoza kwa njia ya kunyoka, Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa. Na wamshukuru BWANA, kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Maana hushibisha nafsi yenye shauku, Na nafsi yenye njaa huijaza mema. Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na minyororo, Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu, Wakalidharau shauri lake Aliye Juu. Hata akawadhili moyo kwa taabu, Wakajikwaa, wala pasiwe na wa kuwasaidia. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya kutoka kwa shida zao. Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti, Akaivunja minyororo yao. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Maana ameivunja milango ya shaba, Ameyakata mapingo ya chuma. Wapumbavu, kwa sababu ya ukosaji wao, Na kwa sababu ya maovu yao, hujitesa. Nafsi zao zachukia kila namna ya chakula, Wameyakaribia malango ya mauti. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya kutoka kwa shida zao. Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Na wamtolee dhabihu za kushukuru, Na kuyasimulia matendo yake kwa kuimba.
Zaburi 107:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. Na waseme hivi waliokombolewa na BWANA, Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi. Akawakusanya kutoka nchi zote, Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini. Walitanga-tanga jangwani katika njia ya nyika; Hawakuona mji wa kukaa. Waliona njaa, waliona na kiu, Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Akawaongoza kwa njia ya kunyoka, Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa. Na wamshukuru BWANA, kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Maana hushibisha nafsi yenye shauku, Na nafsi yenye njaa huijaza mema. Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na chuma, Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu, Wakalidharau shauri lake Aliye juu. Hata akawadhili moyo kwa taabu, Wakajikwaa wala hakuna msaidizi. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti, Akayavunja mafungo yao. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Maana ameivunja milango ya shaba, Ameyakata mapingo ya chuma. Wapumbavu, kwa sababu ya ukosaji wao, Na kwa sababu ya maovu yao, hujitesa. Nafsi zao zachukia kila namna ya chakula, Wameyakaribia malango ya mauti. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Na wamtolee dhabihu za kushukuru, Na kuyasimulia matendo yake kwa kuimba.
Zaburi 107:1-22 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mshukuruni BWANA, kwa kuwa yeye ni mwema, fadhili zake zadumu milele. Waliokombolewa wa BWANA na waseme hivi, wale aliowaokoa kutoka mkono wa adui, wale aliowakusanya kutoka nchi mbalimbali, kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini. Baadhi yao walitangatanga jangwani, hawakuona njia ya kuwafikisha mji ambao wangeweza kuishi. Walikuwa na njaa na kiu, nafsi zao zikadhoofika. Ndipo walipomlilia BWANA katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao. Akawaongoza kwa njia iliyo sawa hadi mji ambao wangeweza kuishi. Basi na wamshukuru BWANA kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu, kwa maana yeye humtosheleza mwenye kiu, na kumshibisha mwenye njaa kwa vitu vyema. Wengine walikaa gizani na katika huzuni kuu, wafungwa wakiteseka katika minyororo, kwa sababu waliasi dhidi ya maneno ya Mungu, na kudharau ushauri wa Aliye Juu Sana. Aliwatumikisha kwa kazi ngumu; walijikwaa na hapakuwa na mtu wa kuwasaidia. Ndipo walipomlilia BWANA katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao. Akawatoa katika giza na huzuni kuu na akavunja minyororo yao. Basi na wamshukuru BWANA kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu, kwa kuwa yeye huvunja malango ya shaba na kukata mapingo ya chuma. Wengine wakawa wapumbavu kutokana na uasi wao, wakapata mateso kwa sababu ya uovu wao. Wakachukia kabisa vyakula vyote, wakakaribia malango ya mauti. Ndipo walipomlilia BWANA katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao. Akalituma neno lake na kuwaponya, akawaokoa kutoka maangamizi yao. Basi na wamshukuru BWANA kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu. Na watoe dhabihu za kushukuru, na wasimulie matendo yake kwa nyimbo za furaha.