Mithali 26:13-22
Mithali 26:13-22 SRUV
Mtu mvivu husema, Simba yuko njiani, Simba yuko katika njia kuu. Kama vile mlango ugeukavyo katika bawaba zake; Kadhalika mtu mvivu katika kitanda chake. Mtu mvivu hutia mkono wake katika sahani; Kwamchosha kuupeleka tena kinywani pake. Mtu mvivu ni mwenye hekima machoni pake, Kuliko watu saba wawezao kutoa sababu. Mtu apitaye na kujisumbua kwa ugomvi usio wake; Ni kama mtu ashikaye mbwa kwa masikio yake. Kama mtu mwenye wazimu atupaye mienge, Na mishale, na mauti; Ndivyo alivyo amdanganyaye mwenzake, Na kusema, Je! Sikufanya mzaha tu? Moto hufa kwa kukosa kuni; Na bila mchongezi fitina hukoma. Kama makaa juu ya makaa yanayowaka, Na kama kuni juu ya moto; Ndivyo mtu mgomvi achocheavyo uadui. Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo. Nayo hushukia pande za ndani za tumbo.