Mithali 26:13-22
Mithali 26:13-22 NENO
Mvivu husema, “Yuko simba barabarani, simba mkali anazunguka mitaa!” Kama vile mlango ugeukavyo kwenye bawaba zake, ndivyo mvivu ajigeuzavyo kitandani mwake. Mtu mvivu hutumbukiza mkono wake kwenye sahani, naye huchoka kuupeleka kwenye kinywa chake. Mtu mvivu ni mwenye hekima machoni pake mwenyewe, kuliko watu saba wawezao kujibu kwa busara. Kama yeye amkamataye mbwa kwa masikio, ndivyo alivyo mtu apitaye njiani na kujiingiza kwenye ugomvi usiomhusu. Kama mwendawazimu atupaye mishale ya moto ya kufisha, ndivyo alivyo mtu amdanganyaye jirani yake na kusema, “Nilikuwa nikifanya mzaha tu!” Bila kuni moto huzimika; pasipo uchongezi ugomvi humalizika. Kama makaa juu ya makaa yanayowaka, na kama kuni kwenye moto, ndivyo alivyo mtu mgomvi kwa kuchochea ugomvi. Maneno ya mchongezi ni kama chakula kitamu; huingia sehemu za ndani sana za mtu.