Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya BWANA.
Heri wazitiio shuhuda zake,
Wamtafutao kwa moyo wote.
Naam, hawakutenda ubatili,
Wamekwenda katika njia zake.
Wewe umetuamuru mausia yako,
Ili sisi tuyatii sana.
Ningependa njia zangu ziwe thabiti,
Nizitii amri zako.
Ndipo mimi sitaaibika,
Nikiyaangalia maagizo yako yote.
Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo,
Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako
Nitazitii amri zako,
Usiniache kabisa
Jinsi gani kijana aisafishe njia yake?
Kwa kutii, akilifuata neno lako.
Kwa moyo wangu wote nimekutafuta,
Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.
Moyoni mwangu nimeliweka neno lako,
Nisije nikakutenda dhambi.
Ee BWANA, umehimidiwa,
Unifundishe amri zako.
Kwa midomo yangu nimezisimulia
Hukumu zote za kinywa chako.
Nimeifurahia njia ya shuhuda zako
Kana kwamba ni mali mengi.
Nitayatafakari mausia yako,
Nami nitaziangalia njia zako.
Nitajifurahisha sana kwa amri zako,
Sitalisahau neno lako.
Umtendee mtumishi wako ukarimu,
Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.
Unifumbue macho yangu niyatazame
Maajabu yatokayo katika sheria yako.
Mimi ni mgeni katika nchi,
Usinifiche maagizo yako.
Roho yangu imepondeka kwa kutamani
Hukumu zako kila wakati.
Umewakemea wenye kiburi,
Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako.
Uniondolee laumu na dharau,
Kwa maana nimezishika shuhuda zako.
Wakuu nao waliketi wakaninena,
Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako.
Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu,
Na washauri wangu.
Nafsi yangu imeambatana na mavumbi,
Unihuishe sawasawa na neno lako.
Nalizisimulia njia zangu ukanijibu,
Unifundishe amri zako.
Unifahamishe njia ya mausia yako,
Nami nitayatafakari maajabu yako.
Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito,
Unitie nguvu sawasawa na neno lako.
Uniondolee njia ya uongo,
Unineemeshe kwa sheria yako.
Nimeichagua njia ya uaminifu,
Na kuziweka hukumu zako mbele yangu.
Nimeambatana na shuhuda zako,
Ee BWANA, usiniaibishe.
Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako,
Utakaponikunjua moyo wangu.