Hesabu 26:1-11
Hesabu 26:1-11 NENO
Baada ya hiyo tauni, BWANA akamwambia Musa na Eleazari mwana wa kuhani Haruni, “Hesabu jumuiya yote ya Waisraeli kufuatana na jamaa zao, wale wote wenye umri wa miaka ishirini na zaidi, wanaoweza kutumika katika jeshi la Israeli.” Hivyo Musa na kuhani Eleazari wakazungumza na watu kwenye nchi tambarare ya Moabu, ngʼambo ya Yordani kutokea Yeriko, wakasema, “Hesabuni wanaume wenye umri wa miaka ishirini na zaidi, kama BWANA alivyomwagiza Musa.” Hawa ndio Waisraeli waliotoka Misri: Wazao wa Reubeni, mwana mzaliwa wa kwanza wa Israeli, walikuwa: kutoka kwa Hanoki, ukoo wa Wahanoki; kutoka kwa Palu, ukoo wa Wapalu; kutoka kwa Hesroni, ukoo wa Wahesroni; kutoka kwa Karmi, ukoo wa Wakarmi. Hizi zilikuwa ndizo koo za Reubeni; wale waliohesabiwa walikuwa elfu arobaini na tatu mia saba na thelathini (43,730). Mwana wa Palu alikuwa Eliabu, nao wana wa Eliabu walikuwa Nemueli, Dathani na Abiramu. Hawa wawili Dathani na Abiramu ndio walikuwa maafisa wa jumuiya ambao walimwasi Musa na Haruni, na walikuwa miongoni mwa wafuasi wa Kora wakati walimwasi BWANA. Ardhi ilifunua kinywa chake na kuwameza pamoja na Kora, ambaye wafuasi wake walikufa wakati moto ulipowateketeza wanaume mia mbili na hamsini. Nao walikuwa kama alama ya onyo. Pamoja na hayo, hao ukoo wa Kora hawakufa.