Hesabu 26:1-11
Hesabu 26:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya yale maradhi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Eleazari mwana wa kuhani Aroni, “Hesabuni jumuiya yote ya Waisraeli, kila mtu kufuatana na jamaa yake. Wahesabuni watu wote wenye umri wa miaka ishirini na zaidi wanaofaa kwenda jeshini.” Mose na kuhani Eleazari wakazungumza na watu kwenye nchi tambarare za Moabu, ngambo ya mto Yordani, karibu na Yeriko, wakawaambia, “Hesabuni watu kuanzia na wenye umri wa miaka ishirini na zaidi, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.” Idadi ya Waisraeli waliotoka Misri ni hii: Kwanza ni kabila la Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo. Henoki, Palu, Hesroni na Karmi. Hizo ndizo koo za kabila la Reubeni. Idadi ya wanaume waliohesabiwa ni 43,730. Wazawa wa Palu walikuwa Eliabu, na wanawe Nemueli, Dathani na Abiramu. (Hawa wawili: Dathani na Abiramu, ndio waliokuwa wamechaguliwa miongoni mwa jumuiya, lakini wakampinga Mose na Aroni, na kujiunga na wafuasi wa Kora wakati walipomwasi Mwenyezi-Mungu. Wakati huo ardhi ilifunguka ikawameza, wakafa pamoja na Kora na wafuasi wake moto ulipoangamiza watu 250; wakawa onyo kwa watu. Pamoja na hayo wana wa Kora hawakufa.)
Hesabu 26:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa baada ya hilo pigo, BWANA akanena na Musa na Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, na kuwaambia, Fanya hesabu ya jumuiya yote ya wana wa Israeli, tangu umri wa miaka ishirini, na zaidi, kwa nyumba za baba zao, hao wote katika Israeli wawezao kutoka kuenenda vitani. Kisha Musa na Eleazari kuhani wakanena nao katika nchi tambarare za Moabu karibu na mto wa Yordani, huko Yeriko, wakawaambia, Fanyeni hesabu ya watu, kuanzia umri wa miaka ishirini, na zaidi; kama BWANA alivyomwagiza Musa na wana wa Israeli, hao waliotoka nchi ya Misri. Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Israeli, wana wa Reubeni; wa Hanoki, jamaa ya Wahanoki; na wa Palu, jamaa ya Wapalu; na wa Hesroni, jamaa ya Wahesroni; na wa Karmi, jamaa ya Wakarmi. Hizi ndizo jamaa za Wareubeni; na hao waliohesabiwa kwao walikuwa elfu arubaini na tatu, mia saba na thelathini. Na wana wa Palu; Eliabu. Na wana wa Eliabu; Nemueli, na Dathani, na Abiramu. Hawa ndio Dathani na Abiramu waliochaguliwa na mkutano, ambao walishindana na Musa na Haruni katika mkutano wa Kora, hapo waliposhindana na BWANA; nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza pamoja na Kora, mkutano huo ulipokufa; wakati moto ulipowateketeza watu mia mbili na hamsini, nao wakawa ishara. Hata hivyo, hao wana wa Kora hawakufa.
Hesabu 26:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa baada ya hilo pigo, BWANA akanena na Musa na Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, na kuwaambia, Fanya jumla ya mkutano wote wa wana wa Israeli, tangu umri wa miaka ishirini, na zaidi, kwa nyumba za baba zao, hao wote katika Israeli wawezao kutoka kuenenda vitani. Kisha Musa na Eleazari kuhani wakanena nao katika nchi tambarare za Moabu karibu na mto wa Yordani, huko Yeriko, wakawaambia, Fanyeni jumla ya watu, tangu umri wa miaka ishirini, na zaidi; kama BWANA alivyomwagiza Musa na wana wa Israeli, hao waliotoka nchi ya Misri. Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Israeli, wana wa Reubeni; wa Hanoki, jamaa ya Wahanoki; na wa Palu, jamaa ya Wapalu; na wa Hesroni, jamaa ya Wahesroni; na wa Karmi, jamaa ya Wakarmi. Hizi ndizo jamaa za Wareubeni; na hao waliohesabiwa kwao walikuwa arobaini na tatu elfu na mia saba na thelathini. Na wana wa Palu; Eliabu. Na wana wa Eliabu; Nemueli, na Dathani, na Abiramu. Hawa ndio Dathani na Abiramu waliochaguliwa na mkutano, ambao walishindana na Musa na Haruni katika mkutano wa Kora, hapo waliposhindana na BWANA; nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza pamoja na Kora, mkutano huo ulipokufa; wakati moto ulipowateketeza watu mia mbili na hamsini, nao wakawa ishara. Pamoja na hayo, hao wana wa Kora hawakufa.
Hesabu 26:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya hiyo tauni, BWANA akamwambia Musa na Eleazari mwana wa kuhani Haruni, “Hesabu jumuiya yote ya Waisraeli kufuatana na jamaa zao, wale wote wenye umri wa miaka ishirini na zaidi, wanaoweza kutumika katika jeshi la Israeli.” Hivyo Musa na kuhani Eleazari wakazungumza na watu kwenye nchi tambarare ya Moabu, ngʼambo ya Yordani kutokea Yeriko, wakasema, “Hesabuni wanaume wenye umri wa miaka ishirini na zaidi, kama BWANA alivyomwagiza Musa.” Hawa ndio Waisraeli waliotoka Misri: Wazao wa Reubeni, mwana mzaliwa wa kwanza wa Israeli, walikuwa: kutoka kwa Hanoki, ukoo wa Wahanoki; kutoka kwa Palu, ukoo wa Wapalu; kutoka kwa Hesroni, ukoo wa Wahesroni; kutoka kwa Karmi, ukoo wa Wakarmi. Hizi zilikuwa ndizo koo za Reubeni; wale waliohesabiwa walikuwa elfu arobaini na tatu mia saba na thelathini (43,730). Mwana wa Palu alikuwa Eliabu, nao wana wa Eliabu walikuwa Nemueli, Dathani na Abiramu. Hawa wawili Dathani na Abiramu ndio walikuwa maafisa wa jumuiya ambao walimwasi Musa na Haruni, na walikuwa miongoni mwa wafuasi wa Kora wakati walimwasi BWANA. Ardhi ilifunua kinywa chake na kuwameza pamoja na Kora, ambaye wafuasi wake walikufa wakati moto ulipowateketeza wanaume mia mbili na hamsini. Nao walikuwa kama alama ya onyo. Pamoja na hayo, hao ukoo wa Kora hawakufa.