Isaya 32:1-8
Isaya 32:1-8 NENO
Tazama, mfalme atatawala kwa uadilifu na watawala watatawala kwa haki. Kila mtu atakuwa kama kivuli cha kujificha kutokana na upepo na kimbilio kutokana na dhoruba, kama vijito vya maji jangwani na kivuli cha mwamba mkubwa katika ardhi yenye kiu. Ndipo macho ya wale wanaoona hayatafumbwa tena, nayo masikio ya wale wanaosikia yatasikiliza. Moyo wa mtu mwenye hamaki utafahamu na kuelewa, nao ulimi wenye kigugumizi utanena kwa ufasaha. Mpumbavu hataitwa tena muungwana, wala mtu mbaya kabisa kupewa heshima ya juu. Kwa kuwa mpumbavu hunena upumbavu, moyo wake hushughulika na uovu: Hutenda mambo yasiyo ya kumcha Mungu, na hueneza habari za makosa kuhusu BWANA; yeye huwaacha wenye njaa bila kitu, na wenye kiu huwanyima maji. Taratibu za mtu mbaya kabisa ni ovu, hufanya mipango miovu ili kumwangamiza maskini kwa uongo, hata wakati hoja za mhitaji ni za haki. Lakini mtu muungwana hufanya mipango ya kiungwana, na kwa matendo ya kiungwana yeye hufanikiwa.


