Isaya 32:1-8
Isaya 32:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Kutatokea mfalme atakayetawala kwa uadilifu, nao viongozi wataongoza kwa kufuata haki. Kila mmoja atakuwa kama mahali pa kujikinga na upepo, kama mahali pa kujificha wakati wa tufani. Watakuwa kama vijito vya maji katika nchi kame, kama kivuli cha mwamba mkubwa jangwani. Macho hayatafumbwa tena, masikio yatabaki wazi. Wafanyao mambo kwa hamaki wataamua kwa busara, wenye kigugumizi wataongea sawasawa. Wapumbavu hawataitwa tena waungwana, wala walaghai hawataitwa tena waheshimiwa. Wapumbavu hunena upumbavu, na fikira zao hupanga kutenda uovu, kutenda mambo yasiyo mema, kusema mambo ya kumkufuru Mwenyezi-Mungu. Huwaacha wenye njaa bila chakula, na wenye kiu huwanyima kinywaji. Ulaghai wa walaghai ni mbaya; hao huzua visa viovu, na kumwangamiza maskini kwa maneno ya uongo, hata kama madai ya maskini ni halali. Lakini waungwana hutenda kiungwana, nao hutetea mambo ya kiungwana.
Isaya 32:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tazama, mfalme atamiliki kwa haki, na wakuu watatawala kwa hukumu. Na mwanadamu atakuwa kama mahali pa kujificha na upepo, na mahali pa kujisitiri na dhoruba; kama mito ya maji mahali pakavu, kama kivuli cha mwamba mkubwa katika nchi yenye uchovu. Tena macho yao waonao hayatakuwa na kiwi, na masikio yao wasikiao yatasikiliza. Tena moyo wa mtu mwenye hamaki utafahamu maarifa, na ndimi zao wenye kigugumizi zitakuwa tayari kunena sawasawa. Mpumbavu hataitwa tena muungwana, wala mlaghai hataitwa kuwa ni mheshimiwa. Maana mpumbavu atanena yaliyo upumbavu, na moyo wake utafanya maovu, ili kutenda hila na kusema yasiyo kweli juu ya BWANA, ili kuziacha nafsi za watu wenye njaa bila chakula, na kuwanyima kinywaji wenye kiu. Tena vyombo vyake mlaghai ni vibaya; hutunga hila mbaya, ili kuwaangamiza wanyonge kwa maneno ya uongo, mtu mhitaji ajaposema maneno yenye haki. Bali muungwana huwaza mambo ya kiungwana, naye hushika sana mambo ya kiungwana.
Isaya 32:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tazama, mfalme atamiliki kwa haki, na wakuu watatawala kwa hukumu. Na mwanadamu atakuwa kama mahali pa kujificha na upepo, na mahali pa kujisitiri na dhoruba; kama mito ya maji mahali pakavu, kama kivuli cha mwamba mkubwa katika nchi yenye uchovu. Tena macho yao waonao hayatakuwa na kiwi, na masikio yao wasikiao yatasikiliza. Tena moyo wa mtu mwenye hamaki utafahamu maarifa, na ndimi zao wenye kigugumizi zitakuwa tayari kunena sawasawa. Mpumbavu hataitwa tena mwungwana, wala ayari hatasemwa kwamba ni karimu. Maana mpumbavu atanena yaliyo upumbavu, na moyo wake utafanya maovu, ili kutenda hila na kusema yasiyo kweli juu ya BWANA, ili kuziacha nafsi za watu wenye njaa hazina kitu, na kukikomesha kinywaji chake mwenye kiu. Tena vyombo vyake ayari ni vibaya; hutunga hila mbaya, ili kuwaangamiza wanyonge kwa maneno ya uongo, mtu mhitaji ajaposema maneno yenye haki. Bali mwungwana huwaza mambo ya kiungwana, naye hushika sana mambo ya kiungwana.
Isaya 32:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Tazama, mfalme atatawala kwa uadilifu na watawala watatawala kwa haki. Kila mtu atakuwa kama kivuli cha kujificha kutokana na upepo na kimbilio kutokana na dhoruba, kama vijito vya maji jangwani na kivuli cha mwamba mkubwa katika ardhi yenye kiu. Ndipo macho ya wale wanaoona hayatafumbwa tena, nayo masikio ya wale wanaosikia yatasikiliza. Moyo wa mtu mwenye hamaki utafahamu na kuelewa, nao ulimi wenye kigugumizi utanena kwa ufasaha. Mpumbavu hataitwa tena muungwana, wala mtu mbaya kabisa kupewa heshima ya juu. Kwa kuwa mpumbavu hunena upumbavu, moyo wake hushughulika na uovu: Hutenda mambo yasiyo ya kumcha Mungu, na hueneza habari za makosa kuhusu BWANA; yeye huwaacha wenye njaa bila kitu, na wenye kiu huwanyima maji. Taratibu za mtu mbaya kabisa ni ovu, hufanya mipango miovu ili kumwangamiza maskini kwa uongo, hata wakati hoja za mhitaji ni za haki. Lakini mtu muungwana hufanya mipango ya kiungwana, na kwa matendo ya kiungwana yeye hufanikiwa.