Isaya 32:1-8
Isaya 32:1-8 SRUV
Tazama, mfalme atamiliki kwa haki, na wakuu watatawala kwa hukumu. Na mwanadamu atakuwa kama mahali pa kujificha na upepo, na mahali pa kujisitiri na dhoruba; kama mito ya maji mahali pakavu, kama kivuli cha mwamba mkubwa katika nchi yenye uchovu. Tena macho yao waonao hayatakuwa na kiwi, na masikio yao wasikiao yatasikiliza. Tena moyo wa mtu mwenye hamaki utafahamu maarifa, na ndimi zao wenye kigugumizi zitakuwa tayari kunena sawasawa. Mpumbavu hataitwa tena muungwana, wala mlaghai hataitwa kuwa ni mheshimiwa. Maana mpumbavu atanena yaliyo upumbavu, na moyo wake utafanya maovu, ili kutenda hila na kusema yasiyo kweli juu ya BWANA, ili kuziacha nafsi za watu wenye njaa bila chakula, na kuwanyima kinywaji wenye kiu. Tena vyombo vyake mlaghai ni vibaya; hutunga hila mbaya, ili kuwaangamiza wanyonge kwa maneno ya uongo, mtu mhitaji ajaposema maneno yenye haki. Bali muungwana huwaza mambo ya kiungwana, naye hushika sana mambo ya kiungwana.


