YouVersion Logo
Search Icon

Methali 23

23
1Ukiketi kula pamoja na mtawala,
usisahau hata kidogo uko pamoja na nani.
2Zuia sana hamu yako,
ikiwa wewe wapenda sana kula.
3Usitamani vyakula vyake vizuri,
maana vyaweza kukudanganya.
- 7 -
4Ikiwa unayo hekima ya kutosha,
usijitaabishe kutafuta utajiri.
5Kufumba na kufumbua utajiri hutoweka,
huwa kama umepata mabawa ghafla,
ukaruka na kutowekea angani kama tai.
- 8 -
6Usile chakula cha mtu bahili,
wala usitamani mapochopocho yake,
7maana moyoni mwake anahesabu unachokula.#23:7 maana … unachokula: Maana katika Kiebrania si dhahiri.
Atakuambia, “Kula, kunywa!”
Lakini moyoni mwake hayuko pamoja nawe.
8Utatapika vipande ulivyokula;
shukrani zako zote zitakuwa za bure.
- 9 -
9Usiseme maneno yako mbele ya mpumbavu,
maana atapuuza hekima ya maneno yako.
- 10 -
10Usiondoe alama ya mpaka wa zamani,
wala usiingilie mashamba ya yatima,
11maana Mungu, Mkombozi, ni mwenye nguvu,
naye ataitetea haki yao dhidi yako.
- 11 -
12Tumia akili zako kufuata mafundisho;
tumia masikio yako kusikiliza maarifa.
- 12 -
13Usiache kumrudi mtoto;
ukimchapa kiboko hatakufa.
14Ukimtandika kiboko,
utayaokoa maisha yake na kuzimu.
- 13 -
15Mwanangu, moyo wako ukiwa wenye busara,
moyo wangu pia utakuwa wenye furaha.
16Moyo wangu utashangilia,
mdomo wako utakaposema maneno yaliyo sawa.
- 14 -
17Moyo wako usiwaonee wivu wenye dhambi,
ila endelea kumcha Mwenyezi-Mungu siku zote.
18Hakika kuna kesho ya milele,
na tumaini lako halitakuwa bure.
- 15 -
19Sikia mwanangu, uwe na hekima;
fikiria sana jinsi unavyoishi.
20Usiwe mmoja wa walevi wa divai,
wala walafi wenye kupenda nyama,
21maana walevi na walafi wataishia kuwa maskini,
anayetumia siku yake kusinzia atavaa matambara.
- 16 -
22Msikilize baba yako aliyekuzaa,
wala usimdharau mama yako akizeeka.
23Nunua ukweli, wala usiuuze;
nunua hekima, mafunzo na busara.
24Baba wa mtoto mwadilifu atajaa furaha;
anayemzaa mtoto mwenye hekima atamfurahia.
25Wafurahishe baba na mama yako;
mama aliyekuzaa na afurahi.
- 17 -
26Mwanangu, nisikilize kwa makini,
shikilia mwenendo wa maisha yangu.
27Malaya ni shimo refu la kutega watu;
mwanamke mgeni ni kama kisima chembamba.
28Yeye hunyemelea kama mnyanganyi,
husababisha wanaume wengi kukosa uaminifu.
- 18 -
29Ni nani wapigao yowe?
Ni nani wenye huzuni?
Ni nani wenye ugomvi?
Ni nani walalamikao?
Ni nani wenye majeraha bila sababu?
Ni nani wenye macho mekundu?
30Ni wale ambao hawabanduki penye divai,
wale wakaao chonjo kuonja divai iliyokolezwa.
31Usiitamani divai hata kwa wekundu wake,
hata kama inametameta katika bilauri,
na kushuka taratibu unapoinywa.
32Mwishowe huuma kama nyoka;
huchoma kama nyoka mwenye sumu.
33Macho yako yataona mauzauza,
moyo wako utatoa mambo yaliyopotoka.
34Utakuwa kama mtu alalaye katikati ya bahari,
kama mtu alalaye juu ya mlingoti wa meli.
35Utasema, “Walinichapa, lakini sikuumia;
walinipiga, lakini sina habari.
Nitaamka lini?
Ngoja nitafute kinywaji kingine!”
- 19 -

Currently Selected:

Methali 23: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy