YouVersion Logo
Search Icon

Marko UTANGULIZI

UTANGULIZI
Injili ya Marko ni fupi kuliko zote, nayo yafikiriwa kuwa iliandikwa kabla ya hizo Injili nyingine tatu. Marko bila shaka alikuwa anafahamiana vizuri na viongozi kadha wa kadha wa jumuiya changa ya Kikristo. Katika Matendo ya Mitume anaitwa pia Yohane Marko. Aliandamana na Barnaba na Paulo katika safari yao ya kwanza ya kitume na kutokana na kutoelewana na Paulo, Marko aliandamana na Barnaba (Matendo 15:36-41). Marko huenda pia alikuwa na Petro huko Roma na jambo hili huenda ladhihirisha kwa nini Petro anapewa nafasi maalumu katika Injili hii. Labda Marko aliiandika Injili yake yapata mwaka 70 B.K. na aliiandika kwa ajili ya Wakristo walioongoka kutoka mataifa mengine na ambao hawakufahamu mengi juu ya desturi, mila na mapokeo ya Wayahudi.
Injili hii imeandikwa kwa mpango kamili na huenda ilitumiwa na waandishi wa Injili za Mathayo na Luka walipoandika habari zao juu ya Yesu Kristo. Marko anaonekana kutilia mkazo hasa matendo ya Yesu. Hana habari zozote juu ya kuzaliwa kwake Yesu wala juu ya orodha ya ukoo wake. Tangu mwanzoni mwa Injili picha tunayopewa juu ya Yesu ni ya mtu mwenye uwezo mkuu, ambaye anavunjilia mbali utawala wa Shetani na kwa matendo yake hata nguvu za maumbile zinalegea.
Jambo mojawapo la kushangaza ni kwamba tunahabarishwa kuwa Yesu mwenyewe hataki ajulikane kuwa yeye ni Masiha. Anawaamuru pepo wabaya wanyamaze, wasiseme habari zake; na wagonjwa aliowaponya, wasiseme habari zake; na hata Petro ambaye anakiri na kumtambua rasmi kuwa Masiha, anaambiwa asitoe habari hizo kwa mtu yeyote. Kwa nini? Yesu alitaka wasimseme alivyo kweli (7:36; 8:30) ili kuepa kueleweka vibaya, yaani kadiri Wayahudi walivyokuwa wanatazamia. Tena katika kujitaja yeye mwenyewe anatumia jina Mwana wa Mtu (2:10; linganisha na Mathayo 8:20). Hiyo ndiyo inayoitwa na wataalamu wa Maandiko Matakatifu kuwa “Siri ya Masiha.”
Katika Injili hii watu wanaelekezwa kwenye jambo muhimu la habari hizi, yaani mateso na kifo cha Yesu. Ni yule tu anayempokea na kumtambua Yesu aliyesulubiwa, ndiye anayejua Masiha au Kristo ni nani.

Currently Selected:

Marko UTANGULIZI: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy