YouVersion Logo
Search Icon

Yobu 32

32
Elihu anatoa hoja zake
(32:1–37:24)
1Basi hawa watu watatu: Elifazi, Bildadi na Sofari, wakaacha kumjibu Yobu kwa vile alijiona kuwa mwema. 2Ndipo Elihu, mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi#32:2 Buzi: Kabila moja la Kiarabu (taz Yer 25:23). wa ukoo wa Rama, akakasirika. Alimkasirikia Yobu kwa sababu Yobu alijiona yeye mwadilifu na sio Mungu. 3Pia, aliwakasirikia rafiki watatu wa Yobu kwa sababu hawakuwa na la kumjibu Yobu, na hivyo kuonesha kwamba Mungu amekosa.#32:3 kuonesha kwamba Mungu amekosa: Tafsiri hii yaambatana na kusahihishwa makala ya Kiebrania. 4Elihu alikuwa amekaa kimya wakati hao wazee waliposema na Yobu kwa kuwa yeye alikuwa kijana kuliko wao. 5Lakini alipoona hao watu watatu wameshindwa kumjibu Yobu, aliwaka hasira.
6Basi, Elihu mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi akaanza kusema:
“Mimi ni kijana, nyinyi ni wazee zaidi;
kwa hiyo niliogopa kuwaambieni mawazo yangu.
7Nilisema moyoni: ‘Waache wenye siku nyingi waseme,
wenye miaka mingi wafundishe hekima.’
8Lakini hiyo roho iliyomo ndani ya mtu,
hiyo pumzi ya Mungu Mwenye Nguvu,
ndio inayomwezesha mwanadamu kufahamu.
9Si lazima kuwa mzee ili uwe na hekima
wala wazee siyo wenye kufahamu lililo sawa.
10Kwa hiyo nasema, ‘Nisikilizeni,
acheni nami nitoe maoni yangu.’
11“Basi, mimi nilingojea mlichotaka kusema,
nilisikiliza misemo yenu ya hekima,
mlipokuwa mnajaribu kutafuta la kusema.
12Niliwasikiliza kwa makini sana,
lakini hakuna mmoja wenu aliyemshinda Yobu;
nyote mlishindwa kuyajibu maneno yake.
13Jihadharini msije mkasema, ‘Sasa tumepata hekima.
Atakayemshinda ni Mungu, sio binadamu.’
14Maneno ya Yobu hayakuwa kwa ajili yangu,
kwa hiyo sitamjibu kama mlivyomjibu nyinyi.
15“Nyinyi mmeduwaa; mmeshindwa,
nyinyi hamna cha kusema zaidi.
16Je, ningoje tu kwa vile hamsemi,
kwa sababu mnakaa tu bila kujibu kitu?
17Mimi pia nitatoa jibu langu;
mimi nitatoa pia maoni yangu.
18Ninayo maneno mengi sana,
roho yangu yanisukuma kusema.
19Moyo wangu umefurika kama divai iliyozibwa,
kama kiriba cha divai mpya tayari kupasuka.
20Ni lazima niseme ili nipate nafuu;
yanipasa kufungua kinywa changu na kujibu.
21Sitampendelea mtu yeyote
wala kutumia maneno ya kubembeleza mtu.
22Maana mimi sijui kubembeleza mtu,
la sivyo, Muumba wangu angeniangamiza.

Currently Selected:

Yobu 32: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy