YouVersion Logo
Search Icon

Yeremia 48

48
Moabu
1Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi:
“Ole watu wa Nebo, maana mji wake umeharibiwa!
Kiriathaimu umeaibishwa, umetekwa,
ngome yake imebomolewa mbali;
2fahari ya Moabu imetoweka.
Mpango ulifanywa huko Heshboni dhidi yake:
‘Haya! Tuwaangamize wasiwe tena taifa!’
Nawe Madmeni utanyamazishwa,
upanga utakufuatia.
3Sikiliza! Kilio kutoka Horonaimu:
‘Maangamizi na uharibifu mkubwa!’
4Moabu tayari imeangamizwa
kilio chake chasikika mpaka Soari.
5Walionusurika wanapanda kwenda Luhithi
huku wanalia kwa sauti.
Wanapoteremka kwenda Horonaimu,
wanasikia kilio cha uharibifu.
6Kimbieni! Jiokoeni wenyewe!
Kimbieni kama pundamwitu jangwani!
7“Moabu, ulitumainia ngome na hazina zako,
lakini sasa wewe pia utatekwa;
mungu wako Kemoshi atapelekwa uhamishoni
pamoja na makuhani na watumishi wake.
8Mwangamizi atapita katika kila mji,
hakuna mji utakaomwepa;
kila kitu mabondeni kitaangamia
nyanda za juu zitaharibiwa,
kama alivyosema Mwenyezi-Mungu.
9Mchimbieni Moabu kaburi,
maana kuangamia kwake ni hakika;
miji yake itakuwa tupu,
bila mkazi hata mmoja.
10Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya Mwenyezi-Mungu kwa ulegevu; alaaniwe anayezuia upanga wake usimwage damu!
11Moabu amestarehe tangu ujana wake,
ametulia kama divai katika gudulia.
Hajamiminiwa toka chombo hata chombo,
hajapata kuchukuliwa uhamishoni.
Kwa hiyo yungali na ladha yake,
harufu yake nzuri haijabadilika kamwe.
12“Kwa hiyo, wakati waja, nasema mimi Mwenyezi-Mungu ambapo nitampelekea wamiminaji ambao wataimimina divai yake. Wataimwaga yote kutoka vyombo vyake na kuvivunja vipandevipande. 13Hapo Wamoabu watamwonea aibu mungu wao Kemoshi, kama vile watu wa Israeli walivyomwonea aibu Betheli, mungu waliyemtegemea.
14Mwawezaje kusema: ‘Sisi ni mashujaa,
na watu wenye nguvu nyingi za vita?’
15Mwangamizi wa Moabu na miji yake amewasili
vijana wake wazuri wamechinjwa.
Nimesema mimi mfalme
niitwaye Mwenyezi-Mungu wa Majeshi.
16Janga la Moabu limekaribia,
maangamizi yake yanawasili haraka.
17Mwomboleezeni Moabu, enyi jirani zake wote,
na nyote mnaomjua vizuri
semeni: ‘Jinsi gani fimbo ya nguvu ilivyovunjwa,
naam fimbo ile ya fahari!’
18Enyi wenyeji wa Diboni:
Shukeni kutoka mahali penu pa fahari,
mkaketi katika ardhi isiyo na maji.
Maana mwangamizi wa Moabu,
amefika kuwashambulia;
amekwisha haribu ngome zenu.
19Enyi wakazi wa Aroeri,
simameni kando ya njia mtazame!
Mwulizeni anayekimbia na anayetoroka:
‘Kumetokea nini?’
20Moabu imeaibishwa maana imevunjwa;
ombolezeni na kulia.
Tangazeni kando ya mto Arnoni,
kwamba Moabu imeharibiwa kabisa.
21“Hukumu imeifikia miji iliyo nyanda za juu: Holoni, Yasa, Mefaathi, 22Diboni, Nebo, Beth-diblathaimu, 23Kiriathaimu, Beth-gamuli, Beth-meoni, 24Keriothi na Bosra. Naam, hukumu imeifikia miji yote ya Moabu mbali na karibu. 25Nguvu za Moabu zimevunjiliwa mbali na uwezo wake umevunjwa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
26“Mlewesheni Moabu kwa sababu alijikuza dhidi yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Moabu atagaagaa katika matapishi yake na watu watamcheka. 27Kumbuka Moabu ulivyomcheka Israeli. Je, alikamatwa pamoja na wezi, hata ukawa unatikisa kichwa chako kila ulipoongea juu yake?
28“Enyi wenyeji wa Moabu,
tokeni mijini, mkakae mapangoni!
Mwigeni njiwa ajengaye kiota penye genge.
29Tumesikia juu ya kiburi cha Moabu;
Moabu ana majivuno sana.
Tumesikia juu ya kujiona, kiburi na majivuno yake;
tumesikia jinsi anavyojigamba moyoni.
30“Nami Mwenyezi-Mungu nasema:
Najua ufidhuli wake;
Majivuno yake ni ya bure,
na matendo yake si kitu.
31Kwa hiyo ninaomboleza juu ya Moabu,
ninalia kwa ajili ya Wamoabu wote,
naomboleza juu ya watu wa Kir-heresi.
32Nakulilia wewe bustani ya Sibma
kuliko hata watu wa Yazeri.
Matawi yako yametanda
mpaka ngambo ya bahari ya Chumvi
yakafika hata mpaka Yazeri.
Lakini mwangamizi ameyakumba
matunda yako ya kiangazi na zabibu zako.
33Furaha na shangwe zimeondolewa
kutoka nchi ya Moabu yenye rutuba.
Nimeikomesha divai kutoka mashinikizo
hakuna mtu anayekamua zabibu kwa shangwe;
kelele zinazosikika si za shangwe.
34“Kilio cha watu wa Heshboni chasikika huko Eleale mpaka Yahazi; kinaenea kutoka Soari mpaka Horonaimu na hata Eglath-shelishiya. Hata maji ya kijito Nimrimu yamekauka. 35Nami nitamfutilia mbali kila mtu katika Moabu ambaye anatambikia vilimani na kumfukizia ubani mungu wake.
36“Kwa hiyo, moyo wangu unaomboleza juu ya watu wa Moabu na watu wa Kir-heresi, kama mpiga zumari mazishini; maana hata mali yote waliyojipatia imeangamia. 37Kila mtu amenyoa upara na ndevu zake. Wote wamejikatakata mikononi na viunoni wamevaa mavazi ya gunia. 38Juu ya nyumba za Moabu na katika viwanja vyao hakuna kinachosikika ila tu maombolezo. Mimi nimemvunja Moabu kama chombo kisichotakiwa na mtu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. 39Tazama alivyovunjika! Tazama wanavyoomboleza! Ajabu jinsi Moabu alivyorudi nyuma kwa aibu! Moabu amekuwa kichekesho na kioja kwa jirani zake wote.”
40Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Tazama, taifa litaruka kasi kuivamia Moabu,
kama tai aliyekunjua mabawa yake.
41Miji yake itatekwa,
ngome zitachukuliwa.
Siku hiyo mioyo ya wanajeshi wa Moabu,
itaogopa kama mwanamke anayejifungua.
42Wamoabu wataangamizwa, wasiwe tena taifa,
kwa sababu walijikweza dhidi ya Mwenyezi-Mungu.
43Kitisho, mashimo na mtego,
vinawasubiri enyi watu wa Moabu.
Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
44Atakayetoroka kitisho
atatumbukia shimoni;
atakayetoka shimoni
atanaswa mtegoni.
Kwa maana nitaleta mambo hayo juu ya Moabu,
katika mwaka wao wa adhabu.
Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
45Wakimbizi wachovu wanatua Heshboni kutaka usalama,
maana moto umezuka huko mjini;
mwali wa moto toka ikulu ya mfalme Sihoni;
umeteketeza mipaka#48:45 mipaka: Kiebrania: Uso. ya Moabu,
umeunguza milima#48:45 milima: Kiebrania: Utosi. yao hao watukutu.
46Ole wenu watu wa Moabu!
Watu wa Kemoshi sasa mmeangamizwa,
wana wenu wamechukuliwa mateka,
binti zenu wamepelekwa uhamishoni.
47Lakini siku zijazo
nitamstawisha tena Moabu.
Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
Hii ndiyo hukumu juu ya Moabu.”

Currently Selected:

Yeremia 48: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy