YouVersion Logo
Search Icon

Habakuki 2

2
1Mimi nitasimama mahali pa kuchungulia,
na kukaa juu mnarani;
nitakaa macho nione ataniambia nini,
atajibu nini kuhusu lalamiko langu.”
Mungu anamjibu Habakuki
2Kisha, Mwenyezi-Mungu akanijibu hivi:
“Yaandike maono haya;
yaandike wazi juu ya vibao,
anayepitia hapo apate kuyasoma.
3 # Taz Ebr 10:37 Maono haya yanangoja wakati wa kufaa;
ni maono ya ukweli juu ya mwisho.
Kama yaonekana kuchelewa, uyasubiri;
hakika yatafika, wala hayatachelewa.
4 # Taz Roma 1:17; Gal 3:11; Ebr 10:38 Andika:
‘Waangalie wenye kiburi, hao wataangamia;
lakini waadilifu wataishi kwa kumwamini Mungu.’”
Waovu wataangamia
5Zaidi ya hayo, divai hupotosha;
mtu mwenye kiburi hatadumu.
Yuko tayari kuwameza wengine kama Kuzimu;
kama vile kifo, hatosheki na kitu.
Hujikusanyia mataifa yote,
na watu wote kama mali yake.
6Kila mtu atamdhihaki mtu wa namna hiyo
na kumtungia misemo ya dhihaka:
“Ole wako unayejirundikia visivyo vyako,
na kuchukua rehani mali za watu lakini hulipi!
Utaendelea kufanya hivyo hadi lini?
7Siku moja wadeni wako watainuka ghafla,
wale wanaokutetemesha wataamka.
Ndipo utakuwa mateka wao.
8Wewe umeyapora mataifa mengi,
lakini wote wanaosalimika watakupora wewe,
kwa mauaji na dhuluma uliyoitendea dunia,
naam, uliyoifanyia miji na wakazi wake wote.
9“Ole wako unayejitajirisha kwa hasara ya mwingine,
ujengaye nyumba yako juu milimani
ukidhani kuwa salama mbali na madhara.
10Lakini kwa mipango yako umeiaibisha jamaa yako.
Kwa kuyaangamiza mataifa mengi,
umeyaangamiza maisha yako mwenyewe.
11Ndiyo maana hata mawe yatalalamika ukutani,
na boriti za nyumba zitayaunga mkono.
12“Ole wako unayejenga mji kwa mauaji
unayesimika jiji kwa maovu!
13Mwenyezi-Mungu wa majeshi husababisha
juhudi za watu zipotelee motoni,
na mataifa yajishughulishe bure.
14 # Taz Isa 11:9 Utukufu wa Mwenyezi-Mungu utaenea pote duniani,
kama vile maji yaeneavyo baharini.
15Ole wako unayewalewesha jirani zako,
na kutia sumu katika divai yao
ili upate kuwaona wamekaa uchi.
16Utajaa aibu badala ya heshima.
Utakunywa wewe mwenyewe na kupepesuka!
Mwenyezi-Mungu mwenyewe atakulevya,
na aibu itaifunika heshima yako!
17Maovu uliyoitenda Lebanoni yatakuvamia wewe;
uliwaua wanyama, wanyama nao watakutisha.
Yote hayo yatakupata wewe,
kwa mauaji na dhuluma uliyoitendea dunia,
naam, uliyoifanyia miji na wakazi wake wote.
18“Chafaa nini kinyago alichotengeneza mtu?
Sanamu ni madini yaliyoyeyushwa,
ni kitu cha kueneza udanganyifu!
Mtengeneza sanamu hutumaini alichotengeneza mwenyewe,
kinyago ambacho hakiwezi hata kusema!
19Ole wake mtu aliambiaye gogo: ‘Amka!’
Au jiwe bubu ‘Inuka!’
Je, sanamu yaweza kumfundisha mtu?
Tazama imepakwa dhahabu na fedha,
lakini haina uhai wowote.”
20Lakini Mwenyezi-Mungu yumo katika hekalu lake takatifu;
dunia yote na ikae kimya mbele yake.

Currently Selected:

Habakuki 2: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy