YouVersion Logo
Search Icon

Waefeso UTANGULIZI

UTANGULIZI
Mji wa Efeso ulikuwa mji mkuu wa mojawapo ya mikoa ya utawala wa Waroma katika Mashariki ya Kati (au Asia Ndogo). Ulikuwa kitovu cha biashara na tamaduni kadhaa. Huko kulikuwa pia na Wayahudi wengi. Paulo aliutembelea mji huo kwa muda mfupi wakati wa ziara yake ya pili ya kitume (Mate 18:19-21) na katika ziara yake ya tatu alikaa huko miaka mitatu (tazama Mate 19:1-20:1,31).
Barua ya Paulo kwa jumuiya ya Wakristo kule Efeso iliandikwa kutoka kifungoni (tazama 3:1), labda kule Roma, kati ya mwaka wa 60 na 61 B.K. Barua nyingine zilizoandikwa na Paulo akiwa kifungoni ni pamoja na barua kwa Wakolosai, kwa Wafilipi na kwa Filemoni (taz pia Kol 4:3,10,18; File 9-10,13,23). Walengwa wa barua hii, tofauti na barua nyingine zijulikanazo kama za Paulo, hawatajwi moja kwa moja isipokuwa tu mwanzoni mwa barua hii katika 1:1. Hata hapa, hati nyingine za kale hazina neno Efeso. Vilevile, salamu kwa watu binafsi hazipo na watu binafsi hawatajwi isipokuwa tu Tukiko ambaye anatajwa katika 6:21. Kutokana na hayo, baadhi ya wafafanuzi wa Maandiko Matakatifu wanafikiri kwamba barua hii haikuwa tu kwa Waefeso ila pia kwa jumuiya mbalimbali.
Wazo kuu ambalo barua hii na muundo wake inalizungukia ni lile la umoja wa kanisa na viumbe vyote chini ya utawala wa Kristo aliyefufuka (1:20–2:20), na chini yake Kristo, vitakusanywa viumbe vyote: Kila kitu mbinguni na duniani (1:10). Huo ni mpango wa Mungu ambao atautekeleza kwa njia ya kanisa (3:10-11).
Barua yenyewe imeundwa katika sehemu mbili kuu:
Ya kwanza (sura 1:3–3:21) kwa jumla ina mafundisho. Hii imetanguliwa na 1:1-2 ambayo ni salamu za mwanzo. Sehemu hii inaanza na shukrani kwa Mungu (1:3-14) ambaye alituchagua kwa njia ya Kristo kabla ya kuumbwa ulimwengu na kututeua tuwe watoto wake kwa kuungana na Kristo (aya ya 4). Kisha inafuata sala ya kushukuru kwa ajili ya upendo na imani ya walengwa wake (1:15-23). Sura ya pili inawakumbusha walengwa wake kwamba wakati mmoja walikuwa wamekufa kwa sababu ya makosa na dhambi lakini sasa wameokolewa kwa neema ya Mungu na kuwa raia pamoja na watu wa Mungu. Roho Mtakatifu aliwafunulia manabii na mitume wa Kristo fumbo la kuokolewa kwa wasio Wayahudi (3:5).
Katika sehemu ya pili (sura 4:1–6:20) Paulo anawahimiza wahifadhi “umoja uletwao na Roho kwa kuzingatia amani” (4:3-6). Mkristo lazima ajirekebishe upya rohoni na katika fikra na kuvaa hali mpya ya utu ulioumbwa kwa mfano wa Mungu (4:22-24). Mioyo ya waumini sharti iongozwe na kanuni za watoto wa mwanga: Wema, uadilifu na ukweli (5:9). Ni katika sura hii ya tano (5:21-33) ambapo Paulo anathibitisha kuweko kufanana kwa pekee kati ya umoja wa ndani wa Kristo na kanisa lake na umoja wa ndoa. Mfano mwingine ni ule wa jumba ambalo Yesu Kristo ndiye jiwe la msingi.
Sehemu hii ya pili inamalizia kwa maneno ya kuwahimiza waumini waupige vita uovu wakitumia silaha za kiroho kukabili vita vya kiroho.

Currently Selected:

Waefeso UTANGULIZI: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy