YouVersion Logo
Search Icon

Mhubiri 7

7
Mawaidha kuhusu maisha
1Sifa njema ni bora kuliko marashi ya thamani.
Siku ya kufa ni bora kuliko siku ya kuzaliwa.
2Afadhali kwenda kwenye matanga,
kuliko kwenda kwenye karamu,
kwa sababu walio hai yawapasa kukumbuka kwamba kifo chatungojea sisi sote.
3Huzuni ni afadhali kuliko kicheko
maana, huzuni ya uso ni faida ya moyo.
4Moyo wa mwenye hekima huthamini matanga,
lakini moyo wa mpumbavu hupenda raha.
5Afadhali kusikia maonyo ya wenye hekima
kuliko kusikiliza nyimbo za wapumbavu.
6Maana, kicheko cha mpumbavu
ni kama mlio wa miiba motoni.
Hayo nayo ni bure kabisa.
7Mwenye hekima akimdhulumu mtu;
hujifanya mwenyewe kuwa mpumbavu
kupokea rushwa hupotosha akili.
8Mwisho wa jambo ni afadhali kuliko mwanzo wake;
mvumilivu rohoni ni bora kuliko mwenye majivuno.
9Usiwe mwepesi wa hasira,
maana, hasira hukaa ndani ya wapumbavu.
10Usiulize, “Kwa nini nyakati za kale zilikuwa bora kuliko za sasa?”
Huulizi hivyo kwa kutumia hekima.
11Hekima ni ya thamani kubwa kama urithi;
ni muhimu kwa wale wote walio hai.
12Kulindwa na hekima ni kama kulindwa na fedha.
Faida ya maarifa ni kwamba hekima hulinda maisha ya mtu aliye nayo.
13Tafakarini vema kazi yake Mungu;
ni nani awezaye kunyosha alichopinda Mungu?
14Katika siku za fanaka uwe na furaha; katika siku za maafa utafakari jambo hili: Fanaka, pia maafa, Mungu amefanya hiyo ya kwanza iambatane na ya pili ili binadamu asiweze kujua yatakayotukia baada yake.
15Katika maisha yangu duni, nimeona kila kitu; mtu mwadilifu hufa ingawa ni mwadilifu, ambapo mtu mwovu huendelea kuishi maisha marefu ingawa ni mwovu. 16Basi, usiwe mwadilifu sana, wala usiwe mwenye hekima mno! Ya nini kujiangamiza wewe mwenyewe? 17Lakini pia, usiwe mwovu sana wala usiwe mpumbavu! Ya nini kufa kabla ya wakati wako? 18Inakupasa ushike la kwanza na la pili pia; maana anayemtii Mungu atajengwa kwayo.
19Hekima humfanya mwenye busara kuwa na nguvu zaidi kuliko watawala kumi mjini.
20Hakika, hakuna mtu mwadilifu duniani atendaye mema daima bila kutenda dhambi.
21Usitie maanani maneno yote wasemayo wanadamu, usije ukamsikia mtumishi wako akikutukana. 22Wewe mwenyewe wajua moyoni kwamba umeapiza wengine mara nyingi.
Kuomba hekima
23Nimeyapima hayo yote kwa hekima; nikajisemea: “Nataka kuwa mwenye hekima!” Lakini hekima iko mbali sana nami. 24Jinsi gani binadamu ataweza kugundua maana ya maisha; jambo hilo ni zito na gumu mno kwetu! 25Hata hivyo, nilipania kujua na kuchunguza na kutafuta hekima na maana ya mambo yaliyoko, na pia kujua uovu ni upuuzi, na upumbavu ni wazimu.
26Jambo moja nililogundua lililo baya zaidi kuliko kifo, ni mwanamke ambaye moyo wake ni mtego na wavu, na mikono yake ni kama minyororo. Lakini anayempendeza Mungu humkwepa mwanamke huyo, lakini mwenye dhambi hunaswa naye. 27Haya, nakuambia mimi Mhubiri, ndio niliyogundua nilipofanya uchunguzi wangu kidogokidogo. 28Nilipania kugundua mambo hayo tena na tena, lakini sikufaulu. Kati ya wanaume elfu moja, nilifaulu kumwona mwanamume mmoja, anayestahili heshima, lakini kati ya wanawake wote kama hao sikumwona hata mmoja anayestahili heshima. 29Tazama, nimegundua jambo hili moja: Kwamba Mungu aliwaumba wanadamu wanyofu, lakini wao wenyewe wamejitafutia matatizo.

Currently Selected:

Mhubiri 7: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy