YouVersion Logo
Search Icon

1 Samueli UTANGULIZI

UTANGULIZI
Kitabu cha kwanza cha Samueli ni sehemu ya kwanza ya kitabu kirefu (sehemu ya pili ikiwa ni kitabu cha pili cha Samueli) ambacho kiligawanywa katika sehemu mbili kwa vile hakikuweza kuenea katika msokoto mmoja wa hati ya mkono. Zaidi ya hayo, Vitabu vya Samueli na vile vya Wafalme (viwili) vinafanana; hata ile tafsiri ya Septuajinta (LXX) inaviita kwa jina moja: “Wafalme 1-4”. Wengine wanataka kuvitazama vitabu vyote tangu Yoshua mpaka Wafalme kama vyenye uhusiano mahsusi kwa vile vinasema juu ya historia ya Waisraeli tangu kuiteka nchi ya Kanaani hadi walipochukuliwa uhamishoni Babuloni.
Nabii Samueli ambaye jina lake limechukuliwa na kitabu hiki na kile cha pili kinachofuata, alikuwa mmoja wa “Waamuzi” wa mwisho ambao Mungu aliwapatia watu wake nyakati za misukosuko na hatari. Yeye alitoa huduma zake za mseto: Kwa upande mmoja kusema kweli yeye ni mtu wa dini, msemaji wa Mungu yaani nabii; lakini pia kwa upande mwingine alihudumu kama mwanasiasa (sura 1–7.)
Huduma za Samueli zilikuwa muhimu sana kwani zilifanyika nyakati za mageuzi ya hali ya maisha ya jumuiya nchini Palestina, yaani kutoka uongozi wa wale “Waamuzi” na kufikia uongozi wa kifalme. Kitabu hiki basi, kina hoja moja muhimu: Kuanzishwa kwa utawala wa kifalme nchini Israeli. Samueli mwenyewe anajulikana kama mtu maarufu aliyewaonya Waisraeli juu ya athari za utawala wa kifalme. Mfalme wa kwanza wa Israeli, Shauli, alikuwa balaa; mfalme wa pili, Daudi, alikuwa mfano mzuri wa mtu ambaye Mungu alimtaka.
Kitabu hiki cha kwanza cha Samueli kina sehemu tatu:
Sura 1:1–7:17: Zahusu hasa Samueli mwenyewe (mtu wa dini na mwanasiasa).
Sura 8:1–15:35: Samueli na Shauli. (Ingawa Samueli anasita na kuwa na mashaka juu ya maombi ya watu ya kutaka kuwa na mfalme, kufuatia amri ya Mungu, anakubali kuwateulia mfalme – Shauli ambaye, muda si muda, anaonekana hana uaminifu kwa Mungu).
Sura 16:1–31:13: Shauli na Daudi. (Kwa sababu ya hali ya Shauli, Mungu anamchagua kijana Daudi awe mfalme badala yake. Shughuli hiyo ya kuteua na kutawaza anaifanya Samueli. Daudi anazidi kufanikiwa – Shauli anazidi kupata balaa.)
Samueli alihudumu kama nabii, kuhani na mwamuzi katika mwaka 11 K.K. na kuwasaidia Waisraeli kuleta mabadiliko kutoka uongozi wa waamuzi wa kivita na kuingia katika uongozi wa kifalme. Ndiye aliyemtawaza mfalme wa kwanza wa Israeli, “Shauli” (10:1) na mfalme wa pili baadaye, yaani Daudi (16:1-13). Kifo chake kimeandikwa katika aya ya 1 sura ya 25.
Kitabu hiki chatukumbusha miongoni mwa mengine kwamba Mwenyezi-Mungu peke yake ndiye mfalme wa watu wake. Miongoni mwa watu wake madaraka ya kweli hayawezi kutekelezwa vizuri isipokuwa tu na mtu yule ambaye anakubali kukaa chini ya madaraka ya Mungu na kumtegemea kikamilifu.

Currently Selected:

1 Samueli UTANGULIZI: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy