1 Petro UTANGULIZI
UTANGULIZI
Barua hii ya kwanza ya Petro imeandikiwa Wakristo waliotawanyika katika mikoa mitano ya Mashariki ya Kati, au sehemu ijulikanayo kama Asia Ndogo, na ambayo kwa sasa ni nchi ya Uturuki. Jumuiya hizo za Wakristo zinazohusika zilikuwa zimeanzishwa na mtume Paulo au na wenzake, kwa mfano Timotheo, n.k. Mwandishi anawaandikia labda kutoka Roma (“Babuloni” Taz 5:13). Barua hii aliiandika labda mnamo mwaka 62 B.K. akisaidiwa na mwandishi wake Silwano.
Hali ya wakati huo inavyoonekana na kutajwa katika barua hii yaonesha kwamba Wakristo hao walikuwa wameonewa na kushtakiwa kuhusu mambo kadha wa kadha na jirani zao wasiomjua Mungu, wakatishwa na udhalimu. Kwa hiyo mtume Petro anaandika kuwatia moyo akiwakumbusha msimamo wake Yesu Kristo ambaye sasa wanashiriki mateso yake. Wakristo hao wanatakiwa wawe na matumaini thabiti sio tu wakiwa wanangojea kurudi kwake Kristo, bali wakiwa wanaishi kulingana na mfano uleule wa nafsi yake Kristo.
Baada ya salamu fupi (1:1-2), mwandishi anaingiza mara wazo la jumla kuhusu mpango wa ukombozi uliotayarishwa na Mungu kwa ajili ya wale wanaomwamini Yesu Kristo, imani ambayo ni ya thamani kuliko dhahabu (1:7) na ambayo lengo lake ni wokovu wa roho (1:9). Kisha mwandishi anatoa mfululizo wa mashauri kwa waumini (1:13–2:10). Hao waumini ni “ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe” ambao aliwateua kutangaza matendo makuu ya Mungu (2:9).
Kwa hiyo, katika sura 1:3-12, Petro anawakumbusha Wakristo juu ya jinsi Mungu alivyowaokoa na kuwapa matumaini thabiti kwa tukio la kifo na ufufuo wake Kristo.
Katika 1:13–2:10, anawahimiza wawe waangalifu, wawe macho na kuishi maisha matakatifu katika kuungana na Kristo.
Katika sura ya 2:11–4:49 anawaambia kwamba wanapaswa kuonesha uaminifu wao kwa ujumbe wake Kristo kwa tabia yao na kwa uhusiano wao na watu maskini. Anawapa mashauri yahusuyo maisha ya kila siku: Mwongozo kuhusu wenye mamlaka na serikali, juu ya heshima kati ya mume na mkewe, juu ya watumwa na mabwana zao, juu ya maisha ya jamii na namna ya kuhusiana na watu wasiomjua Mungu.
Katika sura ya 5, mwandishi anaendelea kutoa mwongozo wake na mawaidha hasa kwa wenye madaraka katika jumuiya (au wale waitwao “wazee”), mawaidha kuhusu vijana na waumini wote. Anawahimiza wote wakae imara katika mateso wakitazamia kwa hamu kutekelezwa kwa ahadi zile walizopewa na Mungu. Kuonesha kwa vitendo maisha yao ya imani kuna shabaha pia ya kuwafanya watu wasiomjua Mungu wajue matendo makuu ya Mungu (2:9) na hivyo kuwaongoza watambue matendo hayo mema na kumsifu Mungu siku atakapokuja (2:12).
Currently Selected:
1 Petro UTANGULIZI: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.