YouVersion Logo
Search Icon

Hekima ya Solomoni 1

1
Ukweli wa Mungu waleta uhai
1Pendeni haki, enyi watawala wa dunia!
Jiaminisheni kikamilifu kwa Bwana.
na kumtafuta kwa moyo mnyofu.
2Maana yeye huwajalia wanaojiaminisha kwake wampate;
hujionesha kwa wale wanaomtegemea.
3Fikira potovu huwatenganisha watu mbali na Mungu;
watu wakiijaribu nguvu yake, yeye hudhihirisha upumbavu wao.
4Hekima haiingii kwa mtu mdanganyifu,
wala haikai kwa mtu aliye mtumwa wa dhambi.
5Mtu aliye mtakatifu amejifunza kuepukana na udanganyifu.
Mtu huyo huepa kushiriki fikira za kipumbavu;
huwa na wasiwasi endapo haki zinavunjwa ovyo.
6Hekima ana moyo wa huruma;
lakini hatamsamehe yeyote anayemkufuru Mungu.
Mungu ajua yote: Hisia zetu na fikira zetu;
husikia kila neno tusemalo.
7Roho ya Bwana inaujaza ulimwengu;
hiyo inayotegemeza kila kitu pamoja.
hujua kila kitu asemacho binadamu.
8Kila mtu asemaye mabaya dhidi yake hawezi kufichika,
na hukumu inapotolewa hataweza kuiepa adhabu.
9Mawazo ya waovu yatachunguzwa;
Bwana atapata ripoti ya maneno yao mabaya
na kuwaadhibu kwa sababu ya uovu wao.
10Bwana ametega sikio lake; anasikia kila kitu.
Hakuna mnongono wowote ule ambao utasitirika.
11Kwa hiyo jihadharini na manunguniko ya bure,
epukeni kusema uchongezi.
Mungu husikia hata nunguniko la siri kabisa.
Asemaye uongo huiangamiza roho yake mwenyewe.
12Kwa hiyo usijiletee kifo kwa dhambi zako,
wala kukaribisha maangamizi kwa matendo yako maovu.
13Kifo hakikuanzishwa na Mungu;
Mungu hafurahii kufa kwa mtu yeyote yule.
14Mungu aliumba viumbe vyote vipate kuwapo,
akavipa nguvu zifaazo za kuendeleza maisha.
Ndani ya viumbe hamna sumu ya kuua;
Kuzimu haina mamlaka hapa duniani.
15Mwadilifu ataishi milele!
Fikira potovu huleta kifo
16Lakini wasiomcha Mungu hukaribisha kifo kwa matendo na maneno yao,
hufanya urafiki na kifo
na kufanya mkataba pamoja nacho;
sasa wanastahili kuwa mateka wake!

Currently Selected:

Hekima ya Solomoni 1: BHND

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy