YouVersion Logo
Search Icon

Mathayo UTANGULIZI

UTANGULIZI
Kutokana na muundo wa Habari hii Njema, mwandishi Mathayo alitaka kusisitiza jambo moja muhimu: Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu na, kwa nafsi yake, Mungu amewajia wanadamu pamoja na mwongozo wake na kukaa nao. Kwa kuungana na Yesu Kristo ambaye ndiye Emanueli, yaani “Mungu pamoja nasi,” Mungu anaunda jumuiya mpya ya watu wake – Kanisa. Kwa maneno mengine, yeyote anayeusikia ujumbe huu na kuwa mwanafunzi wa Yesu aliye Mwana wa Mungu, huyo pia anakuwa mwana wa Mungu na kupewa jukumu lilelile alilopewa Yesu Kristo: Kuwatangazia watu wamgundue Mungu katika nafsi yake Yesu Kristo na kuwa wanafunzi wake.
Jambo la Mungu kuwa pamoja na watu linatangazwa waziwazi mwanzoni mwa Injili hii: “Naye ataitwa Emanueli,” yaani “Mungu pamoja nasi” (1:23); na mwishoni mwa Injili hii, pale Yesu Kristo anapoondoka kurudi kwa Mungu, anawaambia wanafunzi wake: “Nami nipo pamoja nanyi siku zote; naam, mpaka mwisho wa nyakati” (28:20).
Mathayo aliiandika Injili hii akiwa anawafikiria wasomaji wake ambao walikuwa Wayahudi walioikubali hii Habari Njema juu ya Yesu Kristo na kumwamini. Ndiyo maana kila inapowezekana, Mathayo anawarudisha wasomaji wake mpaka Agano la Kale katika sehemu zile ambazo sasa zaonekana zimekamilika katika ujio wake Yesu Kristo. Mojawapo ya sehemu hizo maalumu ni ile inayomhusu Yesu kuwa Mwana wa Mungu. Yafaa kukumbuka kwamba nao watu wa Israeli waliitwa wana wa Mungu (Hos 11:1), msemo ambao sasa unatumiwa kuhusu mwito wa Yesu Kristo: “Nilimwita Mwanangu kutoka Misri” (2:15). Aghalabu msemo huo waonekana kuwa muhimu kabisa katika Injili hii. Awali kabisa, kabla ya Yesu kuanza kazi yake rasmi, Mungu mwenyewe anatamka rasmi juu yake: “Huyu ni Mwanangu mpendwa nimependezwa naye” (3:17). Na, mara tu baada ya tamko hilo, Shetani naye anauchukua msemo huo kuwa kisababu cha kumjaribu Yesu: “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu…” (4:3). Tena pale katika kilele cha kazi yake, Yesu akiwa anakufa msalabani, nao wapita njia pale wanarudia hayohayo, “…sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi, shuka msalabani!” (27:40).
Baada ya kuwafundisha wanafunzi wake kiasi cha kutosha, nao pia wanamtambua kuwa “Mwana wa Mungu” (14:33; 16:16). Katika mfano ule wa watumishi shambani mwa bwana wao, mfano ambao Yesu aliutoa mbele ya maofisa wa Kiyahudi, Yesu anagusia jambo la yeye kuwa Mwana wa Mungu na kwa kusema hivyo hao maofisa wakapania kumuua. Katika mahakama mbele ya Pilato, hiyo ilikuwa sababu maalumu ya kumuua. Walakini hata wakati wa kifo chake, askari wa Kiroma nao wanatamka wazi: “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu” (27:54).
Ndivyo basi ilivyo katika Injili hii ya Mathayo: Yesu ni Mwana wa Mungu; kwa nafsi yake Yesu Mungu amekuja kukaa pamoja na watu wake. Wanaopata kuwa wanafunzi wa Yesu nao pia wanakuwa wana wa Mungu, wanaweza kumwita Mungu Baba yao kama Yesu naye anavyomwita Baba yake; wanapewa jukumu lilelile la Yesu: Kuwafanya watu wawe wanafunzi wa Yesu na hivyo kuunda jumuiya mpya, jumuiya ambayo inawahusu watu wote. Jumuiya hiyo mpya inakuwa kanisa la Kristo (16:18; 18:17).

Currently Selected:

Mathayo UTANGULIZI: BHND

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in