YouVersion Logo
Search Icon

2 Wamakabayo 15

15
Mpango wa kikatili wa Nikanori
1Nikanori aliposikia kwamba Yuda na watu wake walikuwa sehemu za Samaria, alifanya mpango kuwashambulia siku ya Sabato, wakati ambapo walikuwa wamepumzika. 2Wayahudi waliokuwa wameshurutishwa kumfuata walimwomba asifanye ukatili na unyama kama huo, bali aiheshimu siku hiyo ambayo Mungu aonaye yote alikuwa ameiheshimu na kuifanya takatifu kuliko siku nyingine zote. 3Ndipo Nikanori, mlaaniwa mkuu, alipouliza kama eti kulikuwa na mfalme mbinguni aliyekuwa amewaamuru wao kuiheshimu Sabato. 4Wayahudi wakajibu: “Ndiyo, yuko; Bwana aishiye, atawalaye mbinguni, alituamuru tuiheshimu Sabato.”
5Lakini Nikanori akajibu: “Mimi ndiye mtawala duniani, na ninawaamuru kushika silaha zenu na kufanya anachoamuru mfalme.”
Hata hivyo, Nikanori hakufaulu kutekeleza mpango wake wa kikatili.
Yuda aandaa askari wake kwa mapambano
6Katika majivuno yake, Nikanori alikuwa amejigamba eti angejenga mnara wa ukumbusho wa ushindi wake dhidi ya Yuda. 7Lakini Yuda alikuwa na imani thabiti kwamba Bwana angemsaidia. 8Hivi akawahimiza watu wake wasiwaogope maadui. Aliwatia moyo kwa kuwataka wakumbuke jinsi Mungu Mwenye Nguvu alivyokuwa amewasaidia siku za nyuma, na akawathibitishia kwamba Mungu angewasaidia pia safari hii. 9Aliwatia moyo kwa maneno ya sheria na mafundisho ya manabii na kwa kuwakumbusha mapambano mbalimbali waliyokuwa wameshinda, akawafanya wawe na hamu zaidi ya kupiga vita. 10Watu wake walipokuwa tayari kwa mapigano, aliwapa maagizo yake, akiwaonesha jinsi watu wa mataifa mengine walivyokuwa hawaaminiki, kwa sababu hawakushika mikataba yao. 11Aliwahimiza wawe hodari, si kwa kutegemea ngao na mikuki, bali kwa maneno ya ujasiri ya kutia moyo. Pia aliwachangamsha wote kwa kuwasimulia ndoto - aina ya maono aliyokuwa amepata, ambayo ilistahili kusadikiwa.
12Aliwaeleza kwamba alikuwa amemwona katika ndoto Onia yule aliyekuwa zamani kuhani mkuu, mtu mwema na wa ajabu, mnyenyekevu na mpole, mtu aliyekuwa msemaji maarufu na ambaye alikuwa amefundishwa tangu utoto juu ya mambo mema kabisa, amenyosha mikono kuiombea jumuiya yote ya Wayahudi. 13Kisha, Yuda aliona mtu mwenye nywele nyeupe na wa kupendeza. 14Onia akasema: “Huyu, Yeremia, ni nabii wa Mungu, nabii ambaye anawapenda Wayahudi wenzake, na hutoa sala nyingi kwa ajili yetu na Yerusalemu, mji mtakatifu.”
15Hapo Yeremia alinyosha mkono wake wa kulia na kumpa Yuda upanga wa dhahabu, akisema: 16“Upanga huu wa dhahabu ni zawadi kutoka kwa Mungu. Pokea, ukawaangamizie maadui zako.”
17Maneno mazuri aliyosema Yuda yalimtia moyo na ushujaa kila mtu, na wavulana walikuwa wametiwa hamu ya kupiga vita kama watu wazima. Mji wao, dini yao, na hekalu lao vilikuwa hatarini. Hivyo, Wayahudi wakaamua wasipoteze muda zaidi, ila wamshambulie adui na kuchunguza uwezekano wa kufaulu kwa mapigano ya ana kwa ana. 18Hofu yao haikuwa juu ya wake na watoto wao wenyewe na jamaa, ila hasa juu ya hekalu lao takatifu. 19Na wale waliopaswa kubaki Yerusalemu walipata wasiwasi juu ya mapigano yaliyokuwa yanaendelea nje kwenye uwanja wa mapambano.
Kushindwa na kuuawa kwa Nikanori
20Kila mmoja alikuwa anangoja kuona nani angeshinda vita hivyo. Askari wa maadui walikuwa wanasonga mbele, wakiandamana na wapandafarasi kulia na kushoto kwao, na tembo wao wamewaweka katika sehemu muhimu. 21Basi, Yuda Makabayo akaangalia hilo jeshi kubwa la maadui, silaha zao za ainaaina, na tembo wao wakali. Halafu akainua mikono yake kuelekea mbinguni, akamwomba Bwana ambaye hutenda maajabu, maana alijua kwamba Bwana huwapa ushindi wale wanaostahili, si wale ambao wana jeshi lenye nguvu. 22Basi, akamwomba Mungu hivi: “Bwana, Hezekia alipokuwa mfalme wa Uyahudi, ulimtuma malaika wako, akawaua watu 185,000 wa jeshi la mfalme Senakeribu. 23Sasa, kwa mara nyingine, ewe Bwana wa mbingu, umtume malaika wako mwema kuwatikisa na kuwatetemesha kwa hofu maadui zetu. 24Kwa uwezo wako mkuu, uwaangamize watu hawa ambao wamekukufuru wewe, na ambao wamekuja kulishambulia taifa lako teule.” Kwa maneno hayo, Yuda alimaliza sala yake.
25Nikanori na watu wake walisonga mbele kwa muziki wa tarumbeta na nyimbo za vita, 26lakini Yuda na watu wake walijitia vitani huku wanamwomba Mungu awasaidie. 27Kwa mikono yao walipiga vita; kwa mioyo yao walimwomba Mungu; hivi Wayahudi wakawaua maadui zaidi ya 35,000. Shukrani yao haikuwa na kifani kwa msaada huo waliokuwa wamepata kutoka kwa Mungu. 28Baada ya vita, walipokuwa wanarudi nyumbani huku wanafurahia ushindi wao, wakamwona Nikanori katika uwanja wa mapambano, amekufa, akiwa amevaa silaha zake zote. 29Ndipo wakapaaza sauti wakishangilia na kumsifu Bwana kwa lugha yao.
30Yuda Makabayo, ambaye daima alikuwa amepiga vita kwa nguvu zake zote na kwa moyo wake wote kwa ajili ya Wayahudi wenzake, bila kupoteza kamwe wema wake wa ujanani, akawaamuru watu wake kukata kichwa cha Nikanori na mkono wake wa kulia na kupeleka Yerusalemu. 31Walipowasili mjini Yerusalemu, Yuda aliwakusanya pamoja watu wote, akawaweka makuhani mbele ya madhabahu, na kuagiza waletwe watu waliokuwa ngomeni. 32Akawaonesha kichwa cha yule mlaaniwa, Nikanori na mkono ambao yule mwovu alikuwa ameunyosha kwa ufidhuli dhidi ya hekalu takatifu la Mungu Mwenye Nguvu. 33Kisha akaukata ulimi wa yule mkufuru, akiahidi atawatupia ndege wale, na mabaki ya kichwa kuyaning'iniza mkabala na hekalu, yawe ushindi wa mapato ya upumbavu wa Nikanori. 34Kila mmoja aliinua macho mbinguni, akamsifu Bwana aliyeonesha uwezo wake na kuzuia hekalu lake lisitiwe najisi. 35Yuda akakining'iniza kichwa cha Nikanori katika ukuta wa ngome, kiwe ushahidi waziwazi kwa kila mmoja kuhusu msaada wa Bwana. 36Kwa kauli moja iliamuliwa kwamba siku hiyo isisahauliwe kamwe, bali iadhimishwe kila mwaka siku inayotangulia siku ya Mordekai,#15:36 siku ya Mordekai: Sikukuu ya Purimu (taz Esta 9:17-22). yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili uitwao Adari kwa Kiaramu.
Hatima
37Hivyo ndivyo mambo yalivyomwendea Nikanori. Toka siku hiyo mji wa Yerusalemu umebaki mikononi mwa taifa la Wayahudi; nami namalizia masimulizi yangu hapa. 38Kama yameandikwa kwa ufasaha na mpangilio, ninafurahi; lakini kama yameandikwa ovyoovyo na bila kivutio, hivyo ndivyo nilivyoweza. 39Tunajua kwamba haileti afya kunywa divai au maji peke yake, ambapo divai iliyochanganywa na maji hufanya kinywaji chenye ladha ya kupendeza. Hivi, pia, masimulizi mazuri yakiandikwa kwa ustadi huwafurahisha na kuwaburudisha wasomaji. Na hapa ndio mwisho.

Currently Selected:

2 Wamakabayo 15: BHND

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy