YouVersion Logo
Search Icon

Luka 6

6
Suala juu ya siku ya Sabato
(Mat 12:1-8; Marko 2:23-28)
1Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano, na wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya ngano, wakaondoa punje zake kwa mikono, wakala. 2Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato?” 3Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma jinsi alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? 4Yeye aliingia katika nyumba ya Mungu, akachukua ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu, akala na kuwapa wenzake. Haikuruhusiwa mtu kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani.” 5Hivyo akawaambia, “Mwana wa Mtu ana uwezo juu ya Sabato.”
Mtu mwenye mkono uliopooza
(Mat 12:9-14; Marko 3:1-6)
6Siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia katika sunagogi, akafundisha. Mle ndani kulikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kulia ulikuwa umepooza. 7Waalimu wa sheria na Mafarisayo walitaka kupata kisa cha kumshtaki Yesu na hivyo wakawa wanangojea waone kama angemponya mtu siku ya Sabato. 8Lakini Yesu alijua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka, simama katikati.” Yule mtu akaenda kusimama katikati. 9Kisha Yesu akawaambia, “Nawaulizeni, je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuyaangamiza?” 10Baada ya kuwatazama wote waliokuwa pale, akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Naye akafanya hivyo, na mkono wake ukawa mzima tena. 11Lakini wao wakakasirika sana, wakajadiliana jinsi ya kumtendea Yesu maovu.
Yesu anateua mitume kumi na wawili
(Mat 10:1-4; Marko 3:13-19)
12Siku moja Yesu alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha akisali. 13Kesho yake aliwaita wanafunzi wake, na miongoni mwao akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume: 14Simoni (ambaye Yesu alimpa jina Petro) na Andrea ndugu yake, Yakobo na Yohane, Filipo na Bartholomayo, 15Mathayo na Thoma, Yakobo wa Alfayo na Simoni (aliyeitwa Zelote), 16Yuda wa Yakobo na Yuda Iskarioti ambaye baadaye alikuwa msaliti.
Yesu anafundisha na kuwaponya watu
(Mat 4:23-25)
17Baada ya kushuka mlimani pamoja nao, Yesu alisimama mahali palipokuwa tambarare. Hapo kulikuwa na kundi kubwa la wanafunzi wake na umati wa watu waliotoka pande zote za Yudea na Yerusalemu na pwani ya Tiro na Sidoni. Wote walifika kumsikiliza Yesu na kuponywa magonjwa yao. 18Aliwaponya pia wote waliokuwa wanasumbuliwa na pepo wachafu. 19Watu wote walitaka kumgusa, kwa maana nguvu ilikuwa inatoka ndani yake na kuwaponya wote.
Heri na ole
(Mat 5:1-12)
20Yesu akawageukia wanafunzi wake, akasema:
“Heri nyinyi mlio maskini,
maana ufalme wa Mungu ni wenu.
21Heri nyinyi mnaosikia njaa sasa,
maana baadaye mtashiba.
Heri nyinyi mnaolia sasa,
maana baadaye mtacheka kwa furaha.
22“Heri yenu nyinyi iwapo watu watawachukia, watawatenga, watawatukana na kuwaharibieni jina kwa ajili ya Mwana wa Mtu. 23Wakati hayo yatakapotokea, furahini na kucheza, maana hakika tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana wazee wao waliwatendea manabii vivyo hivyo.
24Lakini ole wenu nyinyi mlio matajiri,
maana mmekwisha pata faraja yenu.
25Ole wenu nyinyi mnaoshiba sasa,
maana baadaye mtasikia njaa.
Ole wenu nyinyi mnaocheka kwa furaha sasa,
maana baadaye mtaomboleza na kulia.
26Ole wenu nyinyi iwapo watu wote wanawasifu,
maana wazee wao waliwafanyia manabii wa uongo vivyo hivyo.
Kuwapenda maadui
(Mat 5:38-48; 7:12a)
27“Lakini nawaambieni nyinyi mnaonisikiliza, wapendeni maadui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni. 28Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. 29Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie pia la pili. Mtu akikunyanganya koti lako mwachie pia shati lako. 30Yeyote anayekuomba mpe, na mtu akikunyanganya mali yako usimtake akurudishie. 31Jinsi mnavyotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo.
32“Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda nyinyi, je, mtapata tuzo gani? Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao. 33Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya hayo. 34Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni, je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili warudishiwe kima kilekile. 35Ila nyinyi wapendeni maadui zenu na kuwatendea mema; kopesheni bila kutazamia kurudishiwa, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani na walio wabaya. 36Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma.
Juu ya kuwahukumu wengine
(Mat 7:1-5)
37“Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa; msiwalaumu wengine, nanyi hamtalaumiwa; wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa. 38Wapeni wengine wanavyohitaji, nanyi mtapewa. Naam, mtapokea mikononi mwenu kipimo kilichojaa, kikashindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika. Kwa maana kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho atakachotumia Mungu kwenu.”
39Akawaambia mfano huu: “Je, kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake? La! Wote wataanguka shimoni. 40Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, lakini kila mwanafunzi akisha hitimu huwa kama mwalimu wake. 41Kwa nini wakiona kibanzi jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako? 42Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako,’ na huku huioni boriti iliyomo katika jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe! Toa kwanza boriti iliyomko jichoni mwako, na hapo ndipo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako.
Mtu hujulikana kwa matunda yake
(Mat 7:16-20; 12:33-35)
43“Mti mzuri hauzai matunda mabaya, wala mti mbaya hauzai matunda mazuri. 44Watu huutambua mti kutokana na matunda yake. Ni wazi kwamba watu hawachumi tini katika michongoma, wala hawachumi zabibu katika mbigili. 45Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina bora iliyomo moyoni mwake; na mtu mbaya hutoa yaliyo mabaya kutoka katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake, kwa maana mtu huongea kutokana na yale yaliyojaa moyoni mwake.
Wajenzi wa namna mbili
(Mat 7:24-27)
46“Mbona mwaniita ‘Bwana, Bwana,’ na huku hamtimizi yale ninayosema? 47Nitawapeni mfano unaofaa kuonesha alivyo yeyote yule anayekuja kwangu, akasikia maneno yangu na kuyatimiza: 48Huyo anafanana na mtu ajengaye nyumba, ambaye amechimba chini na kuweka msingi wake juu ya mwamba; kukatokea mafuriko ya mto, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, lakini haukuweza kuitikisa, kwa sababu ilikuwa imejengwa imara. 49Lakini yeyote anayesikia maneno yangu asifanye chochote, huyo anafanana na mtu aliyejenga nyumba juu ya udongo, bila msingi. Mafuriko ya mto yakatokea, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, ikaanguka na kuharibika kabisa!”

Currently Selected:

Luka 6: BHND

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy