YouVersion Logo
Search Icon

Isaya 45

45
Mwenyezi-Mungu amteua Koreshi
1Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya Koreshi:
“Wewe ni mfalme wangu niliyekuteua;
mimi naitegemeza nguvu yako
ili uyashinde mataifa mbele yako,
na kuzivunja nguvu za wafalme.
Mimi nayafungua malango ya mji mbele yako,
na hakuna lango litakalofungwa.
2Mimi nitakutangulia,
na kuisawazisha milima mbele yako.
Nitaivunjavunja milango ya shaba,
na kuvikatakata vizuizi vyake vya chuma.
3Nitakupa hazina zilizofichwa gizani,
na mali iliyo mahali pa siri,
upate kutambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu,
Mungu wa Israeli, ninayekuita kwa jina lako.
4Kwa ajili ya mtumishi wangu Yakobo,
naam, kwa ajili ya mteule wangu Israeli,
nimekuita kwa jina lako;
nimekupa jina la heshima ingawa wewe hunijui.
5“Mimi ni Mwenyezi-Mungu, wala hakuna mwingine;
hakuna Mungu mwingine ila mimi.
Ninakuimarisha ingawa wewe hunijui,
6ili watu wote, toka mashariki hadi magharibi,
wajue kwamba hakuna Mungu mwingine ila mimi;
mimi ni Mwenyezi-Mungu na hakuna mwingine.
7Mimi hufanya mwanga na kuumba giza;
huleta fanaka na kusababisha balaa.
Mimi Mwenyezi-Mungu hutenda vitu hivi vyote.
8Enyi mbingu, nyesheni kutoka huko juu,
mawingu na yadondoshe uadilifu;
dunia na ifunuke, ichipushe wokovu,
na kuchanusha uadilifu pia!
Mimi, Mwenyezi-Mungu nimefanya hayo.”
Uwezo mkuu wa Mungu
9 #45:9 Taz Isa 29:16; Rom 9:20 Ole wake mtu ashindanaye na Muumba wake,
mtu aliye chombo cha udongo
kushindana na mfinyanzi wake!
Je, udongo humwuliza anayeufinyanga:
“Unatengeneza nini hapa?”
Au kumwambia, “Kazi yako si kamili!”
10Ole wake mtoto amwambiaye baba yake,
“Kwa nini umenizaa?”
Au amwambiaye mama yake,
“Ya nini umenileta duniani?”
11Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli,
Mungu, Muumba wa Israeli asema:
“Je, mwathubutu kuniuliza juu ya watoto wangu,
au kuniamuru juu ya kazi zangu mwenyewe?
12Ni mimi niliyeifanya dunia,
na kuumba binadamu aishiye humo.
Mikono yangu ndiyo iliyozitandaza mbingu,
na jeshi lote la nyota liko kwa amri yangu.
13Ni mimi niliyemwamuru Koreshi kuchukua hatua,
atekeleze matakwa yangu.
Nitazifanikisha njia zake zote;
ataujenga upya mji wangu Yerusalemu,
na kuwapa uhuru watu wangu walio uhamishoni,
bila kutaka malipo wala zawadi.”
Mwenyezi-Mungu wa majeshi amesema.
14Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Utajiri wa Misri na bidhaa za Kushi,
pamoja na za watu wa Seba, majitu marefu,
zitakuja kwako mwenyewe wewe taifa la Israeli,
zote zitakuwa mali yako.
Watu hao watakutumikia wamefungwa minyororo;
watakusujudia na kukiri wakisema:
‘Kwako kuna Mungu wa kweli,
wala hakuna Mungu mwingine ila yeye.’”
15Kweli wewe ni Mungu uliyefichika,
Mungu wa Israeli, Mungu Mwokozi.
16Watengenezaji sanamu wataaibika na kufadhaika,
wote kwa pamoja watavurugika.
17Lakini taifa la Israeli litaokolewa na Mwenyezi-Mungu,
litapata wokovu wa milele.
Halitaaibishwa wala kufadhaishwa milele.
18Mwenyezi-Mungu, Mungu pekee,
ndiye aliyeiumba dunia,
ndiye aliyeiumba na kuitegemeza.
Hakuiumba iwe ghasia na tupu,
ila aliiumba ikaliwe na viumbe vyake.
Yeye asema sasa:
“Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu,
wala hakuna mwingine.
19Mimi sikunena kwa siri,
wala katika nchi yenye giza.
Mimi sikuwaambia wazawa wa Yakobo
wanitafute katika ghasia.
Mimi Mwenyezi-Mungu husema ukweli,
maneno yangu ni ya kuaminika.”
20Enyi watu wa mataifa mliosalia,
kusanyikeni pamoja mje!
Nyinyi mmekosa akili:
Nyinyi mwabeba sanamu za miti
na kumwomba mungu asiyeweza kuokoa watu.
21Semeni wazi na kutoa hoja zenu;
shaurianeni pamoja!
Ni nani aliyetangaza zamani matukio ya sasa?
Ni nani aliyetamka mambo haya zamani?
Je, haikuwa mimi Mwenyezi-Mungu?
Hakuna Mungu mwingine ila mimi!
Mimi ni Mungu wa haki na mwokozi;
hakuna mwingine ila mimi.
22Nigeukieni mimi mpate kuokolewa,
popote mlipo duniani.
Maana mimi ni Mungu, wala hakuna mwingine.
23 #45:23 Taz Rom 14:11; Fili 2:10-11 Mimi nimeapa kwa nafsi yangu,
ninachotamka ni ukweli,
neno langu halitarudi nyuma:
Kila binadamu atanipigia magoti,
kila mtu ataapa uaminifu.
24“Watasema juu yangu,
‘Haki na nguvu viko kwa Mwenyezi-Mungu peke yake.’”
Wote waliomwakia hasira Mwenyezi-Mungu
watamjia yeye na kuaibishwa.
25Lakini wazawa wa Israeli
watapata ushindi kwake Mwenyezi-Mungu na kufurahi.

Currently Selected:

Isaya 45: BHND

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy