YouVersion Logo
Search Icon

2 Wamakabayo UTANGULIZI

UTANGULIZI
Sehemu kubwa ya kitabu hiki inarudia na kueleza kinaganaga matukio yaliyotajwa katika kitabu kile cha kwanza cha Wamakabayo. Kitabu kinazungumzia hali ilivyokuwa tangu utawala wa Seleuko 1V ambaye alimtangulia Antiokio Epifane mpaka wakati wa kufa kwake kamanda Demetrio I ambaye alishindwa na Yuda Makabayo mnamo mwaka 160 K.K.
Mwandishi anatuambia katika 2:19-32 kwamba kitabu hiki ni muhtasari wa maandishi katika sehemu tano yaliyoandikwa na mtu mmoja aitwaye Yasoni wa Kurene.
Lengo la kitabu chenyewe ni kuwaalika Wayahudi wa Misri wapate nao kukumbuka kuwekwa wakfu kwa hekalu ambalo lilimalizika kujengwa upya na Yuda Makabayo yapata mwaka 165 au 164 K.K. Lengo hilo linatolewa dhahiri katika sehemu ya kwanza ya kitabu chenyewe (sura 1 na 2) na hasa katika barua mbili ambazo wakuu wa Yerusalemu wanaiandikia jumuiya ya Wayahudi kule Misri.
Sura 3–7 zaeleza jinsi Wagiriki pamoja na wale waliowaunga mkono walivyopora hazina za hekalu na kuanzisha humo ibada za kipagani, na jinsi walivyowashurutisha kwa mateso Wayahudi waaminifu waikane dini yao na kuweka mahali pake tamaduni na dini ya Kigiriki.
Sura 8–15 tunahabarishwa juu ya uasi wa silaha ulioanzishwa na Yuda Makabayo na ushindi wa kwanzakwanza dhidi ya majeshi ya Wagiriki, jambo ambalo liliwezesha kutakaswa kwa hekalu na matengenezo mapya ya ibada ya Wayahudi. Jambo moja jipya katika kitabu hiki ni ile sala ya Yuda kwa ajili ya wale waliokufa, na tambiko aliyotoa kwa faida yao. Katika sura ya 15 Yuda anaona ono la kuhani mkuu Onia na nabii Yeremia, wote wa nyakati zilizopita, wakimwomba Mungu kwa ajili ya watu walio hatarini.

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy