YouVersion Logo
Search Icon

2 Wamakabayo 2

2
Yeremia aficha Hema
1“Kutokana na kumbukumbu za maandishi tunajua kwamba nabii Yeremia aliwaagiza watu waliokuwa wanapelekwa uhamishoni wafiche kiasi fulani cha moto wa madhabahuni, kama tulivyokwisha eleza. 2Tunajua kwamba baada ya kuwapa sheria aliwaagiza hao waliokuwa wanachukuliwa mateka wasisahau amri za Bwana au kupotoshwa fikira zao wakiona sanamu za dhahabu na fedha na mapambo yake. 3Kwa maneno kama hayo aliwahimiza waiweke sheria mioyoni mwao.
4“Kumbukumbu hizohizo zinatuambia pia kwamba Yeremia, akiongozwa na Mungu, aliamuru hema la mkutano na sanduku la agano, vifuatane naye hadi mlimani mahali ambako Mose alikuwa amesimama zamani na kuiangalia chini ile nchi waliyoahidiwa watu wetu na Mungu. 5Yeremia alipofika mlimani, aliona pango kubwa, akaficha humo pangoni lile hema la mkutano, lile sanduku la agano na madhabahu ya kufukizia ubani. Halafu akaziba mlango wa pango.
6“Baadhi ya marafiki zake walijaribu kumfuata Yeremia na kutia alama njia aliyopita; hata hivyo, hawakufaulu kuligundua pango hilo. 7Yeremia aliposikia kwamba wamefanya hivyo, aliwakemea, akisema: ‘Mahali hapo patabaki siri, mpaka Mungu atakapowakusanya tena pamoja watu wake na kuwaonesha huruma. 8Wakati huo Bwana atawafichulia vitu hivyo, na utukufu wa Bwana na lile wingu vitaonekana, kama ilivyokuwa wakati wa Mose, na kama Solomoni aliposali ili hekalu liwekwe wakfu kwa utukufu.’
Solomoni alivyoadhimisha sikukuu
9“Pia imeandikwa katika kumbukumbu ya maandishi jinsi Solomoni, mfalme mwenye hekima, alivyotoa tambiko wakati wa kutabaruku hekalu, baada ya kumaliza kulijenga, 10na kwamba aliposali, moto ulishuka kutoka mbinguni, ukateketeza tambiko, kama ilivyokuwa imetokea zamani wakati Mose aliposali. 11Mose alikuwa ameeleza kwamba tambiko ya kuondoa dhambi iliteketezwa kwa moto kwa sababu haikuwa imeliwa. 12Solomoni aliadhimisha sikukuu hiyo kwa muda wa siku nane.
Maktaba ya Nehemia
13“Mambo hayo yameandikwa pia katika kumbukumbu za mfalme na kumbukumbu za Nehemia ambaye alianzisha maktaba na kukusanya maandishi ya Daudi, barua za wafalme kuhusu tambiko na vitabu juu ya wafalme na manabii. 14Yuda pia alikusanya vitabu vilivyokuwa vimetapanywa kwa sababu ya vita; vitabu hivyo tunavyo bado. 15Kama mnavihitaji, basi, tumeni watu waje kuvichukua.
Mwaliko wa kuadhimisha sikukuu
16“Kwa kuwa hivi karibuni tutaadhimisha sikukuu ya utakaso, tunawaandikieni kuwashauri nanyi mwadhimishe sikukuu hiyo. 17Mungu amewaokoa watu wake wote, na ameturudishia sisi sote nchi yetu takatifu, ufalme, ukuhani, na huduma za hekalu, 18kama alivyoahidi katika sheria. Ametuokoa katika maovu ya hatari, akalitakasa hekalu, nasi tunatumaini kwamba kwa huruma yake atatukusanya hivi punde katika hekalu takatifu kutoka kila taifa ulimwenguni.”
Utangulizi wa mtunzi
19Yasoni wa Kurene ameandika, katika juzuu tano, habari ya Yuda Makabayo na nduguze, utakaso wa hekalu kuu, na kuwekwa wakfu kwa madhabahu yake. 20Amesimulia mapambano dhidi ya Antioko Epifane na dhidi ya mwanawe, Eupatori, 21na ameeleza juu ya maono ya mbinguni waliyopata wale waliopigana kufa na kupona kuitetea dini ya Kiyahudi. Idadi ya askari wetu ilikuwa ndogo. Hata hivyo, waliiteka nchi nzima na kuyafukuzia mbali majeshi ya mataifa mengine. 22Walilitwaa tena hekalu lililojulikana duniani kote, wakaukomboa mji wa Yerusalemu, na kukaza tena sheria zilizokuwa katika hatari ya kufutwa. Walifanikiwa kufanya hayo yote kwa sababu Bwana alikuwa mwema na mwenye huruma kwao.
23Sasa nitajaribu kuandika kwa muhtasari katika kitabu kimoja yale yaliyoandikwa na Yasoni katika juzuu tano. 24Maana wingi wa mahesabu uliomo na masimulizi yake mengi huweza kumtatanisha na kumchosha yeyote yule anayetaka kuelewa historia hiyo. 25Mimi lakini nimejaribu kurahisisha mambo kwa ajili ya wasomaji: Wale wanaosoma kwa kujifurahisha wataburudika, na wale wanaotaka kujifunza mambo yaliyotukia hawataona ugumu. 26Kuandika muhtasari kama huo ni kazi ngumu, inayodai mmoja atoke jasho na kukesha usiku. 27Ni ngumu kama kuandaa karamu ambayo watu wa vionjo mbalimbali watafurahia. Lakini mimi nafurahi kubeba mzigo huo ili kuwanufaisha wasomaji wangu. 28Kwa vyovyote vile, sitaandika kinaganaga; hiyo kazi namwachia yeye aliyetunga kwanza. Mimi nitajaribu kutoa muhtasari tu wa mambo yaliyotukia. 29Mimi si mjengaji wa nyumba mpya ambaye anajihusisha na kila kipengele cha jengo, bali mimi ni mpaka rangi tu ambaye kazi yangu ni kuifanya nyumba ivutie. 30Mwanahistoria ni lazima alijue somo lake, achunguze kila kipengele, na halafu aeleze kwa makini na ufasaha. 31Lakini mtu anayeandika muhtasari tu anaruhusiwa kutoa maelezo mafupi bila ya kuzama katika mjadala wa mambo. 32Kwa hiyo, basi, bila kuongeza maneno, nitaanza masimulizi yangu. Maana ni ujinga kuandika maneno mengi kwa utangulizi wa kitabu cha historia, na halafu kuifupisha historia yenyewe.

Currently Selected:

2 Wamakabayo 2: BHND

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy